Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mtazamo wa Jiji la Gaza kutoka majini, huku moshi mwingi mweusi ukitoka katika eneo la mjini.

Türk: Dunia ichukue hatua kulinda Wapalestina

© UNICEF/Mohammed Nateel Mashambulizi ya anga yanalenga eneo la magharibi la mji wa Gaza.

Türk: Dunia ichukue hatua kulinda Wapalestina

Haki za binadamu

Hii leo katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa hapa jijini New York, Marekani, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinajadili kuhusu hali ya Palestina, kwenye mkutano wa ngazi ya juu unaolenga kujadili suluhu ya kudumu kwa mgogoro huo unaodumu kwa miongo kadhaa.

Kabla ya mkutano huo kuanza, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametoa ujumbe mzito akizitaka serikali duniani kote kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mauaji yanayoendelea huko katika Ukanda wa Gaza unaokaliwa kimabavu na Israel Pamoja na Ukingo wa Magharibi.

Katika taarifa yake ya video, Türk ameitaka Serikali ya Israel kusitisha mara moja uwepo wake kinyume cha sheria katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu. Aidha, amezitaka pande zote katika mzozo huo kufanikisha maendeleo ya kweli kuelekea suluhisho la mataifa mawili.

Türk amesema “Naziomba serikali zitumie mkutano huu kama fursa ya kuchukua hatua halisi, kwa kutumia kila mbinu kuishinikiza Israel kusitisha mauaji ya Gaza kwa njia ya kudumu. Mataifa yatakayoshindwa kutumia ushawishi wao yanaweza kuchukuliwa kuwa washirika wa uhalifu wa kimataifa.”

Kamishna huyo amesema kila siku dunia inashuhudia janga lisiloelezeka katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, likijumuisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, mauaji ya raia, na kupotea kabisa kwa utu wa watu wa Palestina.

Amesema watoto wanakufa kwa njaa mbele ya macho ya dunia, huku Gaza ikigeuka kuwa eneo la maangamizi ya kutisha.

Msichana mdogo wa Kipalestina huko Gaza anaweka mkono wake kichwani, akiwa ameshika bakuli tupu la chuma huku akisubiri juani.
UN News Msichana mdogo huko Gaza akiwa na kichwa chake mkononi, sufuria tupu iliyoshikiliwa karibu akisubiri chini ya jua kali, Macho yake, yakiwa yamechoka lakini yamejaa nguvu tulivu, yanaonesha mzigo ambao mtoto anapaswa kubeba - maumivu ya njaa, mkanganyiko wa migogoro, na akitumainia maisha ya kawaida ya amani.

Ugawaji misaada

Turk ameshutumu pia kile alichokiita mifumo ya ugawaji misaada ya kibinadamu isiyo na utaratibu, inayoendeshwa na taasisi zinazoungwa mkono na Marekani na Israel, ambayo imeshindwa kabisa kuwafikia wahitaji kwa kiwango kinachotakiwa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, zaidi ya watu 200,000 wameuawa au kujeruhiwa tangu Oktoba 7 mwaka jana, sawa na asilimia kumi ya wakazi wote wa eneo hilo.

Kamishna huyo amekumbusha kuwa zaidi ya wafanyakazi 300 wa Umoja wa Mataifa wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Israel.

Katika Ukingo wa Magharibi, Türk amesema vikosi vya usalama vya Israel pamoja na walowezi wameendelea kuua raia wa Palestina, kubomoa nyumba, kukata huduma za maji, na kuendeleza mfumo wa ukandamizaji na ubaguzi.

Ameeleza pia kuwa amelaani vikali mashambulizi ya kutisha ya Oktoba 7 yaliyofanywa na Hamas na makundi mengine ya Palestina, lakini akasisitiza kuwa hiyo haipaswi kuwa sababu ya kuhalalisha kiwango kikubwa cha maangamizi yanayoendelea Gaza.

Kwa mara nyingine tena, Türk ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja na kwa kudumu, kuachiliwa kwa mateka wote bila masharti, kuruhusu misaada ya kibinadamu kufika bila vikwazo, na kufikisha misaada hiyo kwa kiwango kikubwa kwa watu wote wa Palestina, popote walipo.

Amehitimisha kwa kusema kuwa dunia itaihukumu mikutano ya aina hii kwa kile inachokifanya kwa vitendo, na kuongeza kuwa ofisi yake iko tayari kusaidia taifa la Palestina katika ujenzi wa nchi yenye msingi wa haki za binadamu na utawala wa sheria, pindi utulivu utakapopatikana.