Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Timor-Leste yatokomeza Malaria; WHO yapongeza

Mwanamke na wavulana wawili wadogo wamesimama mlangoni mwa nyumba ya kijijini huko Timor Leste, wakiangalia nje. Jengo hilo limetengenezwa kwa chuma cha bati na matofali ya zege, huku majani mabichi yakionekana karibu.
Unifeed/Jorge Rodriguez Familia katika jumuiya ya Orlalan, Manatuto huko Mashariki mwa Timor-Leste.

Timor-Leste yatokomeza Malaria; WHO yapongeza

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limetangaza rasmi hii kuwa Timor-Leste haina tena ugonjwa wa malaria, mafanikio makubwa kwa taifa hilo changa ambalo lilianza juhudi za kitaifa kupambana na ugonjwa huo mara baada ya kupata uhuru mwaka 2002.

WHO imetoa tangazo hilo leo mji mkuu wa Timor -Leste, Dili, ikiwa ni ushahidi wa mafanikio ya taifa hilo la Kusini-Mashariki mwa Asia baada ya kutokomeza maambukizi ya malaria ya ndani kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo.

"WHO inawapongeza watu na serikali ya Timor-Leste kwa mafanikio haya makubwa," amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus. "Ushindi huu unaonyesha kuwa malaria inaweza kutokomezwa iwapo kuna nia ya kisiasa, mikakati sahihi, uwekezaji endelevu na juhudi za wafanyakazi wa afya."

Katika eneo la Kusini-Mashariki mwa Asia, Timor-Leste imekuwa nchi ya tatu kuthibitishwa kuwa haina malaria, ikifuata nyayo za Maldives (2015) na Sri Lanka (2016).

Malaria ilikuwa adui yetu mkubwa – Timor-Leste

WHO imesema mafanikio haya yametokana na hatua za haraka zilizochukuliwa na Wizara ya Afya ya Timor-Leste mwaka 2003 kuanzisha Mpango wa Taifa wa Malaria, ambao uliongoza mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwa kutumia mbinu za kisasa kama vipimo vya haraka, matibabu ya mseto na usambazaji wa vyandarua vyenye dawa.

“Tumeweza. Malaria ilikuwa adui yetu mkubwa – kimya lakini hatari. Kutoka visa 223,000 hadi sifuri – ushindi huu ni heshima kwa kila maisha yaliyopotea na kila maisha yaliyookolewa,” amesema Waziri wa Afya, Dkt. Élia António de Araújo dos Reis Amaral.

Ushirikiano wa kimataifa

Mafanikio haya pia yamechangiwa na ushirikiano wa karibu kati ya serikali, WHO, mashirika yasiyo ya kiserikali, wahisani, na jamii za wenyeji. Mfumo wa ufuatiliaji wa wakati halisi na huduma za afya zinazopatikana bila malipo kwa wote umewezesha kudhibiti na kuchunguza visa vya malaria kwa haraka, hata maeneo ya mipakani.

Kwa kutangazwa kuwa nchi isiyo na malaria, Timor-Leste imejiunga rasmi na kundi la jumla ya nchi 47 na eneo moja duniani zilizothibitishwa na WHO kuwa zimeondokana kabisa na ugonjwa huo hatari.