Agosti 1-7: Dunia inadhimisha wiki ya unyonyeshaji
Agosti 1-7: Dunia inadhimisha wiki ya unyonyeshaji
Wiki ya Unyonyeshaji Duniani imeanza rasmi hii leo, chini ya kauli mbiu: "Wekeza katika Unyonyeshaji, Wekeza katika Mustakabali wa Baadaye."
Wiki hii huadhimishwa kila mwaka katika wiki ya kwanza ya mwezi Agosti (tarehe 1 mpaka 7) kwa ushirikiano wa mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la la Afya Duniani (WHO), linalohusika na masuala ya watoto UNICEF, Wizara za Afya na mashirika mbalimbali ya kijamii duniani kote.
Wiki hii hutumika kama kipindi cha kutambua unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni msingi madhubuti wa afya bora, maendeleo na usawa katika maisha ya mwanadamu.
Kwa mujibu wa WHO kupitia kampeni yake ya "Mwanzo wa Afya Njema, Mustakabali wa Tumaini", Wiki ya Unyonyeshaji mwaka huu inaangazia umuhimu wa msaada endelevu kutoka kwenye mifumo ya afya kwa wanawake na watoto wao katika safari ya unyonyeshaji.
Hii inamaanisha kuhakikisha kila mama anapata taarifa sahihi na msaada wa kitaalamu anaohitaji ili aweze kunyonyesha kadri anavyotamani kwa kuwekeza katika wataalamu waliobobea katika kusaidia unyonyeshaji wa maziwa ya mama.