Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa Gaza ni mtihani ambao hatuwezi kumudu kuushindwa – Guterres baada ya ripoti ya IPC

Mtoto mwenye utapiamlo anatibiwa katika Hospitali ya Al Helou huko Gaza
© UNICEF/Rawan Eleyan Mtoto mwenye utapiamlo anatibiwa katika Hospitali ya Al Helou huko Gaza

Njaa Gaza ni mtihani ambao hatuwezi kumudu kuushindwa – Guterres baada ya ripoti ya IPC

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa onyo kali kufuatia ripoti ya  Kipimo Jumuishi cha Upatikanaji wa Chakula (IPC), ambayo inathibitisha kuwa Gaza iko ukingoni kuangukia katika baa la njaa.

“Huu ni mtihani wa ubinadamu wetu wa pamoja – mtihani ambao hatuwezi kumudu kuushindwa.” Amesema Guterres katika wito wake wa dharura, uliosambazwa asubuhi ya leo ya Julai 29 kwa saa za New York, Marekani.
 
Kwa mujibu wa tahadhari ya IPC, viashiria vya ulaji wa chakula na lishe vimefikia viwango vibaya zaidi tangu kuanza kwa mzozo, huku vizingiti viwili kati ya vitatu vya kutangaza njaa vikiwa tayari vimevukwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda huo.
 
Katibu Mkuu ameeleza hali hiyo kuwa “janga la kibinadamu la kiwango cha kutisha,” akisisitiza kuwa hii si tena tahadhari ya hatari bali ni hali halisi inayojitokeza mbele ya macho yetu. “Ukweli upo  na haupingiki,” amesema.
 
Akihimiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka na thabiti, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa ametaka misaada iongezwe kwa kiwango kikubwa, akisema kuwa mtiririko wa sasa wa misaada ni hafifu na lazima ubadilike kuwa “bahari.” Ametaka chakula, maji, dawa na mafuta viletwe bila vikwazo vyovyote, akionya kuwa ucheleweshaji zaidi unaweza kusababisha vifo vya watu wengi.
 
Katibu Mkuu pia amesisitiza hitaji la kusitishwa mara moja na kwa kudumu kwa mapigano ya kibinadamu, kuachiliwa kwa mateka wote bila masharti yoyote, na kupatikana kwa ufikiaji kamili wa kibinadamu katika ukanda mzima wa Gaza.