Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ndoto ya Sahar ya kushamiri kimaisha yatwamishwa na mashambulizi Gaza

Msichana apokea matibabu hospitalini baada ya kushambuliwa katika kituo cha lishe huko Deir Al-Balah, Gaza.
© UNICEF/Rawan Eleyan
Msichana apokea matibabu hospitalini baada ya kushambuliwa katika kituo cha lishe huko Deir Al-Balah, Gaza.

Ndoto ya Sahar ya kushamiri kimaisha yatwamishwa na mashambulizi Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Harakati za kila uchao kwa raia wa Gaza huko eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli za kukimbilia chakula huku mashambulizi yakiendelea zimeendelea kusababisha vifo na majeruhi ambapo majeruhi wa hivi karibuni aliyetajwa ni Sahar, mtoto mwenye umri wa miaka 14 aliyepata ulemavu akikimbilia kupokea msaada wa chakula. 

video iliyochapishwa mtandao wa X na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipaletina, UNRWA, inaonesha kilichojiri.

Sahar, akitembea na kiti mwendo kwenye kituo cha afya hapa Ukanda wa Gaza, Mashariki ya Kati akipatiwa matibabu ya mazoezi ya viungo ya mkono na mguu baada ya kujeruhiwa na mashambulizi kutoka Israeli.

Akiwa ameketi kwenye kiti mwendo Sahar anakumbuka kilichojiri akisema,  nilikuwa katika foleni kwenye shule ya Rohida nikisubiri mgao wa chakula ndipo jiko la umma la Tekiya lilipigwa bomu, nami nilikimbia.

Kituo hiki kinaendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA na Sahar akiendelea na kilichomsibu anasema, nilipoteza fahamu kwa siku 17. Hivi sasa siwezi kutembea. Hakuna chakula, hakuna maji, hakuna wanasesere.

Lakini anachoshukuru Sahar ni kwamba, Niko hapa kituo cha afya cha UNRWA, ninapata matibabu na mazoezi ya viungo kwa ajili ya mkono wangu na mguu wangu ili hatimaye mkono upate fahamu na mguu pia niweze kutembea kama zamani.

Sasa Sahar anasema ndoto yake zamani ilikuwa ni kushamiri kimaisha na kuongoza lakini sasa ndoto yake ni kuweza kutembea tena.

Kamishna Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini anasema wakati umefka kwa misaada ifikie wakazi wa Gaza kwa usalama na kwa utu.