Dunia yaihitaji Amnesty International zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule – Guterres
Dunia yaihitaji Amnesty International zaidi kuliko wakati mwingine wowote ule – Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesisitiza kuwa Amnesty International ina nafasi muhimu isiyoweza kubadilishwa katika harakati za kulinda na kutetea haki za binadamu.
Katika hotuba hiyo ya kihistoria, Guterres – ambaye amekuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuzungumza katika mkutano wa kimataifa wa mwaka wa Amnesty International, – ameangazia umuhimu wa shirika hilo katika kulinda utu, kupinga dhuluma na kusimama kidete kwa wanyonge kwa zaidi ya miongo sita.
“Dunia inawakihitaji zaidi kuliko wakati wowote. Tunahitaji ujasiri wenu, ubunifu wenu, na msimamo wenu usioyumba,” amesema Guterres katika hotuba hiyo aliyoitoa kwa njia ya mtandao kutokea New York, Marekani.
Hali ya Gaza ni janga la maadili linalotikisa dhamira ya ulimwengu
Katibu Mkuu amegusia mateso yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, akisema ni zaidi ya janga la kibinadamu – ni janga la maadili linalopasua dhamira ya jumuiya ya kimataifa.
Ameelezea kwa masikitiko jinsi mashambulizi ya kijeshi ya Israeli, ukosefu wa huruma na ukimya wa kimataifa vinavyozidi kuacha majeraha ya kudumu kwa watu wa Gaza, hususan watoto.
Guterres amesema, wafanyakazi wetu mashujaa wanaendelea kuhudumu katika mazingira yasiyovumilika. Wengi wao wamechoka na wamekufa ganzi kiasi kwamba wanasema hawajisikii kama wako hai au wamekufa. Watoto wanazungumza juu ya kutamani kwenda mbinguni, kwa sababu, wanasema, angalau huko kuna chakula.
Kwa hiyo, tutaendelea kupaza sauti kila tutakapopata nafasi. Umoja wa Mataifa uko tayari kutumia kikamilifu fursa ya usitishaji mapigano ili kuongeza kwa kiwango kikubwa shughuli za kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, kama tulivyofanikiwa kufanya wakati wa kusitishwa kwa mapigano huko nyuma. Mipango yetu iko tayari, na imekamilika kabisa.
Waandishi wa habari na watetezi wa haki mashakani
Katika hotuba hiyo, Guterres ameelezea hofu yake kuhusu kuongezeka kwa mifumo ya kiimla duniani, ambapo viongozi wengi wanaona haki za binadamu kama tatizo badala ya suluhisho.
Amesema mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari, wanaharakati na mashirika ya kiraia yameongezeka kwa kasi ya kutisha – ikiwemo kuuwawa, kutishwa, na kunyimwa uhuru wa kujieleza.
“Tunaona wanahabari na wanaharakati wakinyamazishwa – hata kuuawa. Jamii za wachache zinasingiziwa. Wanawake na wasichana wananyang’anywa haki zao za msingi kabisa – kwa ukatili mkubwa, hasa nchini Afghanistan,” ameongeza.
Guterres ameweka wazi kuwa hii siyo hali ya kawaida bali ni "ugonjwa wa kimataifa" unaotishia misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.
Mapendekezo na wito wa haraka
Katibu Mkuu ametoa mapendekezo kadhaa muhimu katika kukabiliana na changamoto hizi:
- Kuhakikisha ulinzi wa uhuru wa vyombo vya habari na asasi za kiraia: Guterres amehimiza nchi zote kuheshimu na kulinda nafasi ya wanahabari na mashirika ya kiraia kama injini ya demokrasia na maendeleo.
- Kuwajibisha wanaokiuka haki za binadamu: Ameitaka jumuiya ya kimataifa kusimamia uwajibikaji bila upendeleo wala woga, na kulinda mfumo wa kimataifa wa haki za binadamu.
- Kupinga uongo na chuki mitandaoni: Ameonya kuwa mitandao ya kijamii imekuwa silaha ya tawala za kiimla katika kusambaza chuki, taarifa potofu, ubaguzi wa rangi na jinsia, na kuchochea migawanyiko.
- Kulinda mfumo wa kimataifa na kulifanya uwe wa kijumuishi: Amehimiza mabadiliko ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuimarisha ushiriki wa nchi zinazoendelea na kuhakikisha uwakilishi wa Afrika katika chombo hicho ambamo hivi sasa bara hilo halina kiti cha kudumu.
- Kuhimiza haki za mazingira na haki za kijamii: Akizungumzia suala la mabadiliko ya tabianchi, ameeleza kuwa ni "janga la haki za binadamu," na kwamba nchi zilizoendelea zinapaswa kuongoza kwa kupunguza hewa chafu na kufadhili juhudi za nchi zinazoendelea.
Ushujaa na mshikamano
Katika hitimisho lake, Katibu Mkuu amekumbuka maisha yake chini ya utawala wa kidikteta nchini Ureno na jinsi harakati za ukombozi Afrika zilivyochangia kuangusha utawala huo. Ameitaja Amnesty International kama mfano wa mshikamano na ujasiri wa kweli katika historia ya mapambano ya haki.
“Wakati unaposimama kwa ajili ya haki za binadamu, unakuwa upande sahihi wa historia... Tusikate tamaa kamwe,” amehitimisha.
Kwa ujumla, hotuba ya Katibu Mkuu ilikuwa wito wa kutafakari, kuchukua hatua, na kuunganisha nguvu katika mapambano ya kimataifa dhidi ya ukandamizaji, uongozi wa kidikteta, na ukosefu wa haki.
Amnesty International, kwa mujibu wa Katibu Mkuu, ni nguzo muhimu katika safari hiyo.