Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu warejea Sudan, Mashirika ya UN yatoa wito wa msaada wa dharura

Wakimbizi wa ndani wanaishi katika makazi ya muda katika kituo cha mabasi cha zamani huko Gedaref, Sudan. Mahema yaliyotengenezwa kwa blanketi na tarpau zenye rangi nyingi huwekwa chini ya jengo kubwa, lenye pande wazi.
© UNOCHA/Giles Clarke Watu wengi wanarejea Sudan licha ya mustakabali usio na uhakika.

Maelfu warejea Sudan, Mashirika ya UN yatoa wito wa msaada wa dharura

Msaada wa Kibinadamu

Zaidi ya watu milioni 1.3 waliokimbia machafuko nchini Sudan wamerejea nchini mwao licha ya hali ya hatari inayozidi kushuhudiwa katika maeneo mengi ya nchi hiyo. Wengi wanarejea katika majimbo ya Khartoum, Sennar na Al Jazirah, ambako miundombinu imeharibiwa kabisa na huduma muhimu za kibinadamu hazipatikani.

Taarifa iliyotolewa leo huko Geneva Uswisi na mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa lile ya kuhudumia wakimbizi, UNHCR, linalohusika na uhamiaji IOM na la masuala ya maendeleo UNDP imetoa wito wa kutolewa kwa msaada wa dharura ili kuwasaidia wananchi hao ambao sasa wanaenda kuanza upya mifumo yao ya maisha baada ya kuharibiwa kabisa na vita

Wengi wa wakimbizi wanaorejea wanatoka katika nchi za Misri na Sudan kusini.

Yasemavyo mashirika ya UN

Kwa sasa, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa msaada wa kibinadamu unakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha. Mashirika hayo yameeleza yamepokea chini ya robo ya mahitaji ya dola bilioni 4.2 kwa ajili ya Sudan, na asilimia 16 tu ya dola bilioni 1.8 zinazohitajika kwa ajili ya wakimbizi walioko nje ya nchi.

Viongozi wa kikanda wa mashirika ya IOM na UNHCR wlaitembelea katika mji wa Khartoum na wanasema wamekuta miji ikiwa katika hali mbaya mno, huku maelfu ya watu waliolazimika kuhama makazi yao wakikosa msaada wa msingi.

Mkurugenzi wa Kanda wa UNDP, Abdallah Al Dardari, amesema kuwa bila msaada wa haraka, watu wanarejea katika miji iliyojaa magofu na ukosefu wa huduma “Tuko katika mbio dhidi ya muda kusafisha mabaki ya vita na kurejesha maji, umeme, na huduma za afya. Tunahitaji pia msaada wa muda mrefu kwa ajira, biashara na msaada wa kisaikolojia kwa manusura, hasa wanawake.”

Ingawa baadhi ya maeneo yameanza kuwa salama, bado kuna hatari kubwa kutokana na mabaki ya vilipuzi, ukatili wa kingono na ukiukwaji wa haki za watoto.

Othman Belbeisi, Mkurugenzi wa Kanda wa IOM, amesema suala la watu kurejea makwao ni la lazima liwe uamuzi wa hiari na wawe na taarifa za wanapoenda na kwamba “Wanaorejea si waathirika tu, bali ni msingi wa ujenzi wa upya wa Sudan. Wanahitaji msaada wetu ili kuanzisha tena maisha yao kwa heshima na matumaini.”

Kwa upande wakeMamadou Dian Balde, Mratibu wa Kikanda wa Wakimbizi kwa mzozo wa Sudan kutoka UNHCR amesema “Haya siyo tu matamanio ya watu kurejea nyumbani, bali ni kilio cha kukata tamaa kikielekeza haja ya kumaliza vita ili watu waweze kuanza upya maisha yao. Tunatoa wito kwa mshikamano wa kimataifa kusaidia watu wa Sudan na nchi jirani zinazowahifadhi.”

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kushirikiana na wadau wa ndani kusaidia kurejesha huduma za msingi na kutoa msaada wa dharura kwa jamii zinazowahifadhi waliorejea.