Ripoti ya IMF yatoa tahadhari licha ya ongezeko la ukuaji wa uchumi wa dunia
Ripoti ya IMF yatoa tahadhari licha ya ongezeko la ukuaji wa uchumi wa dunia
Shirika la fedha la kimataifa IMF limetangaza utabiri mpya wa ukuaji wa kiuchumi wa kimataifa likikadiria kuwa mwaka 2025 viwango vya ukuaji vitakuwa kwa asilimia 3.0 na mwaka 2026 ukuaji utakuwa kwa asilimia 3.1.
Katika taarifa yake iliyotolewa Washington D.C, mji mkuu wa Marekani na makao makuu ya shirika hilo, Utabiri huu mpya wa 2025 ni ongezeko la asilimia 0.2 ikilinganishwa na utabiri wa marejeleo wa Mtazamo wa Kiuchumi wa Dunia uliotolewa mwezi Aprili 2025, wakati matarajio ya 2026 yamepanda kwa asilimia 0.1 kwa asilimia 0.1.
Pierre-Olivier Gourinchas ambaye ni Mchumi Mkuu wa IMF ameeleza sababu za uchumi kupanda “Ukuaji wa uchumi wa dunia umepanda hadi asilimia 3.0 kwa mwaka 2025 na asilimia 3.1 kwa mwaka 2026. Hii ni kutokana na kasi ya ukuaji iliyotarajiwa mapema, viwango vya ushuru vilivyopungua, mazingira bora ya kifedha ikiwemo dola ya Marekani kuwa dhaifu, na ongezeko la matumizi ya serikali katika baadhi ya nchi. Hata hivyo, bado ukuaji uko chini kwa asilimia 0.2 ikilinganishwa na matarajio kabla ya Aprili, jambo linaloashiria kuwa mvutano wa kibiashara unaathiri uchumi wa dunia. Mfumuko wa bei unatarajiwa kushuka na kufikia asilimia 4.2 mwaka 2025 na asilimia 3.6 mwaka 2026.”
Pamoja na habari hizo njema kwa dunia, IMF inaonya bado kuna hatari zinazoikabili dunia, hasa mvutano wa kibiashara, mabadiliko ya kisiasa na hali tete ya kifedha katika baadhi ya nchi. “Hatari bado zipo. Kukwama kwa mazungumzo ya kibiashara au kurudi kwa sera za kulinda masoko kunaweza kudhoofisha ukuaji na kuongeza mfumuko wa bei katika baadhi ya nchi. Wasiwasi wa kisiasa na madeni ya serikali yanaweza kuathiri uwekezaji na ustawi wa kiuchumi. Ingawa hali ya kifedha imeboreshwa, inaweza kubadilika ghafla, hasa kama uhuru wa benki kuu utatishiwa. Habari njema ni kwamba mafanikio katika mazungumzo ya kibiashara na mageuzi ya kimuundo yanaweza kuimarisha matumaini na tija ya muda mrefu.”
Akizungumza katika Jukwaa la Baraza la Kiuchumi na Maendeleo la Umoja wa Mataifa, ECOSOC mwishoni mwa mwezi April, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres pamoja na mambo mengine alizitahadharisha nchi wanachama hususan za kipato cha chini kuwa madeni na vikwazo vya biashara vinakwamisha utekelezaji wao wa malengo ya maendeleo endelevu na kuzitaka kuwa waangalifu.
Ni kutokana na ukweli huo huo ndio maana katika ripoti hii mpya IMF imezishauri nchi kuimarisha uthabiti wa kisera, kudhibiti matumizi ya serikali, na kulinda uhuru wa Benki Kuu, huku wakikumbatia mageuzi yatakayowezesha ukuaji wao wa muda mrefu.
IMF inasema, “kupunguza sintofahamu katika sera ni jambo la msingi, hasa kwenye sera za biashara. Uchumi wa dunia unahitaji kanuni wazi na zinazotabirika. Nchi nyingi zinapaswa kurekebisha hali ya fedha na kujenga akiba licha ya mahitaji makubwa ya matumizi. Benki kuu lazima zidumishe utulivu wa bei na kifedha, huku zikihifadhi uhuru wao. Urahisi wa kubadilisha viwango vya fedha ni muhimu, ingawa baadhi ya uingiliaji maalum unaweza kuwa wa maana. Na mwisho, mageuzi ya kimuundo ni muhimu kwa ustawi wa muda mrefu.”