Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtu 1 hufariki dunia kila baada ya sekunde 30 kutokana na homa ya ini (Hepatitis)

Sehemu ya kusubiria matibabu katika Kituo cha Afya cha Musovu wilayani Bugesera, Rwanda. Chanjo ya hepatitis B katika dozi ya kuzaliwa ni asilimia 45 tu ulimwenguni, na chini ya asilimia 20 ya chanjo katika kanda ya Afrika ya WHO.
© WHO/Isaac Rudakubana
Sehemu ya kusubiria matibabu katika Kituo cha Afya cha Musovu wilayani Bugesera, Rwanda. Chanjo ya hepatitis B katika dozi ya kuzaliwa ni asilimia 45 tu ulimwenguni, na chini ya asilimia 20 ya chanjo katika kanda ya Afrika ya WHO.

Mtu 1 hufariki dunia kila baada ya sekunde 30 kutokana na homa ya ini (Hepatitis)

Afya

Ikiwa leo dunia inaadhimisha Siku ya kuelimisha umma kuhusu Homa ya Ini  duniani, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limetoa wito kwa serikali na wadau kuchukua hatua za haraka ili kutokomeza homa ya ini kama tishio la afya ya umma na kupunguza vifo vinavyotokana na saratani ya ini.

Katika taarifa yake aliyoitoa hii leo kutoka Geneva Uswisi Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ameeleza kuwa “Kwa kila sekunde 30, mtu mmoja hufariki kutokana na magonjwa yatokanayo na homa ya ini au saratani ya ini inayosababishwa na homa ya ini. Lakini tuna zana za kuizuia.”

WHO, kwa kushirikiana na Rotary International na World Hepatitis Alliance, inaongoza kampeni ya mwaka huu kwa kauli mbiu “Homa ya Ini: Tuivunje Kabisa”, ikisisitiza umuhimu wa kutokomeza unyanyapaa, kuongeza fedha na kushirikisha jamii katika mapambano haya.

Homa ya ini aina ya A, B, C, D na E husababisha maambukizi ya ghafla ya ini.

Tweet URL

Aina za B, C na D ndizo zinazoendelea kuwa sugu mwilini na kuongeza hatari ya ini kushindwa kufanya kazi au kupata saratani. Zaidi ya watu milioni 300 duniani wanaishi na aina hizi, na zaidi ya milioni 1.3 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo ya ini na saratani.

Kwa mara ya kwanza, Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC) limetangaza kuwa homa ya ini aina D ni kansajeni kwa binadamu, sawa na aina B na C. Homa ya ini D huwapata wale walio na homa ya ini B, na huongeza hatari ya kupata saratani ya ini kwa kiwango cha mara mbili hadi sita ikilinganishwa na kuwa na B pekee.

Daktari wa sayansi ya afya wa WHO Meg Doherty amesema “WHO tayari ilichapisha mwongozo wa upimaji na utambuzi wa homa ya ini aina B na D mwaka 2024, na inaendelea kufuatilia matokeo ya matibabu mapya ya aina D.”

Mgonjwa mwenye homa ya ini aina C inaweza kuponywa kwa kumeza dawa kwa kipindi cha miezi 2 hadi3, na aina B hudhibitiwa kwa matibabu ya maisha yote.

Tiba za homa ya ini aina D zinaendelea kuimarishwa, lakini mafanikio ya kweli yatapatikana tu ikiwa huduma za chanjo, upimaji, tiba na uzuiaji zitaingizwa kwenye mifumo ya afya ya msingi.