Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhila yasiyofikirika na njaa iliyokithiri yawakumba watoto na wenyeji Gaza - UN/WHO

Mtoto anayekabiliwa na utapiamlo mkali amelazwa katika hospitali ya Abdel Aziz Al-Rantisi katika Ukanda wa Gaza.
UN News
Mtoto anayekabiliwa na utapiamlo mkali amelazwa katika hospitali ya Abdel Aziz Al-Rantisi katika Ukanda wa Gaza.

Madhila yasiyofikirika na njaa iliyokithiri yawakumba watoto na wenyeji Gaza - UN/WHO

Msaada wa Kibinadamu

Vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati, Ukanda wa Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli kati ya  wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas na jeshi la Israeli tangu mwezi Oktoba mwaka 2023 imeleta madhila yasiyofikirika  kwa wananchi wa kawaida. Mashirika ya misaada yamekuwa yakieleza kuna changamoto lukuki ikiwemo ongezeko kubwa la vifo vinavyosababishwa na utapiamlo. Video zinazotumwa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa vinaonesha hali halisi huko Gaza, ikiangazia utapiamlo kwa watoto.  

Ndani ya moja ya hospitali Gaza, eneo la wapalestina linalokaliwa kimabavu na Israel. ambapo tangu tarehe 17 mwezi huu wa Julai imetangazwa kuwa vituo vya kuhudumia wale wenye utapiamlo mkali au unyafuzi vimejaa. Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO limerekodi vifo 21 vitokanavyo na utapiamlo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Hospitali zinaripoti ongezeko kubwa la wagonjwa wa utapiamlo, hasa miongoni mwa watoto wachanga, huku kukiwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa.

Katika hospitali ya watoto ya Rantisi iliyoko eneo la Al- Nasr, mtoto anafanyiwa uchunguzi na daktari, tumbo lake limevimba, mama yake anamvalisha mfuko mweusi wa nailoni ambao ndio kama nepi yakumsitiri mwanae akijisaidia.

Daktari Ragheb Warshagha mkuu wa magonjwa ya tumbo anasema, “Wagonjwa wenye hali mbaya wanawasili katika hospitali wakitakiwa kulazwa na kupatiwa matibabu stahiki. Tatizo ni kuwa mama zao wenyewe wanaugua utapiamlo na wanakosa maziwa ambayo ndio kirutubisho kikuu hususan kwenye uzito. Matokeo yake sasa ni kwamba watoto wanapata maambukizi makali na wakati mwingine wanakufa kutokana na kudhoofika, kutokuwa na kinga mwilini pamoja na lishe duni.”

Wodini, mtoto Sham Maqattah analia kwa uchungu, anaugua utapiamko mkali, mwili wake umeonesha kudhoofika, ni mifupa na ngozi iliyojikunja, mdomo ameufungua huku kinywa kikionesha hakina hata mate. Mama yake anasema, “Kama unavyoona, hakuna maziwa, nami sina lishe ya kuniwezesha kumnyonyesha kwa kawaida. Afya yake imedhoofika, nimekuwa nikimleta hospitalini hapa kwa muda sasa kwa sababu ya hali yake. Tunatumai kwamba maziwa na nepi za watoto zitaruhusiwa kuingia, na vivuko vitafunguliwa ili waweze kuleta chakula. Kama akina mama, tunatazama watoto wetu wakiteseka, na inatuumiza.”

Mfanyakazi wa UNRWA huko Gaza akimkagua mtoto kama ana utapiamlo.
© UNRWA
Mfanyakazi wa UNRWA huko Gaza akimkagua mtoto kama ana utapiamlo.

Ufinyu wa vifaa tiba inawawia vigumu watoa huduma kuwasaidia watoto kama Hussam Al-Turamsi ambaye mikono yake yote miliwi inaonekana ilitobolewa na sindano na mmoja una njia ya kumuwekeaa dripu.

Mama yake Hussam Al-Turamsi anaema, “Kutokana na hali ilivyo sasa, hakuna maziwa, hakuna chakula, hakuna maji. Hii ni njaa. Siwezi kukidhi mahitaji ya mtoto wangu. Tulilazwa siku ya Ijumaa, na tangu wakati huo mwanangu amekuwa akiishi kwa kuwekewa drip za maji na hawezi kutembea.”

Tukirejea katika foleni ya kwenda kumuona daktari, baba mmoja wa watoto mapacha anasema, “Watoto wangu mapacha wanakabiliwa na utapiamlo mkali. Tumetafuta maziwa kwa ajili yao na tumekosa, hatujui la kufanya.”

Ukitoka hospitalini huko mitaani familia na watoto wanahaha kusaka chakula cha bure kinachotolewa katika majiko ya misaada kwenye kambi za wakimbizi wa ndani.

Video inamuonesha mama wa makamo, akiokota masalia ya chakula kilichomwagika chini baada ya mgao wa chakula kuisha. Machozi yakimtoka huku akionesha chakula hicho alichookota anasema kwa uchungu kwamba, “Hiki nichakula tena? Kinalika hiki? Nimekiokota kutoka chini ili nikawape wanangu wale. Watu jamani, hiki ni chakula? Kuweni na huruma, hurumieni watoto wetu. Mtuangalie- tuoneeni huruma.”

Watoto huko Gaza wakisubiri kwa matumaini ya kupata chakula.
UN News
Watoto huko Gaza wakisubiri kwa matumaini ya kupata chakula.

Hivi karibuni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA, Tom Fletcher, alinukuliwa akisema kuwa “Chakula kinaisha na wale wanaoenda kusaka msaada wa chakula wapo hatarini kupigwa risasi. Watu wanakufa wakijaribu kuwapatia mlo familia zao.”

Hata hivyo hili haliwafanyi watu kutotoka kwani kukaa ndani bila chakula nako ni kifo.  Miongoni mwao ni Bassam Dawood.

“Nimekuja sokoni, sijakuta chakula wala kinywaji. Tunatoa wito kwa ulimwengu kuishinikiza Israeli kuruhusu msaada kuingia Gaza. Kufungwa kwa vivuko vya kuingiza misaada ndiyo sababu ya sisi kuteseka na njaa. Tuna watoto na wazee. Sisi, kama wanaume, tunaweza kuvumilia, lakini watoto hawawezi. Tunatoa wito kwa ulimwengu wote kuwaokoa watoto wetu ili waweze kukua na afya.”

Nour Sobh,  anasaka angalau kilo moja ya unga.

“Tangu asubuhi natafuka kilo moja ya unga na sijapata katika eneo lote la mji wa Gaza. Njaa inawatafuna watoto wetu, wanalala bila kula kitu. Nilitoka asubuhi kutafuta mkate, mke wangu amelazwa hospitalini. Kwa saa kadhaa nimekuwa nikitafuta chakula na sijapata kitu chochote.”

Watoto wakisubiri chakula huko Gaza.
Children wait for food in Gaza.
Watoto wakisubiri chakula huko Gaza.

Na kwa Ibrahim Abu N’meh simulizi yake ni ya kuambulia patupu, “Tunaishi kwenye njaa kali. Niliondoka nyumbani ili niweze kuwaletea chakula na sijapata chochote. Sina uwezo wakununua hata biringanya. Nahitaji kilo moja ya unga kila siku ili watoto wangu wale mkate. Nina nini leo? Nitakuwa na nini kesho? Sina chochote, na fedha kidogo niliyonayo haiwezi kununua chochote.”