UNCTAD: Biashara inaweza kusaidia kukomesha uchafuzi usababishwao na plastiki
UNCTAD: Biashara inaweza kusaidia kukomesha uchafuzi usababishwao na plastiki
Kuelekea mkutano wa kujadili mkataba wa kimataifa na kuunda chombo cha kisheria dhidi ya uchafuzi unaosababishwa na plastiki huko Geneva Uswisi mwezi Agosti, mwaka huu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD limesema biashara inaweza kuwa chombo muhimu katika kulinda mazingira ikiwa itaelekezwa kwa njia sahihi.
Katika taarifa iliyochapishwa hii leo kwenye wavuti wake kabla ya kuanza kwa mkutano huo tarehe 5-14 Agosti, UNCTAD imeeleza kuwa plastiki ni kati ya bidhaa zinazouzwa zaidi duniani biashara yake ilifikia karibu dola trilioni 1.2 mwaka 2021. Lakini bidhaa hizi pia ni chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira, hasa baharini, na zinachangia mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti mpya ya UNCTAD inaeleza kuwa ili kumaliza uchafuzi wa plastiki duniani, biashara lazima iwe sehemu ya suluhisho na si sehemu ya tatizo. Hii inamaanisha kuweka sera bora za kibiashara zitakazosaidia kuzuia uagizaji wa plastiki hatarishi, na kuhimiza matumizi ya bidhaa mbadala kama vile karatasi, mianzi au nyenzo ambazo zinaoza kwa urahisi.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limezishauriserikali kupunguza vikwazo ili kuhimiza biashara ya bidhaa rafiki kwa mazingira. Kwa sasa, bidhaa mbadala za plastiki hukabiliwa na ushuru mkubwa zaidi ikilinganishwa na plastiki ya kawaida jambo linalozuia ushindani wa haki.
Wakati dunia ikielekea kuujadili mkataba wa kimataifa wa kukomesha uchafuzi wa plastiki, UNCTAD inasisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa kupitia biashara ni muhimu. Nchi zinazoendelea pia zina nafasi ya kunufaika kwa kuuza bidhaa mbadala, endapo zitapewa msaada wa kiteknolojia na fedha.