Madhara ya tabianchi Somalia yanahitaij usaidizi wa kimataifa: IOM
Madhara ya tabianchi Somalia yanahitaij usaidizi wa kimataifa: IOM
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), Ugochi Daniels, amehitimisha ziara ya siku nne nchini Somalia, akitoa tahadhari kuhusu kuzidi kuongezeka kwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi na watu kutawanyika katika ukanda huo.
“Watu wa Somalia wanakumbwa na athari kali zaidi mbaya za mabadiliko ya tabianchi – hali inayochochea watu kuhama hama ndani ya nchi na hivyo kuleta mzigo zaidi kwa miji ambayo tayari iko katika shinikizo, na kuongeza mivutano kuhusu rasilimali zinazopungua,” amesema Bi. Daniels akiwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Kupitia taarifa ya IOM iliyotolewa leo huko Mogadishu, Somalia, Bi. Daniels ameongeza kuwa watu hao “wanabeba mzigo huu licha ya kuwa hawahusiki kabisa na utoaji wa gesi chafuzi duniani.”
Suluhu bunifu jimboni Puntland
Kutoka mji mkuu Mogadishu hadi mji wa bandari wa Bossaso kaskazini, jimboni Puntland, Bi. Daniels alikutana na maafisa wa serikali, viongozi wa jamii, vikundi vya wanawake, na watumishi wa IOM mashinani .
Huko ameshuhudia moja kwa moja jinsi jamii za kisomali zinavyokabiliana na ukame wa muda mrefu, mafuriko, na migogoro – hali ambazo zimewafurusha watu takriban milioni 3.6 na kuvuruga karibu nusu ya idadi ya watu kutokana na majanga yanayohusiana na tabianchi.
Ziara yake ilionesha ukubwa wa janga hili pamoja na nguvu ya hatua zinazochukuliwa na jamii za wenyeji.
“Somalia si mahali pa mateso tu – ni ushahidi wa uvumilivu na ustahimilivu,” amesema, akiongeza kuwa “jamii hapa zinaongoza kwa suluhu za ubunifu zinazotokana na mazingira yao wenyewe – kukabiliana na athari za tabianchi huku wakijenga msingi wa amani na utulivu. Dunia ina mengi ya kujifunza kutoka kwa mafanikio haya.”
Katika kila kituo alichotembelea, Bi. Daniels amesisitiza umuhimu wa haraka wa usaidizi wa kifedha kutoka jamii ya kimataifa ili kuweesha Somalia kuhimili na kukabili mabadiliko ya tabianchi – ikiwa ni pamoja na kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Tabianchi (Green Climate Fund) – kufikia jamii na watu wanaohitaji msaada zaidi.
IOM Somalia na kujengea uwezo wananchi
Ameeleza jinsi IOM Somalia inavyotumia mbinu jumuishi inayochanganya msaada wa dharura na hatua za muda mrefu za ujenzi wa ustahimilivu.
Hii ni pamoja na kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema na maandalizi dhidi ya majanga, kuendeleza miundombinu ya kijamii na mifumo ya ulinzi wa jamii, kujenga miundombinu inayohimili hali ya tabianchi pamoja na huduma za msingi, au kupanua njia mbadala za maisha endelevu.
Katika maeneo ya wakimbizi wa ndani, IOM inaunga mkono mifumo ya uongozi ya kijamii inayoongozwa na jamii husika ili kuwapa watu sauti na nafasi ya kushiriki katika mchakato wa kujikwamua.
Katika maeneo ya vijijini na yenye mazingira tete, shirika hilo pia linaendeleza urejeshaji wa ardhi na ujenzi wa amani wa kimazingira, ili kupunguza mivutano juu ya rasilimali na kujenga uthabiti kutoka ngazi ya chini kabisa.
Dunia isiisahau Somalia
Huko Bossaso, pia ameona jinsi athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyochochea uhamiaji wa ndani na wa kuvuka mipaka. “Kinachotokea hapa kinaashiria mabadiliko ya kikanda kwa ujumla,” amesema. “Shinikizo kutokana na mazingira na ugumu wa kiuchumi ni sababu kuu zinazobadilisha mienendo ya uhamaji katika Pembe ya Afrika na zaidi. Hivyo basi, hatua thabiti za kikanda ni muhimu.”
Somalia inapoendelea kukabiliana na hali halisi ya mabadiliko ya tabianchi na mazingira, Bi. Daniels ametoa ujumbe ulio wazi:
“Hili si kuhusu Somalia pekee – ni changamoto kwa dunia nzima. Tunaweza kuamua kuwekeza katika suluhu sasa, au kuwaacha walio hatarini zaidi walipe gharama ya kutochukua hatua baadaye. Dunia haipaswi kugeuza macho.”