Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

"Kila siku tunalala njaa" asema mfanyakazi wa UNRWA huko Gaza

Wapalestina waliokimbia makazi yao hukusanyika katika jiko la jamii katika Jiji la Gaza kupokea dengu kama sehemu ya usambazaji wa chakula cha msaada.
UN News Kundi la wakimbizi wa ndani wa kipalestina wakigombania chakula kwenye jiko la kijamii huko Mashariki mwa Ukanda wa Gaza.

"Kila siku tunalala njaa" asema mfanyakazi wa UNRWA huko Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Wakazi wa kawaida wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli,  wakikumbwa na njaa na misaada ya kibinadamu haitoshi, mfanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Manar, anatoa ushuhuda kuhusu maisha magumu ya kila siku ya wapalestina ambao mara nyingi wanalazimika kulala njaa.

Kulingana na mfanyakazi huyo wa UNRWA, kufurushwa, njaa, na uchovu vimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. "Kila siku naamka bila kujua nini kitatokea," amesema katika ushuhuda uliochapishwa na UNRWA kwenye mtandao wa X zamani Twitter.

"Tulilazimika kukimbia kutoka nyumbani kwetu na tangu wakati huo hatujawahi kujisikia salama. Na hofu bado ipo: hofu ya mabomu mapya, hofu ya kumpoteza mtu, hofu ya kulazimika kuhama tena."

Watoto wetu wanalia kwa sababu wana njaa

Ingawa bado anaendelea kufanya kazi, maji safi na chakula ni haba. "Ninaenda kazini, lakini moyo wangu uko na watoto wangu. Hata mambo rahisi sasa yamekuwa magumu sana," anasema.

Katika maisha haya ya kila siku yaliyojaa kukata tamaa, hata mahitaji ya msingi ni anasa. "Mara nyingi, hakuna maji ya kupikia au ya kuoga. Chakula hakitoshi kamwe."  Wakati bahati inapotokea, familia hizi zilizokata tamaa huweza kupika wali. Lakini mara nyingi, Manar na jamaa zake hulala "wakiwa na njaa." "Watoto wetu wanalia kwa sababu wana njaa. Kama mama, moyo wangu huvunjika."

Manar pia anaelezea jinsi wanavyohangaika kutafuta dawa katikati ya uhaba unaosababishwa na vizuizi vya Israeli.

Kwa ujumla, kama Manar, mamilioni ya wakaazi wa Gaza wanatembea "kwa saa kadhaa chini ya jua kali kutafuta mahitaji ya msingi."

"Hakuna magari, hakuna mabasi, hakuna msaada. Tumechoka, kimwili na kihisia. Lakini tunaendelea. Sio siku tu – huu ndio maisha yetu," anahitimisha.

Mwanamke aliyevaa hijab anamhudumia msichana mdogo mwenye utapiamlo mkali katika mazingira ya kliniki.
© WHO Msichana aliyedhoofika sana kwa utapiamlo huko Gaza. Mashirika ya misaada yamekuwa yakiitaka Israel mara kwa mara iruhusu misaada zaidi kuingia Gaza ili kuzuia janga la kibinadamu linaloendelea.

Wafanyakazi wa misaada wazimia kwa njaa

Ushuhuda wa Manar unakuja wiki mbili baada ya onyo kama hilo kutoka UNRWA, likisema ilipokea "jumbe za kutisha za njaa" kutoka ndani ya Gaza – kutoka kwa raia na hata wafanyakazi wake walioko mashinani.

“Nilitafuta kitu cha kuwalisha watoto wangu, lakini hakuna kitu. Kila siku, tunapokea jumbe za kuomba msaada kutoka kwa wenye njaa na hata kutoka kwa wenzetu UNRWA. Tunawezaje kujibu jumbe kama hizo za kukata tamaa? Hili linanitia aibu na kuongeza zaidi hisia za kushindwa," amesema Philippe Lazzarini, Kamishna Mkuu wa UNRWA, kwenye mtandao wa X, akieleza kwamba "mamlaka za Israeli zinawanyima raia chakula, wakiwemo watoto milioni moja."

"Hakuna anayesamehewa: hata wale wanaowatunza watoto huko Gaza nao wanahitaji kutunzwa. Madaktari, wauguzi, waandishi wa habari, na wafanyakazi wa misaada nao pia wana njaa," amesema Lazzarini, akiongeza kwamba "watu wengi wanazimia kwa njaa na uchovu wanapotekeleza majukumu yao – iwe ni kuripoti mauaji au kupunguza mateso."

Mateka waachiliwe huru bila masharti - OHCHR/WHO/OCHA

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii kumechapishwa video za raia wa Israeli waliotekwa na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas Oktoba 7, 2023, picha zikionesha wamekonda na wako katika hali mbaya kiafya.

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk ametoa taarifa kuelezea masikitiko yake kuhusu picha za watu wanaokufa kwa njaa huko Ukanda Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, halikadhalika video hizo za mateka wa Israeli wanaoshikiliwa na wanamgambo wa kipalestina, Hamas huko Gaza.

