Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mawaziri wapitisha azimio kusongesha kasi ya utekelezaji wa SDGs

Li Junhua,  Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kiuchumi na kijamii
UN /Loey Felipe
Li Junhua, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kiuchumi na kijamii

Mawaziri wapitisha azimio kusongesha kasi ya utekelezaji wa SDGs

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mkutano wa Ngazi ya Juu wa kisiasa wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Kiuchumi na Kijamii, ECOSOC umekunja jamvi Alhamisi Julai 24 kwa kuridhia Azimio la Mawaziri kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs.

Azimio hilo la Mawaziri na Mkutano wa ngazi ya juu wa kikao cha mwaka 2025 cha ECOSOC na Mkutano wa Kisiasa wa Ngazi ya Juu, HLPF kwa mwaka 2025 vilivyofanyika chini ya usimamizi wa Baraza, vilibeba kaulimbiu: “Kusukuma mbele majawabu endelevu, jumuishi, ya kisayansi na yenye ushahidi kwa ajili ya Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu bila kumwacha mtu yeyote nyuma.”

Mawaziri kwa pamoja kupitia azimio hilo ambapo hata hivyo lilipigiwa kura ya Hapana na Marekani na Israeli huku Paraguay na Iran hazikushiriki kupiga kura, linaonesha utashi wa kisiasa wa kufanikisha SDGs kwa manufaa ya wakazi wote wa dunia.

Nchi 154 zilipiga kura ya ndio siku ya Jumatano Julai 23 rasimu ilipowasilishwa.

Kuelekea miaka 80 ya ECOSOC tunaona mchango wake

Li Junhua,  ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kiuchumi na kijamii amesema “tunapokaribia kuadhimisha miaka 80 ya ECOSOC Januari 2026, mjadala wa leo unathibitisha tena nafasi ya kipekee ya Baraza katika kuunganisha nguzo za kiuchumi, kijamii na mazingira za maendeleo endelevu.”

Tweet URL

Halikadhalika amesema mjadala unadhihirisha nafasi ya Baraza hilo ya kusukuma mbele utekelezaji jumuishi wa mifumo ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na SDGs, Mkataba wa Zama Zijazo, Ahadi ya Sevilla na Makubaliano ya Nice kuhusu bahari.

Hivyo Bwana Li amesema, “tuyachukue matokeo chanya ya mikutano hii ya kimataifa, tukijitoa upya kwa mshikamano wa kweli na wa uwakilishi mpana, ili kuendesha mabadiliko madhubuti yanayoweza kuhakikisha mustakabali wa ustawi, endelevu, wa amani na jumuishi kwa wote.”

Kauli ya Rais wa ECOSOC

Kwa upande wake, Bob Rae, ambaye ni Rais wa ECOSOC amesema “licha ya ugumu wa wakati huu na hisia zinazoambatana nao, ninafunga Mkutano huu wa Ngazi ya Juu uliofanyika kwa wiki mbili nikiwa na matumaini yanayoendelea. Sio kwa sababu njia iliyo mbele ni rahisi, bali kwa sababu sote tumeona kile tunaweza kufanya tunapofanya kazi kwa pamoja.”

Marekani na Israeli ndio zilizopinga Azimio hilo huku Paraguay na Iran wakijizuia kupiga kura.

Kwa kipindi cha wiki mbili, kuanzia Julai 14, jukwaa hili lilikutanisha ana kwa ana washiriki zaidi ya 6,000, wakiwemo wawakilishi wa serikali, vijana, asasi za kiraia, wanasayansi, sekta binafsi, na wadau wengine muhimu, ili kubadilishana uzoefu na kuangazia majawabu bunifu na jumuishi ya kusukuma mbele utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).