Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mtoto mwenye utapiamlo anatibiwa katika Hospitali ya Al Helou huko Gaza

WHO: Viwango vya Utapiamlo Vimefikia Hali ya Kutisha Gaza

© UNICEF/Rawan Eleyan
Mtoto mwenye utapiamlo anatibiwa katika Hospitali ya Al Helou huko Gaza

WHO: Viwango vya Utapiamlo Vimefikia Hali ya Kutisha Gaza

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa Afya Duniani (WHO) limetoa onyo kali kuhusu ongezeko la kutisha la utapiamlo katika Ukanda wa Gaza unaokaliwa kimabavu na Israel, likieleza kuwa watu wengi, wakiwemo watoto wadogo, wanakufa kutokana na njaa na hali hiyo inaweza kuzuilika.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa hii leo kutoka Geneva Uswisi, Cairo Misri na Jerusalemu imeeleza kuwa kati ya vifo 74 vinavyohusiana na utapiamlo vilivyoripotiwa mwaka huu, 63 vilitokea mwezi Julai pekee. Miongoni mwao, 24 walikuwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano, mtoto mmoja mwenye umri wa zaidi ya miaka mitano, na 38 walikuwa watu wazima.

WHO imesema wengi walifariki wakifika hospitalini au muda mfupi baada ya kufikishwa, huku miili yao ikionesha dalili za wazi za kudhoofika kwa kiwango cha unyafuzi.

WHO inasema kuwa janga hili lingeweza kuzuilika kabisa kama misaada ya chakula, afya na kibinadamu isingekuwa ikizuiliwa kwa makusudi au kucheleweshwa.

Mtoto anayekabiliwa na utapiamlo mkali amelazwa katika hospitali ya Abdel Aziz Al-Rantisi katika Ukanda wa Gaza.
UN News
Mtoto anayekabiliwa na utapiamlo mkali amelazwa katika hospitali ya Abdel Aziz Al-Rantisi katika Ukanda wa Gaza.

Takwimu

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa karibu mtoto mmoja kati ya watano chini ya miaka mitano huko mjini Gaza ana utapiamlo mkali. Viwango vya Utapiamlo Mkali wa Kimataifa (GAM) vimeongezeka mara tatu tangu mwezi Juni, huku maeneo ya Khan Younis na Eneo la Kati yakishuhudia ongezeko mara mbili kwa kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Hata hivyo, WHO imesema hali halisi huenda ni mbaya zaidi kutokana na ukosefu wa usalama na ugumu wa upatikanaji wa huduma unaowazuia familia nyingi kufika hospitalini.

Katika wiki mbili za mwanzo za mwezi Julai pekee, zaidi ya watoto 5000 walio chini ya miaka mitano walilazwa kwa matibabu ya utapiamlo, asilimia 18 wakiwa na Utapiamlo Mkali Sana au unyafuzi ambayo ni hali hatari zaidi ya utapiamlo.

Zaidi ya watoto 73 wenye unyafuzi na matatizo ya kiafya walipelekwa hospitalini mwezi huu wa Julai, ikilinganishwa na watoto 39 mwezi Juni, na kufikisha idadi ya mwaka huu hadi 263.

Idadi hii kubwa inazidi uwezo wa vituo vinne pekee vya matibabu ya utapiamlo vilivyopo Gaza, ambavyo tayari vinakabiliwa na uhaba wa mafuta na vifaa, hali inayoweza kusababisha kufungwa kwa vituo hivyo ifikapo katikati ya mwezi Agosti 2025.

Wajawazito

Kwa upande mwingine wa akina mama, wajawazito na wanaonyonyesha nao takwimu za WHO zimeonesha namna ambavyo wameathirika vibaya. Zaidi ya asilimia 40 wanakabiliwa na utapiamlo mkali.

Eneo la Kati la Gaza ndio limeelezwa kuwa limeathirika zaidi, huku viwango vikiongezeka mara tatu tangu mwezi Juni, na Katika Mji wa Gaza na Khan Younis vikishuhudia ongezeko mara mbili.

Kwa sasa, si njaa pekee inayoua bali pia harakati za kutafuta chakula. Tangu tarehe 27 Mei, zaidi ya watu 1060 wameuawa na wengine 7200 kujeruhiwa wakijaribu kufikia misaada ya chakula katika mazingira hatarishi na yenye vurugu.”

WHO inatoa wito wa haraka kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti na endelevu kupeleka misaada ya chakula chenye virutubisho mbalimbali kwa wingi katika Ukanda wa Gaza, pamoja na vifaa vya matibabu ya utapiamlo kwa watoto na makundi yaliyo hatarini. Misaada hii inapaswa kuwa ya mara kwa mara, bila vizuizi, ili kusaidia kufufua hali ya afya na kuzuia janga kubwa zaidi.

WHO pia inasisitiza wito wake wa:

  • Kulindwa kwa raia na wafanyakazi wa afya
  • Kuachiwa kwa mfanyakazi wake aliyekamatwa hivi karibuni Pamoja na mateka wote
  • Kusitishwa mara moja kwa mapigano ili kuruhusu upatikanaji wa huduma za afya na misaada ya kibinadamu.