Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la New York lataka suluhisho la mataifa mawili, likitaka Israel itambue taifa la Palestina

Mawaziri wa Mambo ya Nje, Jean-Noël Barrot (kulia) wa Ufaransa na Mwanamfalme, Faisal bin Farhan Al Saud wa Saudi Arabia, ambao ni Wenyeviti Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Utatuzi wa Amani wa suala la Palestina na Utekelezaji wa Suluhisho la Mataif…
UN Photo/Loey Felipe
Mawaziri wa Mambo ya Nje, Jean-Noël Barrot (kulia) wa Ufaransa na Mwanamfalme, Faisal bin Farhan Al Saud wa Saudi Arabia, ambao ni Wenyeviti Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Utatuzi wa Amani wa suala la Palestina na Utekelezaji wa Suluhisho la Mataifa Mawili.

Azimio la New York lataka suluhisho la mataifa mawili, likitaka Israel itambue taifa la Palestina

Amani na Usalama

Baada ya siku tatu za majadiliano, Mkutano wa Ngazi ya Juu kuhusu Suluhisho la Mataifa Mawili umekamilika Jumatano hii ya Julai 30 mjini New York, Marekani kwa kutoa hati ya mwisho inayounga mkono suluhisho hilo na kuitaka Israel kuahidi wazi kuunga mkono kuanzishwa kwa taifa la Palestina.

“Tunautaka uongozi wa Israel kutoa ahadi ya wazi na ya hadharani kwa suluhisho la mataifa mawili, ikiwemo kuundwa kwa taifa huru na endelevu la Palestina,” linasema Azimio la New York, ambalo pia linaitaka Israel kusitisha mara moja mashambulizi dhidi ya Wapalestina, kusimamisha ujenzi wa makazi ya walowezi, na kuachana na nia yoyote ya kunyakua ardhi kwa mabavu.
 
Akizungumza kwa niaba ya Saudi Arabia na Ufaransa, waandaaji wa mkutano huo, pamoja na nchi washiriki muhimu katika vikundi kazi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Faisal bin Farhan Al Saud, ameeleza kuwa hati hiyo inajumuisha mapendekezo ya kina katika nyanja za kisiasa, kibinadamu, kiusalama, kiuchumi, kisheria na kimkakati, “ambayo yanaunda mfumo wa pamoja na unaotekelezeka kwa ajili ya utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili na kufanikisha amani na usalama kwa wote.”
 
“Ninayo furaha kupitisha hati ya matokeo ya Mkutano huu pamoja na kiambatisho chake, kwa mujibu wa azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa Desemba 2024. Tunawasihi mthibitishe Tamko hili kabla ya mwisho wa kikao cha 79 (yaani kufikia tarehe 5 Septemba), kwa kuarifu balozi za kudumu za Saudi Arabia na Ufaransa mjini New York,” aliwaambia wawakilishi wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.
 

Mpango wa amani wenye hatua halisi na zisizoweza kubatilishwa

 
Hati hiyo yenye kurasa saba inaeleza mpango wa utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili kwa kutumia hatua “halisi, zenye muda maalum na zisizoweza kubatilishwa.”
 
Katika hatua ya awali, hati hiyo inataka vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza vikomeshwe na kuundwe mara moja kamati ya muda ya usimamizi chini ya mamlaka ya Palestina.
 
“Katika muktadha wa kumaliza vita Gaza, Hamas inapaswa kukabidhi udhibiti wa Ukanda wa Gaza pamoja na silaha zake kwa Mamlaka ya Palestina, kwa msaada wa kimataifa,” inasema hati hiyo, ikisisitiza pia kuwa Hamas inapaswa kuwaachilia mateka wote.
 
Tamko hilo pia linapendekeza kutumwa kwa ujumbe wa muda wa kimataifa wa uthabiti kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
 
Aidha, hati hiyo inasisitiza kuwa “kama sehemu muhimu ya Taifa la Palestina,” Gaza lazima iunganishwe na Ukingo wa Magharibi. “Hapapaswi kuwepo uvamizi, mzingiro, kupunguzwa kwa eneo la ardhi, au uhamishaji wa kulazimishwa,” imeongeza.
 

Njia bora ya kukomesha machafuko kwa kila namna

 
Kumaliza mzozo wa Israeli na Palestina na kutekeleza suluhisho la mataifa mawili ndilo jibu pekee la kutimiza matarajio halali ya Waisraeli na Wapalestina, kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Ndiyo njia bora ya kumaliza machafuko ya aina zote na kuondoa athari hasi za makundi yasiyo ya kiserikali, hati hiyo inasema.
 
Pia inathibitisha kuwa suluhisho la mataifa mawili ndilo suluhisho la kweli kwa ugaidi na vurugu, na ndilo linaloweza kudumisha usalama wa mataifa yote mawili, uhuru wa kila taifa, pamoja na kuleta amani, ustawi na mshikamano wa kikanda kwa faida ya mataifa yote ya eneo hilo.
Tamko la New York linakuwa mpango wa kwanza wa amani kati ya Israel na Palestina ulioandaliwa bila ushiriki wa Marekani, nchi ambayo haikuhudhuria Mkutano huo, kama ilivyokuwa kwa Israel.