Sitisho la mapigano Gaza: UN yakimbiza misaada kwa walio na njaa
Umoja wa Mataifa umekaribisha tangazo la Israel kusitisha mapigano kwasababu za kibinadamu katika Ukanda wa Gaza unaokaliwa kimabavu na Israel. Timu za Umoja wa Mataifa zinafanya kila jitihada kutumia fursa hii ya sitisho la mapigano ili kuwasilisha misaada kwa haraka kwa wale wanaohitaji msaada, kwani wakazi wote wa Ukanda huo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula huku kukiwa na idadi kubwa ya vifo kutokana na njaa hususani kwa watoto wadogo.
Taarifa zilizotolewa na mashirika mbali mbali ya Umoja wa Mataifa zote zinaeleza namna ambavyo vipo tayari kutekeleza kwa haraka uingizaji wa misaada Gaza tena kwa kiwango kikubwa kwani tayari wana shehena za kutosha kuwalisha zaidi ya wananchi milioni 2 walioko Gaza na ombi kubwa kwa sasa ni kufunguliwa kwa vivuko vingi zaidi ili kurahisisha uingizaji wa misaada.
Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, Tom Fletcher, kupitia mtandao wa kijamii wa X amesema “Tunakaribisha tangazo la usitishaji wa mapigano kwasababu za kibinadamu huko Gaza ili kuruhusu misaada ya kibinadamu kupita. Tunawasiliana na timu zetu zilizoko huko ambazo zitafanya kila tuwezalo kuwafikia watu wengi wenye njaa tuwezavyo katika kipindi hiki cha sitisho.”
UNICEF
Janga la njaa huko Ukanda wa Gaza linamuathiri kila mtu lakini idadi kubwa ya wanaopoteza maisha ni watoto.
Taarifa ya UNICEF imesema “Mtu mmoja kati ya kila watu watatu hajala kwa siku nyingi na asilimia 80 ya vifo vyote vinavyoripotiwa kutokana na njaa ni watoto. Hii ni fursa ya kuanza kubadili janga hili na kuokoa maisha.”
Pamoja na hali ngumu ya utendaji kazi huko Gaza, UNICEF haijawahi kusitisha kutoa huduma, mwezi huu wa Julai pekee shirika hilo liliweza kufikisha lori 147 zilizokuwa na lishe ikiwemo chakula cha watotao, maziwa na biskuti za kuongeza nguvu.
Shirika hilo limesema lipo tayari kuongeza idadi hiyo na kuhakikisha misaada zaidi ya kuokoa maisha inaingia Gaza kwa kiwango kinachohitajika na kuleta matumaini kwa idadi kubwa ya watu ambao wamechoka.
Shirika hilo limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, upatikanaji usio na vikwazo wa misaada ya kibinadamu kote Gaza, ulinzi wa watoto, na kuachiliwa kwa mateka wote ili waweze kurejea nyumbani kwa wapendwa wao.
WFP
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP linahusika moja kwa moja na utoaji wa chakula cha moto kwa kupitia majiko yake huko Ukanda wa Gaza unaokaliwa kimabavu na Israel. Kwa mujibu wa shirika hilo, msaada wa chakula ndio njia pekee ya kweli kwa watu wengi ndani ya Gaza kula.
Taarifa yake imeeleza kuwa “WFP ina chakula cha kutosha - au kiko njiani kinaelekea - katika eneo hilo ili kulisha wakazi wote wa Gaza ambao ni watu milioni 2.1 kwa karibu miezi mitatu.”
Wameongeza kuwa “Theluthi moja ya watu hawajala kwa siku kadhaa. Takriban watu 470,000 wanavumilia hali kama njaa. Wanawake na watoto 90,000 wanahitaji matibabu ya haraka ya lishe. Watu wanakufa kwa kukosa msaada wa kibinadamu.”
WFP imekaribisha taarifa kwamba Israel iko tayari kutekeleza usitishaji wa mapigano kwa sababu za kibinadamu, na kwamba korido maalum za kibinadamu zitaundwa, kuwezesha harakati salama za misafara ya Umoja wa Mataifa inayopeleka chakula cha dharura na misaada mingine kwa watu huko Gaza.
Ahadi hizi mpya za kuboresha hali ya uendeshaji wa shughuli za utoaji wa misaada ya kibinadamu zinakuja baada ya hakikisho la hapo awali kutoka kwa Israel la kuimarisha kuwezesha usaidizi wa kibinadamu.