Ushahidi dhahiri Gaza wa kuenea kwa njaa na ukosefu wa chakula
Ushahidi dhahiri Gaza wa kuenea kwa njaa na ukosefu wa chakula
"Hali mbaya kabisa ya njaa kwa sasa inajitokeza Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli," wamesema hii leo wataalamu wa uhakika wa chakula wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, wakitoa wito wa kuchukuliwa hatua haraka, katikati ya mzozo unaoendelea, watu kuhama kwa wingi, na karibu kuporomoka kabisa kwa huduma muhimu katika ukanda huo uliokumbwa na vita.
Kwa mujibu wa ripoti ya Kipimo Jumuishi cha Upatikanaji wa Chakula, IPC kinachotoa vipimo vya kiwango cha njaa, vigezo viwili kati ya vitatu vya kuthibitisha njaa vimeshafikiwa Gaza. Navyo ni kupungua sana kwa ulaji wa chakula na utapiamlo mkali.
Kuna ushahidi unaoongezeka kuwa "njaa iliyoenea, utapiamlo na magonjwa" vinasababisha ongezeko la vifo vinavyohusiana na njaa – ambacho ni kigezo cha tatu cha kutambua njaa.
"Hili ni janga linalojitokeza mbele ya macho yetu, mbele ya skrini za runinga zetu," amesema Ross Smith, Mkurugenzi wa Masuala ya Dharura wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP). "Hili si onyo, huu ni wito wa kuchukua hatua. Hatujawahi kuona kitu kama hiki katika karne hii," amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi.
Hakuna chakula – kwa siku kadhaa
Muktadha wa tahadhari hiyo ni wa kutisha: mtu 1 kati ya 3 sasa anakosa chakula kwa siku kadhaa mfululizo, kwa mujibu wa IPC.
Hospitali zimelemewa na zimetibu zaidi ya watoto 20,000 wenye utapiamlo mkali tangu mwezi Aprili.
Takriban watoto 16 walio na umri wa chini ya miaka mitano wamefariki kutokana na sababu zinazohusiana na njaa tangu katikati ya Julai.
Tahadhari hii inafuatia tathmini ya IPC ya mwezi Mei 2025 iliyotabiri viwango vya kutisha vya ukosefu wa chakula kwa watu wote ifikapo Septemba. Kwa mujibu wa wataalamu wa jukwaa hilo, angalau watu nusu milioni wanatarajiwa kuwa katika Awamu ya 5 ya IPC – yaani janga – ambayo inaashiria njaa, ufukara wa hali ya juu, na vifo.
Mgogoro huu unasababishwa na takribani miaka miwili ya mzozo uliosababishwa na mashambulio ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 2023, ambayo yaliua takriban watu 1,250 na kuwateka nyara watu wengine wapatao 450.
Kwa mujibu wa mamlaka ya afya ya Gaza, mapigano makali yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 59,500, na kuharibu asilimia 70 ya miundombinu ya ukanda huo.
Kama ambavyo mashirika ya misaada yamekuwa yakieleza, tathmini ya IPC imethibitisha kuwa watu wanahama kwa wingi, huku maeneo salama yakiwa yamesalia chini ya asilimia 12 ya eneo lote la Gaza.
Sitisho la mapigano sasa hivi
Gaza ina idadi ya watu takriban milioni 2.1, na asilimia 90 tayari wamehamishwa, wengi wao mara kadhaa. Zaidi ya watu 762,500 wamehamishwa tangu kumalizika kwa usitishaji mapigano tarehe 18 Machi.
Wakati huohuo, upatikanaji wa misaada ya kibinadamu umekuwa mgumu sana, kwa kuwa misafara ya misaada mara nyingi hukumbwa na vizuizi au kuporwa.
Jumapili iliyopita, Israel ilitangaza kuwa itaanza sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu kila siku huko Gaza. Zaidi ya malori 100 ya misaada yaliripotiwa kuingia siku hiyo, lakini Umoja wa Mataifa bado unasema kuna umuhimu wa kupeleka chakula, mafuta na dawa kwa wingi Gaza.
