Uganda: Kupungua kwa ufadhili, takribani wakimbizi milioni mbili hatarini - UNHCR
Uganda: Kupungua kwa ufadhili, takribani wakimbizi milioni mbili hatarini - UNHCR
Uganda iko katika hatihati ya kulazimika kufikia kuwahifadhi wakimbizi milioni mbili kutokana na migogoro inayoendelea Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kuwasukuma mamia ya watu kuvuka mpaka kila siku wakitafuta usalama na misaada ya kuokoa maisha. Hata hivyo, jitihada za kibinadamu kwa sasa zinakabiliwa na moja ya majanga makubwa ya kifedha kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa, imeeleza taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR iliyotolewa leo Agosti 4.
UNHCR inaeleza kwamba tangu mwanzo wa mwaka 2025, wastani wa watu 600 wamekuwa wakiwasili Uganda kila siku, na idadi hiyo inatarajiwa kufikia milioni mbili kufikia mwisho wa mwaka. Uganda, ambayo tayari ni nchi inayoongoza barani Afrika kwa kuwahifadhi wakimbizi na ya tatu duniani kwa ujumla, kwa sasa inawahifadhi wakimbizi milioni 1.93, zaidi ya milioni moja kati yao wakiwa ni watoto walio na umri chini ya miaka 18. Miongoni mwao, zaidi ya watoto na vijana 48,000 wamewasili wakiwa peke yao.
“Nilikutana na msichana mwenye umri wa miaka 16 aliyeikimbia Sudan Kusini kutokana na machafuko na sasa anawatunza wadogo zake wanne baada ya kupoteza wazazi wake. Ana ndoto ya kurejea shule, lakini kwa sasa anawaza tu kuhusu kuishi. Fedha za dharura zitakwisha mwezi Septemba. Watoto zaidi watakufa kwa utapiamlo, wasichana zaidi watakumbwa na ukatili wa kingono, na familia zitabaki bila makazi wala ulinzi kama dunia haitachukua hatua,” amesema Dominique Hyde, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Nje wa UNHCR, ambaye alitembelea makazi ya wakimbizi wanaotoka Sudan na Sudan Kusini nchini Uganda hivi karibuni.
Sera ya Uganda ya kuwajumuisha wakimbizi inawaruhusu kuishi, kufanya kazi na kupata huduma za umma, lakini upungufu wa ufadhili unaathiri kwa kiwango kikubwa utoaji wa misaada na unatishia kufuta mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mingi. Gharama ya kuhudumia mkimbizi mmoja nchini Uganda inakadiriwa kuwa karibu dola 16 kwa mwezi mwaka 2025. Hata hivyo, isipokuwa UNHCR ipate ufadhili zaidi, itaweza kutoa msaada wa dola 5 tu kwa kila mkimbizi kwa mwezi. Hali hii inasababisha upungufu wa chakula, maji, na dawa, huku viwango vya utapiamlo hasa kwa watoto walio chini ya miaka mitano vikiongezeka kwa kasi ya kutisha.
Uwezekano wa kujiua
Kadri rasilimali zinavyozidi kuzidiwa, wakimbizi wanalazimika kufanya uamuzi mgumu ya kubadili maisha yao ili kuendelea kuishi, ikiwa ni pamoja na kuacha shule. Ripoti za ukatili wa kijinsia zinaongezeka, na pia kuna ongezeko la hatari ya kujiua miongoni mwa vijana wa kimbizi kutokana na kupungua kwa watumishi wa huduma za afya ya akili.
Kufikia mwisho wa Julai mwaka huu 2025, UNHCR ilikuwa na rasilimali za kusaidia watu chini ya 18,000 kwa kuwapa fedha taslimu na misaada ya msingi, kiwango ambacho kinatosha tu kwa kipindi cha miezi miwili kwa waliofika hivi karibuni kwa kasi ya sasa.
Hyde ameongeza kwamba, “vita huvuruga maisha ghafla, na kulazimisha watu kuacha kila kitu nyuma. Wakimbizi wengi wanakumbwa na hali ya kukata tamaa; hakuna uimara unaoweza kuchukua nafasi ya yote yaliyopotea. Uganda imeonesha ukarimu mkubwa, lakini mzigo huu haupaswi kubebwa na jamii zilizo mbali na maeneo ya migogoro pekee. Wajibu uko kwa wale wanaosababisha au kuchochea machafuko. Amani ndiyo suluhisho la kudumu, na hadi ifikie, heshima ya wakimbizi lazima ilindwe.”
Kwa sasa, mwitikio wa Uganda kwa wakimbizi umefadhiliwa kwa asilimia 25 tu. UNHCR inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msaada wa haraka na endelevu, ikiwa ni pamoja na taasisi za maendeleo, ili kuhakikisha wakimbizi na jamii zinazowahifadhi wanaishi maisha salama na yenye heshima zaidi.