Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tulia Ackson: Rais wa IPU atoa wito wa kulinda mifumo ya ushirikiano wa kimataifa

Maspika wa Bunge wakikusanyika kwa picha ya pamoja katika mlango wa Ukumbi wa Mkutano Mkuu, UMOJA WA MATAIFA, Geneva, Uswisi.
© IPU Maspika wa Bunge wakiwa katika picha ya pamoja kwenye mlango wa Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi - 30 Jul 2025. Katikati, kutoka kushoto kwenda kulia: Maja Riniker, Rais wa Baraza la Kitaifa la Uswisi (mwenye nguo nyekundu); Tatiana Valovaya, Mkurugenzi Mkuu, Umoja wa Mataifa huko Geneva; Tulia Ackson, Rais, IPU na Martin Chungong, Katibu Mkuu, IPU.

Tulia Ackson: Rais wa IPU atoa wito wa kulinda mifumo ya ushirikiano wa kimataifa

Na Anold Kayanda - New York
Masuala ya UM

Rais wa Shirikisho la Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, ametoa wito mzito kwa viongozi wa mabunge duniani kulinda na kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa akitetea nafasi muhimu ya Umoja wa Mataifa ambao bado na umuhimu mkubwa duniani.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Sita wa Spika wa Mabunge Duniani unaoendelea jijini Geneva, Uswisi, Dkt. Tulia amesema licha ya changamoto zinazoukumba mfumo wa kimataifa, bado ndio tumaini bora la dunia katika kutafuta amani, haki na ustawi kwa wote.

“Lazima tukatae simulizi hasi zinazoonesha Umoja wa Mataifa kama taasisi isiyo na nguvu na isiyohitajika. Wanaofanya hivyo wanajaribu kwa makusudi kudhoofisha mfumo wa kimataifa kwa manufaa ya wachache wenye nguvu.” anasema Tulia mbele ya zaidi ya Maspika 100 kutoka nchi mbalimbali na anaongeza akisema, “wale wanaojaribu kudhoofisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa na nafasi kuu ya Umoja wa Mataifa wanafanya hivyo kwa makusudi ili kudhoofisha kanuni zilizowekwa kwa ajili ya manufaa ya jumuiya yote ya kimataifa.”

Dkt. Tulia anaeleza kuwa Kanuni dhaifu siku zote hunufaisha wenye nguvu zaidi ambao wana uwezo wa kulazimisha matakwa yao kwa wengine, wakati mwingine bila kuadhibiwa. Tushirikiane kuhakikisha tunalinda na kuimarisha taasisi hii muhimu. Hili ni jukumu letu kama Maspika na viongozi wa mabunge tukifanya kazi kwa ajili ya ustawi wa watu wetu.

Katika hotuba hiyo, Dkt. Tulia alinukuu kauli maarufu ya Rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy, akisema: “Usiulize nchi yako inaweza kukufanyia nini. Uliza unaweza kuifanyia nini nchi yako,” na kuongezea kwa msisitizo, “Uliza unaweza kuifanyia nini dunia.”

Mkutano huo wa siku tatu unaendelea mjini Geneva ukihusisha viongozi wa mabunge kutoka zaidi ya nchi 115, ukijadili mustakabali wa ushirikiano wa kimataifa katika nyakati hizi za migogoro na mivutano ya kidunia.