Sambamba na wito wa kimataifa wa kumaliza vita, jukwaa la IPC pia linatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na bila masharti, upatikanaji usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu, na urejeshaji wa huduma muhimu. Ripoti hiyo inaonya kuwa vifo vya watu wengi vinakaribia kutokea iwapo hakutakuwa na uingiliaji wa haraka.
Wataalamu wa uhakika wa chakula pia wameomba ulinzi kwa raia, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na afya, maji, usafi wa mazingira, barabara na mitandao ya mawasiliano.
Mambo muhimu
- Njaa hutangazwa rasmi iwapo vigezo vyote vitatu vikuu vitafikiwa: kushuka kwa ulaji wa chakula, utapiamlo mkali, na vifo vinavyotokana na njaa. Ni vigumu sana kupata data sahihi kuhusu utapiamlo na vifo vinavyohusiana na njaa kwa sababu mifumo ya afya "inaporomoka," WFP na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) wameeleza katika tahadhari ya pamoja.
- Watoto walio hatarini: Zaidi ya watoto 20,000 wametibiwa kwa utapiamlo mkali; vifo 16 vimeripotiwa.
- Kusambaratika kwa miundombinu: Asilimia 70 ya miundombinu ya Gaza imeharibiwa.
- Mgogoro wa uhamishaji: Maeneo salama sasa ni chini ya asilimia 12 ya Ukanda wa Gaza.
Kwa maelezo zaidi kuhusu IPC na kazi yake ya kufuatilia njaa na hali za baa la njaa tembelea hapa.
Ripoti zilionesha Jumanne kuwa watu 60,000 wa Gaza wameuawa tangu mashambulio ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas nchini Israel yalipoanzisha vita mnamo Oktoba 2023.
"Katika Gaza, wanawake na wasichana wanakabiliwa na chaguo lisilowezekana la kufa kwa njaa katika makazi yao au kutoka kutafuta chakula na maji kwa hatari kubwa ya kuuawa," amesema Sofia Calltorp, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake, UN Women mjini Geneva.
Matarajio ya mkutano unaofanyika New York
Bi. Calltorp pia amesisitiza wito wa UN Women wa kuhakikisha upatikanaji usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu kwa wanawake na wasichana wote, kuachiliwa kwa mateka wote na kusitishwa kwa mapigano mara moja.
"Pia tunaunga mkono matarajio kuwa Mkutano wa Kimataifa wa Ngazi ya Juu kuhusu Suluhisho la Amani kwa Swali la Palestina wiki hii utakuwa hatua ya mwelekeo mpya, kuelekea suluhisho la mataifa mawili, ambapo Israel na Palestina wataishi kwa amani na usalama," ameongeza, akimaanisha juhudi za Ufaransa na Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa New York.
Alipoulizwa kuhusu ufanisi wa misaada inayowasilishwa kwa kurushwa kutoka angani iliyoanza kutolewa Gaza, Bwana Smith wa WFP ameeleza kuwa ni "hatua ya mwisho kabisa inapokosekana njia nyingine yoyote ya usafirishaji au vifaa vya misaada."
Aidha amesema kuwa misaada ya anga ni "ghali mno na haifai," na inahusisha "hatari kubwa sana" kwa watu wanaoishi katika mazingira yenye msongamano mkubwa, huku taarifa zikionyesha kuwa watu 11 walijeruhiwa Jumapili.
Mashirika yasihi yapate fursa kuingia Gaza kikamilifu
Mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yameendelea kusisitiza haja ya kupata fursa ya kuingia Gaza kikamilifu ili kuwafikia watu walio katika hatari kubwa, zaidi ya tangazo la jeshi la Israel la kusimamisha mapigano kwa muda kwa wiki nzima kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 2 usiku.
"Tunakaribisha kipindi cha sitisho la mapigano kwa misingi ya kiutu, na tungetaka kuona nia ya sitisho hilo ikitekelezwa kikamilifu, hadi kufikia maeneo ya kugawa misaada, ili tuweze kusonga kwa haraka na kwa ufanisi," amesema Bw. Smith.
"Hadi pale ucheleweshaji, idhini, na mwingiliano kati ya vikosi vya kijeshi na raia ardhini utakapoboreshwa – hatutaweza kuona mabadiliko ya kutosha ya kubadili hali ya kibinadamu ndani ya Gaza,” amesema Smith.