Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa kipindupindu Darfur: Watoto zaidi ya 640,000 wako hatarini

Watoto na watu wazima wanaougua kipindupindu wanapokea matibabu katika kituo cha kujitenga katika hospitali moja mjini Khartoum, Sudan. Hali ni ya kutisha hasa katika eneo la Darfur Kaskazini, ambako zaidi ya watoto 640,000 wako hatarini.
© UNICEF/Ahmed Mohamdeen Elfatih Watoto na watu wazima wanaougua kipindupindu wanapokea matibabu katika kituo cha kujitenga katika hospitali moja mjini Khartoum, Sudan. Hali ni ya kutisha hasa katika eneo la Darfur Kaskazini, ambako zaidi ya watoto 640,000 wako hatarini.

Mlipuko wa kipindupindu Darfur: Watoto zaidi ya 640,000 wako hatarini

Afya

Zaidi ya watoto 640,000 walio na umri wa chini ya miaka mitano wapo hatarini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu huko Kaskazini mwa Darfur, nchini Sudan. 

Taarifa iliyotolewa hapo jana kutoka Port Sudan na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, inatoa wito wa upatikanaji wa huduma za kibinadamu bila vikwazo ili kuzuia kusambaa kwa mlipuko wa kipindupindu ambao unaendelea kuenea kwa kasi katika eneo la Tawila, Jimboni Darfur Kaskazini, ambako hadi sasa wagonjwa zaidi ya 1,180 wameripotiwa, wakiwemo watoto 300 na vifo ni 20.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan, Sheldon Yett amesema hali ni mbaya zaidi kwa watoto zaidi ya 640,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Yett amesema, “Tunaona ugonjwa wa kipindupindu ukitishia maisha ya maelfu ya watoto, hasa wale wadogo zaidi na walio hatarini. Tunaendelea kufanya kila tuwezalo, lakini tunahitaji msaada sasa.”

Kwa ujumla, Darfur yote imeripoti karibu wagonjwa 2,140 wa kipindupindu kufikia mwisho wa mwezi Julai, huku vifo vilivyothibitishwa vikiwa ni 80.

Hospitali nyingi zimefungwa, huduma za afya na maji safi hazipatikani kwa urahisi, huku uhaba wa misaada ukichangiwa na mashambulizi dhidi ya misafara ya kibinadamu.

UNICEF inatoa wito kwa serikali na pande zote kwenye mzozo nchini Sudan kuruhusu upatikanaji salama na wa haraka wa misaada ya kuokoa maisha kwani hali ni mbaya na watoto hawawezi kusubiri tena hata siku moja.

Licha ya changamoto, UNICEF inaendelea kusambaza dawa za kumeza ambazo zinawasaidia wagonjwa kurejesha maji mwilini, dawa za kutibu kipindupindu, chanjo na vyakula lishe kwa watoto.

Hadi sasa, watu 30,000 wanapata maji safi kila siku kupitia usaidizi wa UNICEF, huku kampeni za kuelimisha jamii zikiendelea mitandaoni na ana kwa ana.