Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO na UNODC watoa ripoti kuu kuhusu dawa zilizochafuliwa, wakitaka hatua za haraka kuokoa maisha

Mikono ya wazee ikimimina vidonge vyeupe kutoka kwenye chupa ya dawa ya chungwa kwenye kiganja kilicho wazi dhidi ya mandhari ya kijivu.
© Unsplash/Towfiqu Barbhuiya Dawa iliyochafuliwa na kemikali ni hatari sana na inaleta tishio kubwa kwa afya ya umma.

WHO na UNODC watoa ripoti kuu kuhusu dawa zilizochafuliwa, wakitaka hatua za haraka kuokoa maisha

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na lile la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), kwa pamoja wametoa ripoti ya kihistoria inayoonesha matokeo muhimu kuhusu tishio la kudumu na linaloweza kuepukika la dawa zilizoharibika, ambazo zimesababisha vifo na kudhoofisha afya ya maelfu ya wagonjwa, hasa watoto, kutokana na matumizi ya dawa zenye viwango vya juu vya kemikali zenye sumu.

Taarifa hiyo iliyotolewa na mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa huko Jijini Geneva Uswisi imesema kuwa katika kipindi cha miaka 90 iliyopita, matukio 25 yaliyothibitishwa ya uchafuzi wa viambato yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1300 duniani kote, wengi wao wakiwa ni watoto. Matukio haya hutokea mara kwa mara kutokana na upungufu wa mfumo katika mnyororo wa usambazaji wa viambato vya dawa, na yameathiri zaidi watu wa nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ambako usimamizi wa udhibiti na upatikanaji wa dawa salama ni mdogo.

Ripoti hii inayoitwa, "Dawa zilizochafuliwa na uadilifu wa mfumo wa usambazaji wa viambato vya dawa”, inaangazia janga kubwa la kiafya linaoendelea: uchafuzi wa dawa kwa kemikali hatari za viwandani, hasa Diethylene glycol (DEG) na Ethylene glycol (EG).

Kemikali hizi hutumika kama viyeyusho vya viwandani na viowevu vya kuzuia kuganda, lakini zinaweza kusababisha madhara makubwa ya kiafya na hata vifo pindi zitakapomezwa, hata kwa kiwango kidogo hasa kwa watoto. Mara nyingi, hubadilishwa kinyume cha sheria badala ya viambato salama vya dawa kama Propylene glycol, Glycerin, na Sorbitol, vinavyotumika katika utengenezaji wa dawa mbalimbali, zikiwemo za kikohozi na Paracetamol kwa watoto.

Tangu Oktoba 2022, WHO imetoa Tahadhari 7 za bidhaa za matibabu kuhusu makundi mbalimbali la dawa za maji zenye uchafu, nyingi zikiwa zinalengwa kwa matumizi ya watoto na kusambazwa katika nchi zenye kipato cha chini. WHO pia imetoa Tahadhari 2 kuhusu kemikali za hifadhi zilizo ghushi zinazodaiwa kuwa na ubora wa viwandani wa dawa.

Kisa kimoja kibaya sana kilitokea nchini Gambia, ambako takriban watoto 66 walipoteza maisha, kikifuatiwa haraka na matukio mengine nchini Indonesia na Uzbekistan, ambapo vifo vingine 268 viliripotiwa pamoja na tahadhari mbili zaidi kutoka WHO.

Matukio mengi ya hivi karibuni yanahusisha dawa za kioevu za kumeza za bei nafuu ambazo zinaweza kununuliwa bila agizo la daktari. Mara nyingi dawa hizi ziliuzwa mahususi kwa ajili ya watoto na ni dawa zilizosajiliwa na zinazopatikana katika maduka ya kawaida, maduka ya dawa au masoko yasiyo rasmi ya mitaani.

