UDADAVUZI: Fahamu faida ya kunyonyesha maziwa ya mama kwa mtoto
UDADAVUZI: Fahamu faida ya kunyonyesha maziwa ya mama kwa mtoto
Lishe duni kwa watoto inahusishwa na idadi ya vifo vya watoto takribani milioni 2.7 kila mwaka au asilimia 45 ya vifo vyote vya watoto. Lishe kwa watoto wachanga na wadogo ni eneo muhimu la kuboresha maisha ya watoto na kukuza ukuaji na maendeleo yenye afya. Miaka miwili ya mwanzo ya maisha ya mtoto ni muhimu sana, kwani lishe bora katika kipindi hiki hupunguza magonjwa na vifo, hatari ya magonjwa sugu, na hukuza maendeleo bora kwa ujumla, linaeleza Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO.
Unyonyeshaji bora ni muhimu sana kiasi kwamba kila mwaka unaweza kuokoa maisha ya zaidi ya watoto 820,000 walio chini ya umri wa miaka mitano.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, la afya duniani (WHO) na lile la kuhudumia watoto (UNICEF) yanapendekeza:
- Kuanza kunyonyesha mapema ndani ya saa 1 pindi mtoto anapozaliwa;
- Kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi 6 ya mwanzo wa maisha ya mtoto; na
- Kuanzisha vyakula vya ziada (imara) vyenye virutubisho na salama, pamoja na kuendelea kunyonyesha hadi umri wa miaka miwili au zaidi.
Hata hivyo, watoto wengi hawapati lishe bora. Kwa mfano, ni karibu asilimia 44 tu ya watoto wenye umri wa miezi 0–6 duniani kote walionyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha mwaka 2015-2020.
Mapendekezo yameboreshwa pia ili kushughulikia mahitaji ya watoto waliozaliwa na akina mama walioambukizwa Virusi vya UKIMWI. Dawa za kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI sasa zinaruhusu watoto hawa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee hadi watakapofikisha umri wa miezi 6 na kuendelea kunyonyesha hadi angalau umri wa miezi 12 na kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Faida za Kunyonyesha
Kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi 6 kuna faida nyingi kwa mtoto na mama. Faida kuu ni ulinzi dhidi ya magonjwa ya tumbo ambayo huonekana sio tu katika nchi zinazoendelea bali pia katika nchi zilizoendelea. Kuanza kunyonyesha mapema, ndani ya saa 1 pindi mtoto anapozaliwa, humlinda mtoto mchanga dhidi ya kupata maambukizi na hupunguza vifo vya watoto wachanga. Hatari ya vifo kutokana na kuhara na maambukizi mengine inaweza kuongezeka kwa watoto wanaonyonyeshwa kwa kiasi kidogo au wasionyonyeshwa kabisa.
Maziwa ya mama pia ni chanzo muhimu cha nishati na virutubisho kwa watoto wenye umri wa miezi 6–23. Huweza kuchangia nusu au zaidi ya mahitaji ya nishati ya mtoto kati ya umri wa miezi 6 na 12, na theluthi moja ya mahitaji ya nishati kati ya umri wa miezi 12 na 24. Maziwa ya mama pia ni chanzo muhimu cha nishati na virutubisho wakati wa ugonjwa, na hupunguza vifo miongoni mwa watoto wenye utapiamlo.
Watoto na vijana ambao walinyonyeshwa wakati wakiwa wadogo, wana uwezekano mdogo wa kuwa na uzito mkubwa au wanene kupita kiasi. Zaidi ya hayo, hufanya vizuri zaidi katika vipimo vya akili na huwa na mahudhurio ya juu shuleni. Kunyonyesha kunahusishwa na kipato cha juu katika maisha ya utu uzima. Kuboresha maendeleo ya watoto na kupunguza gharama za afya husababisha faida za kiuchumi kwa familia binafsi na pia katika ngazi ya kitaifa.