“Picha za watu wanaokufa kwa njaa huko Gaza ni za kuhuzunisha na hazivumiliki. Kufika hatua hii ni dhihaka kwa utu wetu wa pamoja. Hili linatukumbusha tena kwamba ghasia lazima zikome mara moja. Kipaumbele cha kila mmoja wetu kinapaswa kuwa kuokoa maisha,” Bwana Türk kupitia taarifa iliyotolewa na ofisi yake mchana wa Jumatatu Agosti, 4 huko Geneva, Uswisi.

Amesema Israeli inapaswa kuruhusu na kuwezesha mara moja kupitishwa kwa haraka na bila vikwazo kwa kiasi cha kutosha cha msaada wa kibinadamu kwa raia wanaohitaji, ili kuepuka mateso na vifo visivyo vya lazima. Kuwanyima raia chakula kunaweza kuwa uhalifu wa kivita, na huenda pia kuwa uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kuhusu video za mateka wa kiyahudi waliodhoofika kwa njaa zilizochapishwa na makundi ya wapiganaji wa kipalestina, Kamishna Mkuu huyo amesema, “zinatisha, na ninakereka sana na namna ya kuaibisha wanavyotendewa. Wanapaswa kuruhusiwa kupokea msaada mara moja kutoka Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu.”

Amerejelea wito wake wa kutaka mateka na wote waliokamatwa kiholela lazima waachiwe huru mara moja na bila masharti. “Wote walionyimwa uhuru wao wanapaswa kutendewa kwa utu na wasitumike kamwe kama silaha ya kisiasa au chombo cha mashinikizo,” imetamatisha taarifa hiyo.

Kufuatia video hizo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, (WHO) Dkt. Tedros Ghebreyesus ametaka mateka hao waachiliwe huru haraka na bila masharti yoyote.

“Tunasisitiza mateka wote wapatiwe chakula na matibabu na wasinyanyaswe,”  amesema Dkt. Tedros kupitia mtandao wa X.

Naye Mkuu wa Ofisi ya  Umoja wa Mataifa ya kuratibu Misaada ya Dharura, OCHA. Tom Fletcher amesema, “Tunachukizwa na video za hivi karibuni zilizochapishwa zikionesha mateka wa Israeli wanaoshikiliwa Gaza. Tangu siku ya kwanza tulisema na tunasisitiza, mateka lazima waachiliwe huru, haraka na bila masharti.”

Watu 100 wauawa katika siku mbili pekee wakisaka chakula

Ijumaa iliyopita Umoja wa Mataifa uliripoti kuwa zaidi ya watu 100 waliuawa na mamia kadhaa walijeruhiwa katika siku mbili pekee Wakisaka chakula.

Miongoni mwa waliouawa Ijumaa wakisaka chakula kwa ajili ya familia zao ni baba mzazi wa Mohammed Mudeiris ambaye. Akiwa amebeba kibakuli na amekinyanyua juu, Mohammed anasema, mimi ndiye mtoto mkubwa kwa baba yangu ambaye aliuawa kwa kombora la angani jana, Najaribu kuomba mtu yeyote anipatie kibakuli cha unga au chakula kutoka kwenye malori yenye misaada yaliyowasili leo, ambayo tunayaona kwa mara ya kwanza.

Gaza kuna vituo vitatu tu vya kugawa chakula vinavyoratibiwa na Marekani na Israeli na kwa kutazama kauli ya mwenye nguvu mpishe ndio inayoonekana kwani kwa wanawake na watoto kupata chakula ni changamoto.

Wapalestina wakiwa wamebeba magunia ya unga mabegani mwao karibu na kivuko cha Zikim kaskazini mwa Gaza.
UN News

Tunakumbuka Umoja wa Mataifa

Abir Safi mkimbizi wa ndani kutoka kitongoji cha Al -Zaytoun akizungumza kwa uchungu anakumbuka hali ya zamani akisema , "hapo awali Umoja wa Mataifa walikuwa wanasambaza misaada, na nilipata kwa urahisi. Sasa hivi sipati chochote. Nahatarisha maisha yangu kwenda Zikim na kurejea patupu. Nataka nirejee nyumbani kwa wanangu nikiwa nina chakula. Hivi sasa wanaonufaika ni wafanyabiashara na wezi. Mimi ni mjane, nimekonda na afya yangu inazorota, hakuna anayetujali isipokuwa Mungu. Nataka utu wangu. Nataka nipate msaada kupitia Umoja wa Mataifa.”

WHO na misaada iliyowasilishwa

Hadi Jumamosi Agosti 2, WHO ilikuwa imeingiza Gaza malori 24 yaliyojaa vifaa vya matibabu. Vifaa hivyo vinajumuisha dawa muhimu, vifaa vya kutibu majeraha na upasuaji, matibabu kwa magonjwa yasiyoambukiza, pamoja na vifaa vya maabara na vipimo vya maji.

Vifaa hivyo vitapelekwa katika vituo vya afya na kwa washirika wa sekta ya afya katika siku zijazo.

Dkt. Tedros ametoa shukrani kwa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa msaada wao. “Tunatoa wito wa kuendelezwa kwa uingizaji wa misaada bila vikwazo, tena kwa wingi na kwa kasi. Maisha ya watu katika Gaza yanategemea msaada huu.”