Matokeo muhimu

Ripoti inafichua jinsi mitandao ya kihalifu inavyotumia hali ya sintofahamu ya soko na mapengo ya udhibiti kuingiza kemikali hatari kama mbadala wa viambato halali. Matokeo muhimu ni pamoja na:

  • Matumizi ya kibandiko cha jina au lebo za kughushi na kubadilishwa kwa kemikali zenye sumu badala ya viambato halali vya dawa kama Propylene Glycol.
  • Uuzaji wa viambato vya kughushi kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kiditali.
  • Ukosefu wa usimamizi wa udhibiti kwa watengenezaji na wasambazaji wa viambato vyenye hatari kubwa.
  • Mapungufu katika ufuatiliaji wa bidhaa sokoni na mifumo ya utekelezaji katika nchi zinazotengeneza na kuingiza dawa.
  • Uhalifu wa makusudi, ikiwa ni pamoja na kughushi nyaraka na taarifa, unaosababisha matukio mengi ya uchafuzi.
  • Ukosefu wa uratibu wa kutosha kati ya mamlaka za udhibiti, forodha na vyombo vya usalama, jambo linalokwamisha uchunguzi wa haraka na mashtaka.

Wito wa hatua

Ripoti inatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti za kimataifa kufunga mapengo ya udhibiti, kuimarisha usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa viambato msaidizi na kuwalinda hasa watoto dhidi ya sumu hizi zinazoua.

WHO imekuwa mstari wa mbele kwa muda mrefu katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na bidhaa za matibabu duni na ghushi. Ripoti hii inasisitiza umuhimu wa mifumo thabiti ya udhibiti wa dawa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa salama, bora na zenye viwango vya juu.

Kwa upande wake, UNODC inaleta mtazamo wa jinai wa tatizo hili, ikionesha jinsi magenge ya kihalifu yanavyoghushi nyaraka, kutumia kemikali za viwandani na kutumia majukwaa ya kidijitali kuingiza kemikali hatari katika mfumo wa usambazaji wa dawa duniani. Hili linaonesha haja ya hatua za kijinai sambamba na hatua za udhibiti.

Ripoti inasisitiza uhitaji wa:

  • Mfumo thabiti wa udhibiti na utekelezaji wa sheria.
  • Uzingatiaji wa viwango na sheria ulioboreshwa kutoka kwa watengenezaji na wasambazaji
  • Uwazi na ufuatiliaji wa mfumo wa usambazaji wa viambato.
  • Ushirikiano mkubwa kati ya mamlaka za afya, vyombo vya sheria na sekta binafsi.
  • Kuboresha ubadilishanaji wa taarifa na uratibu kati ya mamlaka husika kusaidia uchunguzi na mashtaka.
  • Kuweka adhabu kali dhidi ya ukiukwaji wa kanuni zinazohusu viambato vya dawa.
  • Kuimarisha uchunguzi na uwezo wa mashtaka kwa matukio ya makusudi ya uchafuzi na udanganyifu.
  • Ufuatiliaji thabiti baada ya soko kugundua na kukabili matukio ya jinai.
  • Mifumo bora ya kisheria na ya kiutendaji kukabili ughushi wa lebo, vyeti vya uchambuzi na muundo wa viambato.

Katika matukio mengi, uchafuzi wa dawa ni matokeo ya uhalifu wa makusudi. Kukabiliana na tishio hili kunahitaji ushirikiano kati ya wadau wote – vyombo vya sheria, maafisa wa forodha, waendesha mashtaka na taasisi za kupambana na rushwa. Ripoti inataka ushirikiano wa kimataifa, uwezo wa uchunguzi na matumizi ya mikataba ya kimataifa kama Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhalifu wa kupangwa kimataifa(UNTOC)

Ushirikiano wa Kimataifa

Ripoti hii ni matokeo ya ushirikiano wa pamoja kati ya mamlaka za udhibiti za kitaifa (NRAs) na wadau wa afya wa kimataifa. Maendeleo yake yaliwezeshwa na msaada wa ukarimu kutoka kwa mfuko wa Fleming Fund na Shirika la Gates Foundation.

WHO na UNODC wanatoa shukrani za dhati kwa wadau wote waliochangia katika kazi hii muhimu, hasa NRAs za Gambia, Indonesia, na Pakistan, ambao uzoefu na mitazamo yao ilikuwa muhimu katika kuunda matokeo ya ripoti hii.

Soma ripoti kamili hapa