Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki wa vijana katika Jukwaa la ECOSOC: Kapwani Kavenuke atoa wito wa ushirikishwaji zaidi

Kapwani Kavenuke kutoka Tanzania, mmoja wa washiriki wa mijadala ya Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) limefanyika hivi majuzi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, akizungumza na S…
UN News
Kapwani Kavenuke kutoka Tanzania, mmoja wa washiriki wa mijadala ya Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) limefanyika hivi majuzi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, akizungumza na Sharon Jebichii wa UN News Kiswahili.

Ushiriki wa vijana katika Jukwaa la ECOSOC: Kapwani Kavenuke atoa wito wa ushirikishwaji zaidi

Na Sharon Jebichii - New York, Marekani
Ukuaji wa Kiuchumi

Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) lilifanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani mwezi Aprili mwaka huu wa 2025. Jukwaa hili lilifanyika kwa siku 4 likileta pamoja vijana kutoka mataifa mbalimbali duniani na wadau wa maendeleo na uchumi ili kujadili changamoto zinazowakabili vijana na kutoa mapendekezo ya kuboresha dunia kuelekea usawa na maendeleo endelevu chini ya Ajenda ya 2030 au Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).

Miongoni mwao ni Kapwani Kavenuke, ambaye ameshiriki kikamilifu katika mijadala ya jukwaa hilo, akileta sauti ya vijana wa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Akizungumza na Sharon Jebichii wa Idhaa hii ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Kapwani amesema kuwa lengo la ushiriki wao ni kuhakikisha kuwa sauti za vijana wa Afrika zinajumuishwa katika mijadala ya kimataifa kama ECOSOC.

Kapwani anaeleza kuwa ushiriki wao katika mkutano wa ECOSOC ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha sauti za vijana kutoka Afrika zinasikika katika majukwaa ya kimataifa.

“Tumekuja kuwakilisha vijana kutoka nchi zetu, lakini pia kuonesha mifano halisi ya mambo chanya tunayoyafanya katika ngazi ya kitaifa kuhusu utekelezaji wa SDGs,” amesema Kapwani katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya UN.

Amesema kuwa mwaka jana walishiriki katika mkutano uliojadili “Pact for the Future”, mkataba muhimu wa kimataifa uliopitishwa tarehe 22 Septemba 2024. Baada ya hapo, waliunda kabrasha maalum linaloeleza mchango wa vijana katika kutekeleza SDGs, ambalo sasa linashirikishwa kwa nchi nyingine kama mfano wa kuigwa.

Kapwani Kavenuke kutoka Tanzania, mmoja wa washiriki wa mijadala ya Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) limefanyika hivi majuzi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.
UN News
Kapwani Kavenuke kutoka Tanzania, mmoja wa washiriki wa mijadala ya Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) limefanyika hivi majuzi katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.

BBT: Programu inayoibua uwezo wa vijana katika kilimo

Katika moja ya mijadala ya jukwaa hilo, Kapwani ameshiriki kikao kilichoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kuhusu nafasi ya vijana katika kilimo. Anaeleza namna Tanzania inavyotekeleza programu ya BBT – Building a Better Tomorrow, kwa ushirikiano na Serikali na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

“Programu hii inawafundisha vijana ujuzi wa kilimo, teknolojia rafiki kwa mazingira, na mbinu za kujiajiri kupitia sekta ya kilimo. Ni njia bora ya kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana," ameeleza Kapwani.

Anahimiza kuwa kilimo si tu shughuli ya vijijini bali ni chanzo kikubwa cha ajira na maendeleo ikiwa vijana watawezeshwa kwa maarifa na mitaji sahihi.

Changamoto ya ushiriki wa vijana wa Afrika

Kapwani pia amegusia changamoto mbalimbali zinazokwamisha ushiriki wa vijana wa Afrika katika majukwaa ya kimataifa kama ECOSOC. Ameyataja masuala ya upatikanaji wa visa, ukosefu wa taarifa sahihi, na changamoto za kifedha kama baadhi ya vikwazo vinavyowakwamisha vijana wengi kutoka Afrika.

“Ukweli ni kwamba bado idadi ya vijana kutoka Afrika kwenye jukwaa hili ni ndogo. Tunapaswa kushirikiana zaidi ili kuhakikisha taarifa na fursa hizi zinafika kwa wengi,” alisema kwa msisitizo.

Fursa zipo – vijana wajitokeze

Kapwani ameweka wazi kuwa yuko tayari kusaidia vijana wengine kwa kushirikiana nao kupitia mitandao ya kijamii na makundi ya WhatsApp anayoyaendesha.

“Nina kundi la WhatsApp lenye zaidi ya watu 400, ambapo huwa natuma fursa mbalimbali. Lakini kila kijana ni lazima ajitume mwenyewe. Fursa hazisubiri mtu; unapaswa kuwa na hamasa ya kuzijua, kuzitafuta na kuzitumia,” amehimiza.

Usawa, ushirikiano, na uwezo wa vijana

Kupitia ushiriki wa vijana kama Kapwani Kavenuke, Jukwaa la ECOSOC 2025 limeonesha kuwa vijana wana mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya duniani.

Kwa kushirikiana na serikali, mashirika ya kiraia, na mashirika ya kimataifa, vijana kutoka Afrika wana nafasi adhimu ya kuibadilisha jamii zao kwa kutumia sauti, maarifa, na mshikamano wa kimataifa.

“Ni muhimu tuliporudi nyumbani tukawa mabalozi wa fursa. Sio sisi tu kila mwaka. Tujitahidi kuwavuta wengine. Kila kijana anaweza!” Kapwani Kavenuke.