Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yataka ulinzi wa kisheria dhidi ya manusura wa uhalifu wa kulazimishwa

Mwonekano wa mwanamke unaonekana kutoka nyuma anapotazama nje kupitia dirisha lenye vizuizi kwenye mtaa wa makazi huko Trinidad na Tobago.
© IOM/Gema Cortes Maria* aliondoka Caracas, Venezuela, ili kutafuta fursa bora zaidi huko Trinidad na Tobago.

IOM yataka ulinzi wa kisheria dhidi ya manusura wa uhalifu wa kulazimishwa

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji,  (IOM) limetoa wito wa hatua za dharura na za pamoja kukabiliana na aina moja ya usafirishaji haramu wa binadamu ambao mara nyingi hauzingatiwi: kulazimishwa kutekeleza uhalifu.

IOM imesema hayo leo kupitia taarifailiyoitoa Geneva, Uswisi ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kupinga usafirishaji haramu wa binadamu.

Shirika hilo limesema makundi ya uhalifu yaliyoandaliwa yanawalazimisha watu walio katika mazingira hatarishi – wakiwemo wahamiaji, watoto na vijana – kutenda uhalifu kupitia udanganyifu, vitisho na ukatili.

Uhalifu wanaolazimishwa manusura kutekeleza

Uhalifu huo unajumuisha ulaghai wa mtandaoni, usafirishaji wa dawa za kulevya, na wizi – yote haya yakitekelezwa bila hiari ya mhusika bali kwa kudanganywa na kunyanyaswa.

“Usafirishaji haramu wa binadamu ni janga la haki za binadamu. Lakini pia ni biashara kubwa duniani inayochochea rushwa, kueneza hofu na kuwanyonya walio dhaifu zaidi,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope kwenye taarifa hiyo.

Ameongeza kuwa  “hatutapiga hatua katika kupambana na usafirishaji wa binadamu hadi tutakapoanza kuwalinda waathirika au manusura badala ya kuwaadhibu.”

IOM imeeleza kuwa tatizo hili linakua kwa kasi, hasa katika maeneo ya Kusini-Mashariki mwa Asia ambako mamia ya maelfu wanashikiliwa katika maeneo ya ulaghai.

Manusura hao huwekwa kwenye mazingira ya unyanyasaji na hukosa mamlaka juu ya maisha yao. Hata baada ya kuokolewa au kutoroka, wengi huendelea kubeba madhila kama vile rekodi ya uhalifu, unyanyapaa wa kijamii, na mifumo ya haki inayowachukulia kama wahalifu badala ya waathirika.

Manusura huadhibiwa badala ya wasafirishaji haramu

Kwa mujibu wa IOM, aina hii ya usafirishaji pia huchangia kwa kiasi kikubwa uhalifu wa kimataifa uliopangwa, na inakadiriwa kuzalisha dola bilioni 40 kila mwaka.

Waendeshaji wa uhalifu hunufaika mara mbili: kupitia matendo ya uhalifu yaliyolazimishwa na kupitia mifumo ya sheria inayowashtaki manusura huku ikiwaachia wahalifu halisi huru.

IOM inasisitiza kuwa serikali zinapaswa kuheshimu kanuni ya kutoadhibu waathirika na kuhakikisha kuwa mifumo ya kitaifa ya rufaa  inatoa msaada wa kweli – ikiwemo ulinzi wa kisheria na msaada wa kuanza maisha upya – badala ya kuwa taratibu za kiutawala zisizo na tija.

Katika dunia ambako 1 kati ya manusura 3 ni mtoto, na asilimia 78 wanatumikishwa kwa kazi za lazima au ukatili wa kingono, hatari ya usafirishaji wa binadamu inaongezeka hasa kutokana na migogoro, majanga, na umaskini.

IOM inatoa wito kwa serikali, washirika wa kimataifa na jamii kwa ujumla kuchukua hatua za pamoja. Kipaumbele kiwe kwenye ulinzi, haki na msaada wa muda mrefu kwa waathirika. “Ni lazima tutambue kuwa waathirika hawa ni watu waliovunjiwa haki zao – na mustakabali wao unategemea kujitolea kwetu kwa utu na haki.”