Kunyonyesha kwa muda mrefu pia huchangia afya na ustawi wa akina mama: hupunguza hatari ya saratani ya ovari na matiti na husaidia kupanga uzazi kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa watoto walio chini ya umri wamiezi 6 kuna athari ya homoni ambayo mara nyingi husababisha ukosefu wa hedhi. Hii ni njia ya asili (ingawa si salama kabisa) ya kuzuia mimba inayojulikana kama njia ya unyonyeshaji ya Amenorrhea.
Akina mama na familia wanahitaji kuungwa mkono ili watoto wao wanyonyeshwe kwa njia bora. Mambo yanayosaidia kulinda, kukuza, na kuunga mkono unyonyeshaji ni pamoja na:
- Kupitisha sera kama vile "Mkataba wa Ulinzi wa Uzazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi namba 183" na "Pendekezo Namba 191", ambalo linaongeza "Mkataba namba 183" kwa kupendekeza muda mrefu wa likizo na marupurupu ya juu;
- Kupitisha "Kanuni ya Kimataifa ya Uuzaji wa Maziwa Mbadala ya Mama" na maazimio mengine muhimu ya Mkutano wa Afya Ulimwenguni;
- Utekelezaji wa "Hatua Kumi za Mafanikio ya Kunyonyesha" zilizoelezwa katika Mpango wa Hospitali Rafiki kwa Mtoto, ikiwemo;
○Kugusana ngozi kwa ngozi kati ya mama na mtoto mara tu baada ya kuzaliwa na kuanza kunyonyesha ndani ya saa 1 ya mwanzo pindi mtoto anapozaliwa;
○Kunyonyesha kwa mahitaji (yaani, mara kwa mara kama mtoto anavyotaka, mchana na usiku);
○Kulala chumba kimoja (kuruhusu akina mama na watoto wachanga kukaa pamoja kwa muda wa saa 24 );
○Kutowapa watoto chakula au kinywaji cha ziada, hata maji, isipokuwa ikiwa ni lazima kwa matibabu;
- Kutoa huduma za afya zinazosaidia na ushauri wa lishe ya watoto wachanga na wadogo wakati wa mawasiliano yote na walezi na watoto wadogo, kama vile wakati wa matunzo ya kabla na baada ya kujifungua, ziara za mtoto mwenye afya na mtoto mgonjwa, na chanjo; na
- Msaada wa jamii, ikiwemo vikundi vya kusaidiana vya akina mama na shughuli za kukuza afya na elimu katika jamii.
Unyonyeshaji wa maziwa ya mama unaweza kuboreshwa kwa kiasi kikubwa kwa msaada wa juhudi maalum, na idadi ya akina mama wanaonyonyesha watoto wao maziwa pekee na kwa muda mrefu inaweza kuongezeka ndani ya miaka michache.
Mlo wa ziada kwa watoto
Karibu na umri wa miezi 6, mahitaji ya nishati na virutubisho ya mtoto huanza kuzidi kile kinachotolewa na maziwa ya mama, na vyakula vya ziada ni muhimu ili kukidhi mahitaji hayo. Mtoto wa umri huu, pia yuko tayari kwa vyakula vingine. Ikiwa vyakula vya nyongeza havitaanzishwa karibu na umri wa miezi 6, au vikitolewa kwa njia isiyofaa, ukuaji wa mtoto unaweza kudumaa.
Ulishaji wa watoto katika mazingira magumu sana
Familia na watoto walioko katika hali ngumu wanahitaji uangalizi maalum na msaada kwa vitendo. Kadri inavyowezekana, mama na mtoto wanapaswa kubaki pamoja na kupata msaada wanaohitaji ili waweze kutumia njia bora zaidi ya lishe iliyopo. Kwa mfano, katika karibu kila hali ngumu, unyonyeshaji wa maziwa ya mama bado unabaki kuwa njia bora ya lishe kwa mtoto.