Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Afrika yaanza kutengeneza dawa za kukabiliana na UKIMWI

Wanawake wanapokea tiba ya kurefusha maisha ya VVU katika kliniki katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria. (Maktaba)
© UNICEF/Adeokun Adesegun
Wanawake wanapokea tiba ya kurefusha maisha ya VVU katika kliniki katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria. (Maktaba)

Afrika yaanza kutengeneza dawa za kukabiliana na UKIMWI

Afya

Nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimepiga hatua muhimu na ya tahadhari kuelekea kujitegemea zaidi katika masuala ya afya kupitia hatua ya hivi karibuni zaidi ya kutengeneza dawa za kukabiliana na Virusi Vya Ukimwi, (VVU). Kama hiyo haitoshi vifaa vya uchunguzi vimeanza kupatikana katika programu za kitaifa. Dawa hizo zimenunuliwa kwa ajili ya Msumbiji.

Maendeleo haya ni hatua kubwa kwa bara ambalo linabeba karibu asilimia 65 ya mzigo wa VVU duniani na kwa muda mrefu limekuwa likitegemea uagizaji wa dawa muhimu za kufifisha VVU, (ARVs) na vifaa vya kupima. Lakini hali hiyo inaweza kuanza kubadilika.

Virusi vya UKIMWI (VVU) hudhoofisha kinga ya mwili, na kupunguza uwezo wake wa kupambana na maambukizi na aina fulani za saratani. Bila matibabu ya wakati, inaweza kusababisha ugonjwa wa Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) ambayo ni hatua ya juu zaidi ya maambukizi.

Mnamo mwaka 2023, kampuni ya dawa ya Universal Corporation Ltd iliyoko Kenya ikawa mzalishaji wa kwanza wa Kiafrika kupata kibali cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya (WHO)na kuzalisha TENOFOVIR DISOPROXIL FUMARATE, LAMIVUDINE na DOLUTEGRAVIR (TLD) - dawa ya kwanza ya kufifisha VVU.

Sasa, katika hatua kubwa mbele, Mfuko wa Kimataifa (Global Fund) ambao ni ushirikiano wa kimataifa unaofadhili mapambano dhidi ya VVU, Kifua Kikuu na Malaria - unanunua dawa hizi za VVU zilizotengenezwa barani Afrika  kwa ajili ya Msumbiji. Hii inaifanya kuwa mara ya kwanza TLD iliyotengenezwa Afrika kutumiwa kupitia njia hii.

"Ununuzi wa dawa za VVU zilizotengenezwa Afrika kwa ajili ya Msumbiji ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha mifumo ya usambazaji barani Afrika," amesema Meg Doherty, Mkurugenzi wa Mpango wa VVU wa WHO.

 

"Hii itachangia matokeo bora ya kiafya kwa watu wanaoishi na VVU ambao wanahitaji upatikanaji wa dawa bila kukatizwa."

Kujenga uwezo wa kikanda

WHO inasema mafanikio haya ni sehemu ya juhudi pana za kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani na kuboresha upatikanaji wa teknolojia muhimu za kiafya kote Afrika.

Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limekuwa likishirikiana na nchi, wazalishaji na mashirika,Mifuko ya afya duniani - ikiwemo Global Fund na Unitaid - ili kupanua uzalishaji wa Kiafrika wenye uhakika wa ubora.

"Uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya zenye uhakika wa ubora ni kipaumbele cha dharura," amesema Rogerio Gaspar, Mkurugenzi wa Udhibiti na Uidhinishaji wa WHO.

"Kwa kila mzalishaji wa Kiafrika anayefikia viwango vya uidhinishaji vya WHO, tunasonga karibu na mfumo wa afya unaojitegemea zaidi, imara na wenye usawa."

Licha ya maendeleo, bado kuna changamoto

Licha ya hatua hii muhimu, WHO imeonya kuwa uzalishaji pekee hautoshi. Ili kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu, shirika hilo linataka kuwepo kwa ahadi za soko la juu, sera za ununuzi wa haki na msaada wa kiufundi unaoendelea.

WHO pia imeeleza kuwa vifaa vya uchunguzi ni pengo muhimu. Kwa mabadiliko ya ufadhili kutoka kwa wafadhili, nchi nyingi ziko chini ya shinikizo la kudumisha programu za kupima VVU, ambazo ni mstari wa mbele katika kuzuia na kutibu.

Katika juhudi zinazohusiana, Codix Bio, kampuni ya vifaa vya uchunguzi kutoka Nigeria, hivi karibuni ilipata leseni ya kuzalisha vifaa vya haraka vya kupima VVU. 

"Kuwa na vifaa vya haraka vya kuchunguza VVU vilivyotengenezwa ndani ya Afrika kutasaidia kuongeza uwezo wa kumudu, na kwa ujumla kushughulikia udhaifu wa usambazaji na ucheleweshaji wa upatikanaji wa vifaa vya uchunguzi," amesema Dk. Doherty.

Kudumisha mafanikio katikati ya ukata

Kama sehemu ya mwongozo wake, WHO imehimiza pia nchi kutumia vipimo vya VVU vya haraka, vya bei nafuu na vilivyoidhinishwa na shirika hilo, hasa kama kipimo cha kwanza katika kanuni za kitaifa, ambacho kinaweza kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa huku huduma zikiendelea kutolewa.

Ingawa taarifa za hivi karibuni zinaonesha maendeleo dhahiri, hatua zaidi zinahitajika.

"TLD iliyotengenezwa ndani ya Afrika ni hatua kubwa kuelekea lengo hilo," WHO imesema ikiongeza kuwa, "lakini hatua zaidi zinahitajika."