Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mwonekano wa anga la Nairobi, unaoonyesha Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) na majengo mengine marefu ya kisasa.

Maarifa ya Miji katika kuunda Sayansi ya Kimataifa ya Tabianchi

© Unsplash/Kenny Murgor Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

Maarifa ya Miji katika kuunda Sayansi ya Kimataifa ya Tabianchi

Tabianchi na mazingira

Miji ni nguzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini bado haijawakilishwa vya kutosha katika sayansi ya kimataifa ya tabianchi, hasa katika Nchi za Kusini mwa Dunia.

Hili ni pengo ambalo wataalamu na watendaji wamelenga kulishughulikia wakati wa warsha ya siku tatu iliyoratibiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la makazi(UN-HABITAT) kwa kushirikiana na Mkataba wa Kimataifa wa Mameya wa Tabianchi na Nishati (GCoM) tarehe 22 hadi 24 mwezi Julai, 2025 huko mjini Nairobi,Kenya.

Mkutano huo umewakutanisha waandishi zaidi ya 60 wa Jopo la Serikali Mbalimbali kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) na watendaji wa miji ili kuimarisha uhusiano kati ya sayansi na utendaji. Huku ukichagizwa na ajenda kuhusu Utafiti na Hatua ya Kimataifa kuhusu Miji na Sayansi ya Mabadiliko ya Tabianchi (GRAA), iliyoandaliwa wakati wa Mkutano wa Innovate4Cities wa 2024, ambayo inabainisha maeneo muhimu ya kuunganisha mitazamo ya ndani katika utafiti wa tabianchi.

Maarifa kutoka warsha hiyo yatasaidia kutoa taarifa katika ripoti maalum ijayo ya IPCC kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na miji (SRCities) – ripoti pekee ya IPCC iliyopangwa kabla ya tathmini ijayo ya Kimataifa chini ya Mkataba wa Paris. Kwa kuwa miji tayari inakabiliwa na athari mbaya za tabianchi, ripoti hiyo inaonekana kama fursa muhimu kwa sauti za mijini kutoa taarifa kwa hatua za kimataifa za tabianchi.

Washiriki wamechunguza jinsi uzoefu wa maisha – kutoka kusimamia uhamiaji na taka hadi kushughulikia makazi katika makazi yasiyo rasmi – unaweza kuboresha tathmini za kisayansi na kusababisha suluhisho zinazotekelezwa. Wamesisitiza ushirikishwaji wa watendaji kama washirika, kuunganisha mifumo mbalimbali ya maarifa, kurahisisha lugha ya kisayansi, kushughulikia habari potofu, na kurekebisha matokeo kulingana na mahitaji ya ndani ili utafiti ulete matokeo yanayoonekana katika miji.

Wafanyakazi wanne wa kilimo wanapumzika shambani, wamekaa chini ya miavuli mitatu mikubwa kwa ajili ya kivuli.
UN Photo/Mark Garten wafanyakazi wa mashambani Bogra, Bangladesh ( Maktaba)

Ziara za shambani kwenye makazi yasiyo rasmi ya Korogocho na Kibera jijini Nairobi, ziliwaruhusu washiriki kuona jinsi jamii zinavyokuza uthabiti na kuongoza suluhisho za ndani za tabianchi licha ya rasilimali chache. Ziara hizi zimeonesha hitaji la haraka la fedha za tabianchi kufikia ngazi za chini, umuhimu wa kukusanya gharama zote za kijamii na kiuchumi za hatua za tabianchi, na hitaji la uwakilishi sawa zaidi wa data kutoka Nchi za Kusini mwa Dunia katika utafiti wa kimataifa wa tabianchi.

“Tunakabiliwa na migogoro ya makazi duniani kote, na jinsi tunavyoshughulikia makazi sasa na siku zijazo, itakuwa na mchango mkubwa katika changamoto tunazokabiliana nazo. Tunahitaji kupanga matumizi ya ardhi kwa njia inayokidhi mahitaji ya kiikolojia na ya wanajamii katika jamii “ amesema Anacláudia Rossbach, Mkurugenzi Mtendaji wa UN‑HABITAT.

Warsha hiyo pia imechagiza maendeleo ya Kituo cha Maarifa ya Tabianchi ya Jiji, jukwaa linalotumia akili bandia ambalo linakusanya machapisho yaliyopitiwa na wataalamu na machapisho yasiyo rasmi ili kuimarisha ushirikiano kati ya sayansi, sera na utendaji. Mashauriano yatazinduliwa katika miezi ijayo ili kuunda awamu inayofuata ya Kituo hicho.

Kwa kuwaunganisha watafiti, wataalamu, na jamii za mitaa, warsha hii imethibitisha tena dhamira ya UN-Habitat na GCoM ya kuhakikisha kwamba maarifa na uzoefu kutoka miji mbalimbali vinachangia ripoti ya SRCities na michakato mingine muhimu kama vile COP30, Mkutano wa Innovate4Cities wa mwaka 2026, na kikao cha 13 cha Jukwaa la Miji Duniani (WUF13), ili kuharakisha mabadiliko ya miji kuelekea kuwa ya haki na yenye ustahimilivu duniani kote.