Matangazo ya elimu kwa njia ya redio DRC yaimarisha ndoto ya Francine ya kuwa muuguzi
Alipoulizwa anapenda nini shuleni, Francine mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 12 alitazama juu kwa tabasamu la aibu. Anachokipenda zaidi ya yote ni kugundua mambo mapya — hasa katika somo la sayansi. Baadaye, ana ndoto ya kuwa muuguzi.
Francine anaishi katika kambi ya Kigonze, pembezoni mwa mji wa Bunia, jimboni Ituri, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Conog, DRC, kambi inayohifadhi maelfu ya watu waliofurushwa makwao kutokana mapigano kutoka makundi yaliyojihami.
Kama maelfu ya watoto wengine, alikimbia vurugu akiwa na familia yake, na kuacha nyuma shule yake, marafiki na mazingira aliyoyazoea. Leo, anaishi na shangazi yake na anasoma kupitia mpango wa masomo katika shule ya msingi ya Saint-Luc, iliyojengwa kwenye eneo hilo ili kujifunza kusiwe kumbukumbu iliyosahaulika kwa wakimbizi.
Bana Education ya Radio Okapi na UNICEF
Ndipo alipogundua Bana Education, au Elimu ya Bana, kipindi cha redio kinachorushwa na Radio Okapi, ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani nchini DRC, (MONUSCO), kilichoundwa kuwaletea elimu watoto ambao hawana tena njia rahisi ya kufika shuleni.
"Kipindi hiki cha redio kinatusaidia sana. Tunajifunza hisabati, Kifaransa, na hata sayansi vizuri zaidi. Mwalimu hutusaidia kufuatilia somo vizuri," anaeleza.
Kujifunza kupitia matangazo ya redio
Katika darasa moja, mwalimu anapunguza sauti ya kipaza sauti kilichounganishwa kwenye simu ya kiganjani. Takriban wanafunzi 30 wanasikiliza kwa makini. Sauti ya mwalimu redion inasikika wazi darasani. Somo la siku ni kuhusu ndege wa jamii ya kuku.
"Tunatumia redio moja kwa moja au marudio wanayotutumia. Shukrani kwa mwalimu anayezungumza kwa lugha rahisi kueleweka, watoto wanaweza kufuatilia masomo. Tunaona wanaelewa vizuri zaidi. Wanachangamka," anaeleza mwalimu.
Katika shule hii, kama zilivyo nyingine zilizo maeneo yenye upatikanaji mdogo wa elimu rasmi, Bana Education imekuwa nguzo ya elimu. Ni suluhisho adhimu mahali ambapo vitabu vya kiada ni adimu na walimu hawatoshi.
Mpango huu unaotekelezwa na Radio Okapi unawawezesha watoto waliokatisha masomo au wanaoishi maeneo yaliyoathiriwa vibaya na migogoro kupata msaada wa kielimu katika hisabati, sayansi, Kifaransa, na maarifa ya jumla — kwa njia rahisi, ya kushirikisha, na iliyobadilishwa kulingana na mahitaji yao.
Bana Education inatekelezwa kwa msaada wa MONUSCO na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu ya Msingi, Sekondari na Ufundi na Uraia Mpya, pamoja na Wizara ya Masuala ya Kijamii, Misaada ya Kibinadamu hapa DRC na Taasisi ya Mshikamano wa Kitaifa.
Mgawanyo wa madarasa na matokeo yenye mvuto na matarajio
Katika shule ya Saint-Luc, yenye wanafunzi 978 wakiwemo wasichana 555, watoto wamegawanywa katika ngazi tatu kulingana na historia yao ya kielimu. Kipindi cha redio kimeingizwa darasani ili kupanua upatikanaji wa elimu.
Loti Benoît, Mwalimu Mkuu katika shule ya Saint Luc anasema, “watoto wengi hapa wako katika mazingira magumu. Wengine wamepoteza miaka kadhaa ya masomo baada ya kukimbia vurugu. Wakati mwingine tunawapokea bila ripoti wala historia wazi. Bana Education ni msaada muhimu. Watoto wanataka kujifunza. Wanaposikia redio, macho yao hung'aa."
Anasisitiza faida ya programu hiyo, hasa kwa watoto walio katika madarasa ya mitihani akisema, “maswali kadhaa ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, au ENAFEP yalilenga dhana zilizotajwa kwenye vipindi, hasa maarifa ya jumla. Hii inasaidia kuinua kiwango chao."
Kusikiliza, kujifunza… na kuendelea kuota ndoto
Eliya, mwenye umri wa miaka 14, yuko darasa la sita. Alikimbia kutoka eneo la Djugu jimboni Ituri akiwa na familia yake. Anathibitisha umuhimu wa programu hiyo.
"Ninapenda masomo ya sayansi. Katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi, kulikuwa na swali kuhusu wanyama wanaotaga mayai. Nilijua jinsi ya kujibu kwa sababu niliisikia kwenye Bana Education!" Ndoto yake: kuwa daktari ili "kuponya watu katika jamii."
Katika kituo cha kujenga uelewa wa masomo cha TARAJA, pia mjini Bunia, Évodi, mwanafunzi wa ngazi ya tatu, anasimulia: "Mpango huu unaniokoa. Ninachokosa kuelewa vizuri darasani, nakisikiliza tena nyumbani wakati wa likizo. Siku moja nilikuwa na kazi ya nyumbani kuhusu virai vya kielezi, sikuielewa kabisa. Kisha nikasikiliza Bana Education, nikafanya zoezi vizuri na kupata alama nzuri."
Elimu, hata ikiwa ya mbali
Bana Education si kipindi cha kawaida tu cha redio ya shule. Ni mwanga wa matumaini unaorushwa kila siku kupitia matangazo ya redio. Ni ahadi ambayo maelfu ya watoto husubiri, mara nyingine wakiwa wamekusanyika karibu na redio ya zamani kwenye kituo chao cha mapokezi au nyumbani.
Katika jimo hili la Ituri lililogubikwa na migogoro kwa miaka mingi, mpango huu unarudisha maana ya kujifunza, hupanga ratiba ya siku, huleta mwendelezo, na zaidi ya yote, heshima ya binadamu.
Pamoja na kwamba elimu ni changamoto ya kila siku, leo kupitia mpango huu unaoendeshwa na Radio Okapi, msaada unachukua sura mpya — ile ya sauti, maarifa, na somo kwa sababu mtoto anayejifunza ni mtoto mwenye matumaini.