Siku ya kimataifa ya kuzuia kuzama majini 2025: Kuchukua hatua inapunguza vifo
Siku ya kimataifa ya kuzuia kuzama majini 2025: Kuchukua hatua inapunguza vifo
Leo ni Siku ya Kimataifa ya Kuzuia kuzama majini, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Julai, ni fursa ya kutafakari juu ya athari kubwa na za kuhuzunisha za kuzama majini kwa familia na jamii, na kutoa suluhisho muhimu za kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika.
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO huko Cairo, Misri imesema Kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita, takriban watu milioni 3 wamepoteza maisha kwa kuzama majini duniani. Ingawa vifo vya kuzama vimepungua tangu mwaka 2000, bado zaidi ya watu 300,000 hufariki kila mwaka. Kwa mwaka 2021 pekee, takriban vifo 300,000 vilirekodiwa, ambapo asilimia 12 (takriban 35,000) vilitokea katika Kanda ya Mashariki ya Mediterania.
Watoto na vijana ni waathirika wakuu
Kanda ya Mashariki ya Mediterania ina kiwango cha pili cha juu zaidi cha vifo vinavyotokana na kuzama kati ya kanda zote za WHO, ambapo vijana na watoto wenye umri wa chini ya miaka 29 wanachangia asilimia 83 ya vifo hivyo. Cha kusikitisha zaidi, Kanda hiyo ina kiwango cha juu zaidi cha vifo vya kuzama majini kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 4 duniani.
Aidha, kanda hii imeripoti kupungua kwa kiwango kidogo zaidi cha vifo vinavyotokana na kuzama majini kuliko kanda nyingine, jambo linaloonesha umuhimu wa kuchukua hatua madhubuti. Kiwango cha juu cha vifo katika nchi za kipato cha chini na cha kati, na pia kiwango cha pili kwa nchi tajiri, ni dalili ya hatari inayowakabili watu wote bila kujali maendeleo ya kiuchumi.
Jinsia, umri, umasikini na ukosefu wa usawa ni sababu kuu zinazoongeza hatari ya kuzama majini. Wanaume wako kwenye hatari mara mbili zaidi ya wanawake. Utafiti unaonesha kuwa wahamiaji, hasa katika Kanda ya Mashariki ya Mediterania, wako kwenye hatari kubwa zaidi. Aidha, takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa watu maskini na waliotengwa kijamii huathirika zaidi – kwa nchi za kipato cha chini, kiwango cha vifo hivyo ni mara 3.2 zaidi ikilinganishwa na nchi tajiri.
Sababu zinazoongeza hatari ya kuzama
Wadau katika eneo hili wameripoti sababu kadhaa zinazoongeza hatari ya kuzama maji, yakiwemo:
- Kuishi karibu na mabwawa, mito, maziwa na bahari
- Kukosekana kwa usimamizi au uangalizi kwa watoto
- Kuongezeka kwa shughuli za burudani zinazohusisha maji
- Maafa ya asili kama mafuriko ya ghafla
- Kusafiri kwa kutumia boti zilizojaza watu kupita kiasi
- Uvuvi wa kienyeji na hali mbaya ya hewa
- Uhamiaji haramu kupitia bahari au mito
Hata hivyo, baadhi ya nchi zimefanikiwa kupunguza viwango vya vifo kupitia utekelezaji wa hatua za kinga. Kwa sasa, asilimia 64 ya nchi katika kanda hii zinafanya jitihada zaidi ya wastani wa kimataifa katika kuzuia kuzama. Hatua hizi ni pamoja na:
- Huduma za onyo la hali ya hewa bila malipo
- Mifumo ya tahadhari dhidi ya majanga
- Uokoaji na uimarishaji wa uimara wa jamii dhidi ya majanga
- Mafunzo ya usalama wa maji na huduma za awali za kulelea watoto
- Kuweka vizuizi vya kimwili katika maeneo yenye hatari
Uhamasishaji Jamii
Kuelimisha jamii kuhusu usalama wa maji na kuandaa mipango ya kitaifa ya kuzuia kuzama majini ni muhimu katika kuhakikisha watu wanabaki salama wanapokuwa karibu na maji. Nchi zinaweza kuokoa maisha zaidi kwa kuhamasisha sera shirikishi kati ya sekta mbalimbali, kuongeza tafiti za kuelewa hatari za kuzama majini, kuendeleza mikakati madhubuti ya kuzuia na kufanya kampeni za uhamasishaji kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi.