Maspika wa Mabunge wapitisha azimio la kihistoria
Maspika wa Mabunge wapitisha azimio la kihistoria
Mkutano wa Sita wa Maspika wa Mabunge Duniani uliofanyika jijini Geneva, Uswisi, jana Julai 31 umefika tamati baada ya siku tatu za mijadala ambazo zimezaa Azimio la kihistoria linalotoa wito wa "ushirikiano wa kimataifa ulio thabiti na wenye ufanisi zaidi" ili kuendeleza amani, haki, na ustawi.
Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, (IPU), Tulia Ackson kupitia hotuba ya kufunga mkutano huo uliondaliwa kwa ushirikiano wa IPU na Umoja wa Mataifa akadokeza kilichomo katika Azimio la ngazi ya juu kwamba, “kwanza kabisa, ni wito wa uwajibikaji. Linatuhimiza kufanya kazi kuelekea utataratibu wa dunia ulio wa kibinadamu zaidi ambapo ushirikiano unawekwa katikati ya utungaji sera, ambapo usawa wa kijinsia ni jambo la kawaida, na vijana, watu walioko katika mazingira magumu pamoja na makundi yasiyo na uwakilishi wa kutosha wanajumuishwa kikamilifu. Kwa hakika, amani haitegemei tu mikataba; inadumu kupitia haki, usawa, ujumuishaji, na utawala wa sheria. Azimio letu la ngazi ya juu pia linaweka wazi kuwa kulinda sayari yetu, raia wetu, na demokrasia zetu hakuwezi kuachwa mikononi mwa mamlaka ya utendaji pekee. Kama viongozi wa mabunge yetu, tunawajibika. Uwajibikaji huu unaanzia na sheria tunazopitisha, mijadala tunayoiendesha, na bajeti tunazoidhinisha. Zaidi ya yote, tamko hili linatutaka sisi kama wabunge na wawakilishi wa wananchi tujitambue kama wasanifu wa majadiliano, walezi wa ujumuishaji, na mawakala wa mabadiliko yenye maana. Na ninayo furaha, kutambua kuwa nafasi ya wabunge kama mawakala wa mabadiliko yenye maana imeendelea kukua ndani ya uongozi wa dunia na Umoja wa Mataifa.”
Aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ni Courtenay Rattray ambaye pia ni ‘Chef de Cabinet’ naye akizungumza katika tukio la kufunga mkutano amesema, “Mkutano huu pamoja na Mkutano wa 15 wa Maspika Wanawake wa Mabunge ulioutangulia, “umekuwa ukumbusho wa kipekee wa uwezo wetu wa pamoja wa kuthibitisha tena malengo yetu ya pamoja. Tumefaidika kutokana na ushiriki wa maspika wa mabunge walioungana na wabunge, mashirika ya kiraia, vijana, sekta binafsi na wanazuoni kutoka kila pembe ya dunia. Hivi ndivyo ushirikiano wa kimataifa unaojumuisha wote na unaounganisha wadau unavyopaswa kuwa. Hebu tuendeleze kasi ya leo na kuigeuza midahalo kuwa vitendo. Ninaamini kuwa mahusiano tuliyoyajenga katika siku hizi chache zilizopita yatatuchochea si tu katika majukwaa ya kimataifa, bali pia ndani ya jamii na taasisi zetu. Kama Katibu Mkuu alivyosema wakati wa ‘siku za kuchukua hatua’ za Mkutano wa Zama Zijazo mwezi Septemba iliyopita: Ushirikiano mpya wa kimataifa hautajengwa kwa siku moja, wala na serikali peke yake. Utachochewa na kusongeshwa na kila mmoja wenu na makundi mnayowakilisha. Tumepigania malengo. Sasa na tupiganie utekelezaji pamoja.”
Muhtasari wa Azamio
Azimio la Ngazi ya Juu la Mkutano wa Sita wa Spika wa Mabunge Duniani (Geneva, 29–31 Julai 2025) linazungumzia dunia inayokumbwa na misukosuko, ikiwemo kudhoofika kwa ushirikiano wa kimataifa, kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, vitisho kwa demokrasia, na migogoro ya kimataifa kama vile mizozo, mabadiliko ya tabianchi, na uhamishaji wa watu. Azimio hili linasisitiza wajibu wa mabunge katika kulinda maadili ya kidemokrasia, kukuza amani, na kuongoza hatua za kimaadili na kisheria kushughulikia changamoto za dunia.
Masuala muhimu yaliyosisitizwa ni pamoja na:
- Vitisho kwa amani, demokrasia, utawala wa sheria, na haki za binadamu.
- Kuongezeka kwa mizozo, utaifa usio jumuishi, upotoshaji wa taarifa, na kutengwa kwa makundi.
- Ukosefu wa usawa wa kiuchumi, janga la tabianchi, ukosefu wa usawa wa kijinsia, na kutoshirikishwa kwa vijana.
- Kudhoofika kwa mifumo ya ushirikiano wa kimataifa na kuongezeka kwa vitisho vya nyuklia.
Azimio linatoa wito wa mageuzi makubwa ya sera kama vile:
- Kuimarisha sheria za kimataifa na taasisi za kidemokrasia.
- Kufafanua upya dhana ya usalama kwa kuzingatia zaidi ya masuala ya kijeshi.
- Kukuza utawala wa kidijitali na ushirikiano katika masuala ya mtandao.
- Kuharakisha maendeleo endelevu, hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, na mifumo ya uchumi jumuishi.
- Kukuza usawa wa kijinsia, ushiriki wa vijana, na kuheshimu utofauti.
Maspika wa mabunge wameahidi:
- Kuuunga mkono Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa 2024 wa Mustakabali wa Dunia.
- Kuchukua hatua za kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa kuzingatia jukumu la Umoja wa Mataifa.
- Kuongeza nafasi ya mabunge katika utawala wa kimataifa na usimamizi wa uwajibikaji.
- Kukuza uwakilishi jumuishi, ushirikiano na asasi za kiraia, diplomasia ya kisayansi, udhibiti wa AI, na kuzuia migogoro.