Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jiografia haipaswi kuamua hatima ya nchi: Mkutano wa UN kuhusu nchi zisizo na bandari wafunguliwa Turkmenistan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika mkutano wa LLDC3 mjini Awaza, Turkmenistan.
UN Photo/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia katika mkutano wa LLDC3 mjini Awaza, Turkmenistan.

Jiografia haipaswi kuamua hatima ya nchi: Mkutano wa UN kuhusu nchi zisizo na bandari wafunguliwa Turkmenistan

Ukuaji wa Kiuchumi

Kuvunja vizingiti na kurejesha usawa katika maendeleo ya kimataifa ndilo lengo kuu la Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Nchi Zisizo na Bahari (LLDCs), Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema leo Agosti 5 wakati wa ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika katika mji wa Awaza, Turkmenistan hadi Agosti 8.

Akihimiza viongozi wa dunia kutafakari upya kuhusu maendeleo ya nchi zisizo na bandari, Guterres amesisitiza:
“Tunakusanyika leo kuthibitisha ukweli wa msingi: jiografia haipaswi kamwe kuamua hatima (ya nchi).”

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), kati ya nchi 32 zisizo na bandari duniani, 16 ziko Afrika, 10 Asia, nne Ulaya, na mbili Amerika ya Kusini. Kwa pamoja, nchi hizi zina watu zaidi ya milioni 500.

Lori linapita katika mandhari ya Tajikistan.
© UNDP/Beyond Borders Media
Lori linapita katika mandhari ya Tajikistan.

Vizingiti vya kibiashara, madeni makubwa, na ukosefu wa usawa

Guterres ameeleza changamoto kubwa zinazozikabili LLDCs ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kibiashara, gharama kubwa za usafirishaji, na ukosefu wa upatikanaji wa masoko ya kimataifa. Ameonya kuwa mzigo wa madeni kwa nchi hizi umefikia “viwango vya hatari na visivyodumu.”

Ingawa LLDCs zina asilimia 7 ya watu duniani, zinachangia zaidi kidogo ya asilimia 1 ya pato na biashara ya dunia.

“Hii ni ishara ya wazi ya ukosefu mkubwa wa usawa unaoendeleza pembezoni,” amesema Guterres, akilaani mfumo wa kiuchumi na kifedha wa kimataifa usio wa haki, ambao hauakisi uhalisia wa ulimwengu uliounganishwa wa leo, na pia urithi wa ukoloni.

Muongo wa malengo ya juu: Mpango wa Awaza wa Hatua

Mkutano huu, unaojulikana kama LLDC3, unaendelea Awaza lengo lake ni kutafuta suluhu kwa changamoto hizi.

“LLDC3 unalenga kuanzisha muongo mpya wa malengo ya juu kupitia Mpango wa Awaza wa Hatua na utekelezaji wake  na kufungua kwa ukamilifu uwezo wa maendeleo wa nchi zisizo na baharí.” amesema Guterres.

Mpango huu wa Awaza ulipitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba 2024, na unawakilisha ahadi mpya na imara ya kusaidia matarajio ya maendeleo ya LLDCs.

Bila ufikiaji wa moja kwa moja wa baharini, nchi zinazoendelea zisizo na bandari zinakabiliwa na changamoto kubwa katika biashara ya kimataifa, na kuziacha katika hatari kubwa ya soko na mshtuko wa kisiasa wa kijiografia. Pichani hapa, wanawake wakulima …
© WFP/JohnPaul Sesonga
Bila ufikiaji wa moja kwa moja wa baharini, nchi zinazoendelea zisizo na bandari zinakabiliwa na changamoto kubwa katika biashara ya kimataifa, na kuziacha katika hatari kubwa ya soko na mshtuko wa kisiasa wa kijiografia. Pichani hapa, wanawake wakulima nchini Rwanda.

