Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tanzania kuanza kutekeleza mpango wa WHO wa “Beat the Heat”

Jua lenye mwanga linaangaza kupitia mawingu yanayopinda katika anga la rangi ya machungwa na dhahabu.
© Unsplash/Emerson Peters Joto kali la kupindukia ni moja ya majanga yaliyokatili maisha ya watu wengi katika historia yakisababisha mamilioni ya watu kufungasha virago

Tanzania kuanza kutekeleza mpango wa WHO wa “Beat the Heat”

Tabianchi na mazingira

Tanzania, kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), iko mbioni kuzindua mpango wa “Beat the Heat” yaani “Lishinde Joto”, mpango wenye lengo la kukabiliana na joto kali na hatari za kimazingira katika sehemu za kazi na kwenye matukio makubwa ya kijamii. Anold Kayanda anafafanua zaidi taarifa iliyochapishwa leo na WHO jijini Dar es Salaam, Tanzania.

WHO inaeleza kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi za kwanza duniani kuanza kutekeleza mpango huu, ambao unatekelezwa chini ya ushirikiano kati ya WHO na Shrikisho la Mpira wa Miguu Duniani, FIFA kwa ufadhili kutoka Mfuko wa Urithi wa Kombe la Dunia 2022.

Mpango huu wa "Beat the Heat" au "Lishinde Joto" utatekelezwa hadi Juni 2026 na utatoa nyenzo halisi na mwongozo wa kiufundi kusaidia kuimarisha maandalizi na mwitikio wa kitaifa na wa mitaa dhidi ya vitisho vya kiafya vinavyohusiana na mabadiliko ya tabianchi hasa katika maeneo ya kazi, mazingira ya wazi, na matukio ya hadhara, taarifa ya WHO imeafafanua.

Utekelezaji wa mpango huu nchini Tanzania unakuja katika kipindi muhimu, wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2025, mashindano makubwa ya mpira wa miguu katika bara la Afrika yanayotarajiwa kuvutia umati mkubwa wa watu katika mazingira ya nje yenye joto kali.

“Mpango huu ni hatua ya wakati muafaka na ya kimkakati katika kulinda afya ya wote wanaohusika na kazi au matukio ya nje,” amenukuliwa Daktari Galbert Fedjo, Kaimu Mwakilishi wa WHO nchini Tanzania akiongeza kuwa kwamba, “kwa kuingiza ulinzi dhidi ya joto katika CHAN 2025 na zaidi ya hapo, Tanzania inaonesha mfano wa jinsi mataifa yanavyoweza kushughulikia athari halisi za mabadiliko ya tabianchi kwa afya ya umma.”

Kupitia mpango huu, Tanzania itatekeleza hatua mbalimbali zikiwemo:

  • kuandaa mipango ya kitaifa ya afya dhidi ya joto kali,
  • kuweka mifumo ya tahadhari za mapema na taratibu za dharura kwa hali ya joto,
  • kuweka maeneo ya kupumzikia yenye kivuli, vituo vya maji ya kunywa na vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi wa nje na wahudumu wa matukio,
  • na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya na waandaaji wa matukio juu ya kinga na huduma ya kwanza kwa magonjwa yanayosababishwa na joto.

Mpango huu unatekelezwa chini ya uongozi wa Wizara za Afya ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Michezo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Kitengo cha Dharura cha Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Mkoa ya Lumumba, pamoja na wadau wengine wakuu wanaohusika na uandaaji wa mikusanyiko na matukio makubwa. WHO itatoa msaada wa kiufundi, nyenzo, na uratibu ili kuhakikisha utekelezaji unawafikia zaidi wale walio katika hatari kubwa.

Kuongezeka kwa joto duniani na wimbi la joto la mara kwa mara kunasababisha ongezeko la magonjwa na vifo vinavyohusiana na joto, hasa kwa wafanyakazi wa nje na makundi yaliyo hatarini. WHO inakadiria kuwa ifikapo mwaka 2050, mawimbi ya joto yanaweza kusababisha zaidi ya vifo milioni 1.6 kila mwaka, huku uchafuzi wa hewa ukiendelea kusababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 4 kila mwaka.

“Mabadiliko ya tabianchi si tishio la siku za usoni tena bali ni uhalisia wa kila siku,” anasema Daktari Honest Anicetus, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mazingira na Udhibiti wa Uchafuzi katika Wizara ya Afya. “Mpango huu wa Beat the Heat utasaidia nchi kama Tanzania kubadilisha maandalizi kuwa vitendo, kwa kutumia nyenzo za kulinda maisha dhidi ya hatari za kimazingira zinazoendelea kuongezeka.”

Kwa kuwa miongoni mwa waasisi wa mpango huu, Tanzania inaonesha dhamira yake ya kujenga mifumo ya afya inayoweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi, kuboresha usalama kazini, na kuhakikisha matukio makubwa kama CHAN 2025 yanakuwa salama kwa wote watakaoshiriki.