Baa la njaa lazidi kunyemelea Gaza huku raia wakishambuliwa
Baa la njaa lazidi kunyemelea Gaza huku raia wakishambuliwa
Hali ya njaa inazidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, huku taarifa ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu misaada ya kibinadamu ikionya juu ya ongezeko la vifo vinavyotokana na utapiamlo, mashambulizi yasiyokoma dhidi ya raia, na vizingiti vinavyoongezeka katika upatikanaji wa misaada katikati ya mgogoro unaozidi kuongezeka.
Kati ya vifo 154 vinavyohusishwa na utapiamlo vilivyoripotiwa na mamlaka ya afya ya Gaza tangu Oktoba 2023 (ikiwa ni pamoja na watoto 89), Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa vifo 63 vilitokea mwezi Julai pekee.
Vifo hivi vinatokana na kushuka kwa kiwango kikubwa cha ulaji wa chakula: asilimia 81 ya kaya ziliripoti ulaji duni wa chakula mwezi Julai (ikilinganishwa na asilimia 33 mwezi Aprili), na asilimia 24 walikumbwa na njaa kali (ikilinganishwa na asilimia 4), hali ambayo imevuka kizingiti cha njaa, kwa mujibu wa taarifa ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) siku ya Jumatano.
Viwango vya utapiamlo mkali pia vimevuka viwango vya njaa huko Khan Younis, Deir al Balah na Jiji la Gaza.
Kwa kuzingatia takwimu hizi za hivi karibuni, wataalamu wa vipimo vya upatikanaji wa chakula wameonya kuwa hali mbaya kabisa ya njaa sasa inajitokeza.
Hata hivyo, wamesisitiza kuwa ingawa kizingiti cha tatu cha njaa—yaani vifo vinavyotokana na njaa—kinaongezeka, ukusanyaji wa takwimu unabaki kuwa changamoto.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa muda wa kuitikia kikamilifu kwa hali hii ya kibinadamu unayoyoma. Asilimia 22 ya watu waliotathminiwa wanakabiliwa na hali ya “ukosefu wa chakula wa kiwango cha janga,” huku asilimia 54 zaidi wakikabiliwa na “hali ya dharura.”
Wakati huo huo, chini ya asilimia 15 ya huduma muhimu za lishe bado zinafanya kazi.
Mashambulizi dhidi ya raia
Kati ya wapalestina zaidi ya 60,000 waliouawa tangu Oktoba 2023, takribani 9,000 waliuawa baada ya mapigano kuanza tena mwezi Machi mwaka huu, na 640 waliuawa kati ya tarehe 23 hadi 30 Julai.
Vifo vya raia wakati wa kutafuta chakula pia vinaongezeka, ambapo watu 1,239 wameuawa na zaidi ya 8,152 kujeruhiwa tangu tarehe 27 Mei.
Miongoni mwa waliojeruwa wakati wa kusaka msaada wa chakula ni mtoto Sahar mwenye umri wa miaka 14.
Soma kisa chake hapa.
OCHA pia imeeleza kuwa idadi ya watu waliopoteza makazi tangu tarehe 18 Machi imezidi 767,800, ingawa hakuna amri mpya za kuhamishwa zilizotolewa na mamlaka za Israeli tangu 20 Julai. Amri ya tarehe 20 Julai iliyohusisha kituo cha kibinadamu cha Deir al Balah imebatilishwa tangu wakati huo.
Katikati ya uhamishaji unaoendelea, msongamano wa watu kwenye makazi ya muda, ukosefu wa faragha, na ongezeko la njaa kumeongeza hatari ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana.
Hali ni mbaya zaidi katika eneo la kusini mwa Gaza, ambako hakuna tena maeneo salama ya hifadhi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia..
Hatua za kibinadamu
Kati ya tarehe 23 hadi 29 Julai, ni asilimia 47 pekee ya harakati 92 za misaada zilizoratibiwa zilifanikishwa kikamilifu na mamlaka za Israeli. Takriban asilimia 16 zilikataliwa, asilimia 26 zikikwamishwa baada ya kuidhinishwa awali, na asilimia 11 zilifutwa na waandaaji.
Jeshi la Israeli lilitangaza kusitisha shughuli za kijeshi kwa saa 10 kila siku kuanzia tarehe 27 Julai katika maeneo ya Al Mawasi, Deir al Balah na Jiji la Gaza, “ili kuongeza kiwango cha misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.”
Pia walitangaza hatua nyingine kama vile kuangushwa kutoka angani kwa unga, sukari na vyakula vya kwenye makopo; kurejeshwa kwa njia ya umeme kutoka Israel hadi kwenye mtambo wa kusafisha maji wa kusini mwa Gaza; kuondolewa kwa vikwazo vya forodha kwa chakula, dawa na mafuta kutoka Misri; na kutengwa kwa njia salama za misafara ya misaada ya Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, washirika wa misaada ya kibinadamu wameonya kuwa kuangusha misaada kutoka angani kunaweza kuhatarisha raia, kusababisha usambazaji usio sawa, na kutotosheleza mahitaji.
Kukabiliana na ukosefu wa fedha
Zaidi ya hayo, ukosefu wa ufadhili wa kutosha unazidi kudhoofisha juhudi za kukabiliana na janga hilo.
Kufikia tarehe 30 Julai, ni takriban asilimia 21 pekee ya dola bilioni 4 zilizohitajika kwa ombi la dharura la misaada kwa mwaka 2025 kwa ukanda huo zimepatikana, na hivyo kuacha mapengo makubwa ya huduma muhimu.