UNESCO yahimiza dunia kutunza mikoko
Leo, tarehe 26 Julai dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Mifumo Ikolojia ya Mikoko, ikikumbusha na kusherehekea mchango mkubwa wa mikoko katika maisha ya binadamu na ustawi wa sayari yetu.
Mikoko ni mifumo ya kipekee ya ikolojia inayostawi kati ya ardhi na bahari. Inatoa hifadhi kwa viumbe hai mbalimbali, hulinda jamii za pwani dhidi ya dhoruba na mmomonyoko wa fukwe, huimarisha usalama wa chakula, na ina uwezo mkubwa wa kuhifadhi kaboni kwenye udongo wake hivyo kusaidia kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Licha ya umuhimu wake mkubwa, mikoko inazidi kutoweka kwa kasi ya kutisha mara tatu hadi tano zaidi kuliko misitu ya kawaida duniani. Katika kipindi cha miaka 40 iliyopita, dunia imepoteza nusu ya mikoko yake. Hii inaleta athari kubwa kwa mazingira, uchumi na jamii zinazotegemea mikoko kwa maisha yao ya kila siku.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, Audrey Azoulay katika ujumbe wake wa siku hii amesema mikoko ipo hatarini “Inakadiriwa kuwa zaidi ya robo tatu ya mikoko yote duniani iko kwenye hatari ya kutoweka pamoja na viumbe wote wa majini na nchi kavu wanaoitegemea.”
Kwa sababu hiyo Azoulay amesema “UNESCO inaendelea kuchukua hatua kuilinda, pamoja na mifumo mingine ya kaboni ya buluu, kupitia mitandao yake ya Hifadhi za Maisha, Maeneo ya Jiolojia ya Dunia, na Maeneo ya Urithi wa Dunia wa Asili."
UNESCO ilianzisha siku hii mwaka 2015 kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu thamani ya mikoko na kuhamasisha uhifadhi endelevu wa mifumo hii muhimu.