Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkutano wa kimataifa wa mwaka 2025 kuhusu afya na tabianchi waanza leo huko Brasília, Brazil

Rivière Peruaçu, Brazil.
© UNESCO/Adriana Zehbrauskas
Rivière Peruaçu, Brazil.

Mkutano wa kimataifa wa mwaka 2025 kuhusu afya na tabianchi waanza leo huko Brasília, Brazil

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa Kimataifa wa mwaka 2025 kuhusu afya na tabianchi umeanza rasmi leo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Brazil (CICB), jijini Brasília, Brazil. Mkutano huu wa siku tatu, unaofanyika kuanzia leo tarehe 29 hadi 31 Julai 2025, unawaleta pamoja mawaziri wa afya, mazingira na tabianchi, wataalamu wa kiufundi, watafiti, viongozi vijana na asasi za kiraia kutoka duniani kote kwa lengo la kushirikishana mafanikio na kuongeza kasi ya hatua kuhusu afya katika muktadha wa mabadiliko ya tabianchi.

Lengo kuu la mkutano huo ni kuhakikisha afya ya jamii inawekwa kuwa nguzo kuu katika ajenda ya tabianchi kuelekea Mkutano wa COP30 utakaofanyika baadaye mwaka huu. Mkutano unalenga kuimarisha na kusambaza ushahidi uliopo kuhusu utekelezaji wa sera za kiafya za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuangazia manufaa ya kiafya yanayoweza kupatikana kupitia hatua za haki na zenye malengo makubwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano huu umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Brazil, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Shirika la Afya la Pan-Amerika (PAHO), na Muungano wa Hatua za Mabadiliko ya Tabianchi na Afya (ATACH).

Toleo la mwaka huu ni la tano (V) tangu kuanzishwa kwa mkutano huu wa kimataifa na pia linahudumu kama kikao cha ana kwa ana( in person )cha kila mwaka kwa wanachama wa ATACH.

Katika muktadha huo, mkutano huu unaweka mkazo mkubwa kwenye usawa wa kiafya na ushiriki wa jamii kama vipengele muhimu vya ajenda ya hatua katika sekta ya afya.

Muundo na maudhui ya mkutano

Katika kipindi cha siku tatu, washiriki wanashiriki katika vikao vikuu, majadiliano ya paneli, warsha, mijadala ya wazi na vipindi vya ubunifu vya “Idea Labs”. Mada kuu zitazingatia nguzo tatu kuu za Mpango wa Hatua wa Afya wa Belém:

  • Ufuatiliaji na uangalizi wa afya
  • Mikakati ya sera na uimarishaji wa uwezo kulingana na ushahidi
  • Ubunifu na uzalishaji 

Yanayotarajiwa

Mkutano huu unatarajiwa kutoa matokeo makuu yafuatayo:

  • Mchango halisi katika Mpango wa Hatua wa Afya wa Belém;
  • Uelewano wa pamoja kuhusu wajibu na ahadi za nchi wanachama wa ATACH katika kuunga mkono mpango huo;
  • Njia mahsusi za kuimarisha nafasi ya afya kama nguzo ya msingi ya hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kuelekea COP30;
  • Ushahidi wa kisayansi utakaosaidia utekelezaji wa Mpango wa Hatua wa Afya wa Belém.

Kwa ujumla, mkutano huu ni jukwaa muhimu la kimataifa linalotoa nafasi ya kuonesha ubunifu, kubadilishana uzoefu, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili kulinda afya ya jamii katika enzi ya mabadiliko ya tabianchi.