Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yalaani waasi wa ADF kwa kusababisha vifo vya watu 43 huko Komanda, DRC

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakipiga doria huko Ituri kaskazini mashariki mwa DR Congo. (Maktaba)
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakipiga doria huko Ituri kaskazini mashariki mwa DR Congo. (Maktaba)

MONUSCO yalaani waasi wa ADF kwa kusababisha vifo vya watu 43 huko Komanda, DRC

Amani na Usalama

MONUSCO, ambao ni Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kudumisha Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, imelaani vikali shambulio lililotokea usiku wa juzi tarehe 26 hadi jana 27 Julai 2025 huko Komanda (takribani kilomita 60 kusini-magharibi mwa Bunia), katika eneo la Irumu, jimboni Ituri, mashariki mwa nchi. 

Taarifa iliyotolewa na MONUSCO jijini katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa imeeleza kwamba kwa mujibu wa taarifa za uhakika, shambulio hilo lililofanywa na wapiganaji wa kundi la waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) limesababisha vifo vya raia wasiopungua 43 (wanawake 19, wanaume 15 na watoto 9).
 
Inaripotiwa kuwa waathirika wengi waliuawa kwa kutumia silaha za jadi wakiwa ndani ya nyumba ya ibada. Watu kadhaa walitekwa nyara. Nyumba na maduka pia yalichomwa moto, jambo ambalo limezidisha zaidi hali mbaya ya mazingira ya kibinadamu ambayo tayari ni ya kutisha katika jimbo hilo.
 
Naibu Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Masuala ya Ulinzi na Operesheni ambaye pia ndiye Kaimu Mkuu wa MONUSCO, Vivian van de Perre, amenukuliwa akisema, “mashambulizi haya ya kulenga raia wasio na hatia, hasa ndani ya nyumba za ibada, ni ya kushtusha na ni kinyume kabisa na viwango vyote vya haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu. MONUSCO itaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka za DRC ili kuwalinda raia kwa mujibu wa mamlaka yake.”
 
Kwa kushirikiana na mamlaka za eneo, MONUSCO imetoa msaada kwa hatua za awali, ikiwemo kuratibu shughuli za maziko na kutoa huduma za matibabu kwa majeruhi. Wakati huohuo, MONUSCO imeongeza juhudi za kiusalama ndani na nje ya eneo la Komanda kwa kuongeza idadi ya doria katika eneo hilo.
 
MONUSCO imeweka wazi kuwa inasalia na dhamira thabiti ya kushirikiana na mamlaka za DRC na jamii za wenyeji kusaidia kuzuia mashambulizi mengine, kuwalinda raia, kupunguza mvutano, na kuchangia katika kuimarisha utulivu katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko ya kivita.
 
Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa umeeleza masikitiko na ghadhabu kubwa juu ya vitendo hivi vya kikatili, ambavyo ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu. Ujumbe huu unatoa rambirambi zake za dhati kwa familia na jamii zilizoathirika na unasisitiza mshikamano wake na wakazi wa maeneo hayo. MONUSCO pia inazitaka mamlaka za DRC kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji haya na kuwafikisha wahusika mbele ya sheria.
 
Aidha, MONUSCO imeurudia wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa makundi yote ya waasi kutoka nchi za nje kuweka silaha chini bila masharti na kurejea katika nchi zao za asili.