Vipaumbele vinne kwa maendeleo

Guterres ametaja vipaumbele vinne vya msingi:

  1. Kuharakisha mabadiliko ya kiuchumi na kidijitali
    • Kuwekeza katika viwanda vya kuongeza thamani, ubunifu wa ndani, na ukuaji shirikishi
    • Kuzuia pengo la kidijitali ili kufungua fursa za Akili Unde, AI, biashara mtandaoni, na mifumo ya kisasa ya usafirishaji
  2. Kuimarisha biashara, usafirishaji, na muunganisho wa Kanda
    • Kuboresha miundombinu na kurahisisha taratibu za mipakani
    • Kuingiza LLDCs katika minyororo ya thamani duniani na kufanya mageuzi ya mifumo ya biashara
  3. Kusukuma hatua za hali ya hewa na uhimilivu
    • Kuongeza mara mbili fedha za mabadiliko ya tabianchi na kujenga miundombinu inayohimili hali ya hewa
    • Kusaidia LLDCs katika mpito wa kijani kupitia teknolojia na ushirikiano
  4. Kuhamasisha fedha na fshirikiano
    • Kufanya mageuzi ya mifumo ya kifedha ya kimataifa ili kuhakikisha fedha za haki na rahisi kufikiwa
    • Kuongeza fedha za masharti nafuu na kufungua uwekezaji wa tabianchi kwa kasi

“Ufanisi wa nchi zisizo na Bahari ni muhimu kwa mafanikio ya Ajenda ya 2030,” Guterres amesisitiza akiongeza kwamba, “tuna maarifa, na tuna nyenzo… Pamoja, tunaweza kubadilisha jiografia kutoka kikwazo hadi daraja  si tu kuunganisha masoko, bali pia watu na tamaduni zinazotoa maana kwa maendeleo.”

Ushirikiano wa kikanda na mshikamano wa kimataifa

Baada ya hotuba yake, Guterres aliwaambia waandishi wa habari kuwa mkutano huu unaakisi enzi mpya ya ushirikiano inayoanza kuchipua Asia ya Kati  iliyojaa uaminifu wa pamoja, vipaumbele vya pamoja, na mshikamano wa kikanda unaokua.

“Wakati ushirikiano wa kimataifa unapopitia majaribu, roho hii ya ushirikiano ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote,” amesema.

 Kyrgyzstan ni nchi yenye milima katika Asia ya Kati. Inashiriki mipaka na Uchina, Kazakhstan, Tajikistan, na Uzbekistan na haina ufikiaji wa moja kwa moja wa bahari.
© Unsplash/Jairph
Kyrgyzstan ni nchi yenye milima katika Asia ya Kati. Inashiriki mipaka na Uchina, Kazakhstan, Tajikistan, na Uzbekistan na haina ufikiaji wa moja kwa moja wa bahari.

Masuala ya kikanda yatajwa, mshikamano wa kimataifa wahimizwa

Mkutano umefunguliwa na Rais wa Turkmenistan, Serdar Berdimuhamedov, aliyesisitiza juhudi za taifa lake katika kushirikiana kimataifa kuhusu afya, hatua za tabianchi, na ulinzi wa mazingira.

Amegusia pia changamoto za kikanda kama vile kukauka kwa Bahari ya Aral na kushuka kwa kiwango cha maji katika ‘Bahari ya Caspian’ ambayo ni hifadhi kubwa zaidi ya maji baridi duniani na eneo la mkutano huu wa tatu wa LLDCs.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Philemon Yang, ameonya kuhusu tarehe ya ukomo inayokaribia kwa Ajenda ya 2030, na kutoa wito kwa hatua madhubuti na ahadi mpya kwa ushirikiano wa kimataifa.

Amesisitiza kuwa nguzo tatu za Mkataba wa Umoja wa Mataifa ambazo ni amani, maendeleo, na utu wa binadamu lazima ziendelee kuwa msingi wa juhudi zote, na kwamba ahadi ya kutomwacha mtu nyuma lazima ionekane katika vitendo.

Akitambua udhaifu wa LLDCs dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kimfumo, Yang alisema nchi hizi “hazipaswi kukosa fursa, ustawi, wala matumaini”, akatoa wito kwa mshikamano wa kimataifa, uwekezaji wa miundombinu, na utekelezaji wa uhuru wa kupitisha bidhaa.

Pia ametangaza kuwa tarehe 6 Agosti imetangazwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Uhamasishaji kuhusu Nchi Zisizo na Bahari, ambayo itaadhimishwa kila mwaka.

“Baraza Kuu litaendelea kuwa jukwaa la kimataifa la kuzisaidia nchi hizi,” amesisitiza, akieleza umuhimu wa kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Awaza na kujiandaa kwa mapitio ya ngazi ya juu mwaka 2029.