Viongozi wa dunia kukutana Turkimenistan kusaidia nchi zinazoendelea zisizo na bahari
Maandalizi ya mwisho yanaendelea katika ukumbi wa mkutano wa LLDC3 unaotarajiwa kufanyika Awaza, Turkmenistan.
Viongozi wa dunia kukutana Turkimenistan kusaidia nchi zinazoendelea zisizo na bahari
Malengo ya Maendeleo Endelevu
Mwezi huu wa Agosti kuanzia tarehe 5 hadi 8, wakuu wa nchi, mawaziri, wawekezaji na viongozi wa mashirika ya kiraia wanatarajiwa kukutana mjini Awaza, katika pwani ya Kaspi Sea nchini Turkmenistan, kwa ajili ya mkutano wa kipekee wa Umoja wa Mataifa unaolenga kubadilisha mfumo wa kimataifa ili kusaidia nchi 32 zinazoendelea zisizo na bandari, ambazo uchumi wao mara nyingi hutengwa kutokana na ukosefu wa upatikanaji wa moja kwa moja baharini.
Katika jiji la Avaza, kwenye pwani ya Kaspi, maandalizi ya mwisho yanaendelea kwa ajili ya Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa wa Nchi Zinazoendelea Zisizo na Bahari. Wakuu wa nchi na serikali zaidi ya ishirini wanatarajiwa kuhudhuria, pamoja na wajumbe 3,000 kutoka mashirika ya kimataifa, mashirika ya kiraia, vijana, wasomi na sekta binafsi. Mwandishi wa Habari wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa yupo Avaza akifuatilia maandalizi.
Jukwaa la Kimataifa
Mji wa Avaza uko katika pwani ya ‘Bahari ya Kaspi’, ingawa jina la “Kaspi Sea” linaweza kupotosha Kaspi ni ziwa, kubwa zaidi duniani, ambalo halijaunganishwa na Bahari ya Dunia, na linategemea mito kama Volga kutoka Urusi.
“Kwa sababu ya jiografia yao na gharama kubwa za usafirishaji, nchi zisizo na bandari haziwezi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa dunia,” anasema Aksoltan Atayeva, Mwakilishi wa Kudumu wa Turkmenistan katika Umoja wa Mataifa. “Gharama kubwa za biashara na usafiri huwakatisha tamaa wawekezaji, hivyo kuathiri maendeleo ya kiuchumi. Nchi hizi zinahitaji msaada wa pekee ili kushinda changamoto hizo na kuharakisha maendeleo.”
Anakumbusha kuwa katika kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, azimio lilipitishwa la kuitisha mkutano wa tatu wa kimataifa kwa ajili ya nchi hizi, na Turkmenistan ikateuliwa kuwa mwenyeji.
Maandalizi ya mwisho
Jumapili, vinywaji vya maji bado vilikuwa vinapelekwa katika uwanja mkubwa wa michezo uliogeuzwa kuwa eneo la mkutano. Mifumo ya ulinzi, skrini za televisheni na vifaa vingine vilikuwa vinafungwa. Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliowasili wiki iliyopita walikuwa wakifanya kazi usiku na mchana kuweka kamera kwa ajili ya matangazo ya moja kwa moja ya vikao, meza za majadiliano na mikutano mbalimbali, sambamba na kushirikiana na wenyeji kutatua changamoto za maandalizi.
“Nchi yetu imefanya kazi kubwa ya maandalizi kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa kuhakikisha mazingira bora kwa washiriki wa mkutano,” alisema Aksoltan Atayeva. “Tunaelewa imani kubwa ambayo jamii ya kimataifa imetuwekea, na tunafanya kila liwezekanalo kuhakikisha mafanikio ya mkutano huu.”
Kituo kipya cha Umoja wa Mataifa Kazakhstan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, anatarajiwa kuwasili Avaza Jumapili hii usiku akitokea Almaty, Kazakhstan, ambako alihudhuria uzinduzi wa Kituo cha Kikanda cha Umoja wa Mataifa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa Asia ya Kati na Afghanistan.
“Kituo hiki ni ishara ya enzi mpya ya ushirikiano wa kikanda, unaotegemea vipaumbele na suluhisho za pamoja,” alisema Guterres. Aliongeza kuwa hali ya mabadiliko ya tabianchi inachangia kupungua kwa maji, kuyeyuka kwa barafu, na majanga ya asili.
Ukame wa Ziwa Aral, alisema, unaonesha hatari za mazingira za eneo hilo, huku mvutano wa biashara na hali ya sintofahamu ya kiuchumi duniani ikizidisha changamoto.
“Jiografia ya kutokuwa na bandari ni kikwazo kikubwa kwa biashara, miunganisho, fedha na masoko ya kimataifa,” alisema. “Ndiyo maana ninafurahi sana kuwa hapa kabla ya mkutano wa tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu nchi hizo, mkutano muhimu kwa utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji wa Maendeleo yao.”
Maonyesho ya mafanikio
Katika moja ya kumbi kubwa za Avaza, nchi shiriki zinaonesha mafanikio yao katika nyanja kama usafiri, nishati, mawasiliano, na mengineyo. Maandalizi bado yanaendelea maonesho yanapangwa, vifaa vinafungwa na skrini zinawekwa.
Annaberdy Kashanov, mmoja wa maafisa wa banda la Turkmenistan, alieleza kuhusu miradi mikubwa ya usafiri ikiwemo reli ya Kazakhstan-Turkmenistan-Iran na bomba la gesi litakalounganisha Turkmenistan, Afghanistan, Pakistan na India – mradi unaojulikana kama "mradi wa karne".
Malengo ya mkutano
Kwa mujibu wa Aksoltan Atayeva, mkutano unatarajiwa kupitisha Mpango wa Utekelezaji wa Avaza kwa 2024–2034, pamoja na Tamko la Kisiasa, ambayo yatachangia maendeleo endelevu ya nchi zisizo na bandari.
Jumapili, sherehe rasmi ya kupandisha bendera za Umoja wa Mataifa na Turkmenistan ilifanyika. “Karibuni Avaza. Nawatakia mafanikio washiriki wote wa mkutano!” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Turkmenistan, Rashid Meredov.
Rabab Fatima, Mwakilishi wa Juu wa Umoja wa Mataifa kwa Nchi Maskini Zaidi, Nchi Zisizo na Bahari na Visiwa Vidogo Vinavyoendelea, ameeleza matumaini kuwa mkutano huu utaimarisha na kupanua ushirikiano baina ya nchi hizo.