Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maoni ya kisheria ya ICJ kuhusu wajibu wa nchi kukabili mabadiliko ya tabianchi

Wanaharakati wa hali ya hewa wanatoa maoni yao nje ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague.
© ICJ-CIJ/Frank van Beek
Wanaharakati wa hali ya hewa wanatoa maoni yao nje ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) huko The Hague.

Maoni ya kisheria ya ICJ kuhusu wajibu wa nchi kukabili mabadiliko ya tabianchi

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Leo Julai 23 jijini Geneva, Uswisi, kupitia maoni ya kihistoria ya ushauri, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imefafanua kwa mara ya kwanza wajibu wa kisheria wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na athari za kisheria zinazotokana na kushindwa kutekeleza wajibu huo. Maoni haya yametolewa kufuatia ombi la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Machi 2023, jambo linaloonesha kuongezeka kwa wasiwasi duniani kuhusu janga la tabianchi.

Mahakama imekubaliana kwa kauli moja kwamba nchi zina wajibu wa kisheria chini ya mikataba ya kimataifa na sheria za kimila kulinda mfumo wa tabianchi na mazingira dhidi ya madhara ya hewa chafuzi zinazotokana na shughuli za binadamu. Wajibu huu unahusu vizazi vya sasa na vijavyo, Mahakama imesisitiza.

“Wajibu Mkubwa” Chini ya sheria ya mikataba na kimila

ICJ imeeleza kuwa nchi zinatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kimazingira, zikiwemo mikakati ya kupunguza na kuhimili madhara ya tabianchi. Chini ya Mkataba wa Paris, nchi lazima ziwasilishe michango ya kitaifa (NDCs) inayobeba “nia ya hali ya juu kabisa” katika kukabili janga la tabianchi. Michango hii inapaswa kusaidia kwa dhati kufikia lengo la kuzuia ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto (1.5°C) ambalo Mahakama imethibitisha kuwa ndilo lengo la pamoja la kimataifa.

Mahakama pia imesisitiza umuhimu wa kanuni ya wajibu wa pamoja lakini wa viwango tofauti”, ambayo inamaanisha kuwa kila nchi ina wajibu wa kuchukua hatua, lakini nchi zilizoendelea na zilizo na uwezo zaidi ndizo zinapaswa kuchukua jukumu kubwa zaidi.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki inatoa maoni yake ya ushauri kuhusu Wajibu wa Mataifa kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi.
© ICJ-CIJ/Frank van Beek
Mahakama ya Kimataifa ya Haki inatoa maoni yake ya ushauri kuhusu Wajibu wa Mataifa kuhusiana na Mabadiliko ya Tabianchi.

Wajibu hauchangi tu kwa wanaomiliki mikataba

Mahakama imefafanua kuwa wajibu wa kimataifa wa kulinda mazingira haubadilishwi na kama nchi imeridhia mikataba ya tabianchi au la. Hata nchi ambazo si wanachama wa mikataba hiyo, bado zinafungwa na sheria za kimila  ikiwa ni pamoja na wajibu wa kuzuia madhara makubwa ya mazingira na wajibu wa kushirikiana kimataifa. Utekelezaji wa masharti ya mikataba kwa uaminifu na ukamilifu ni kigezo muhimu cha kutimiza wajibu huo.

Athari za kisheria kwa uzembe wa kimazingira

Kuhusu swali la pili lililowasilishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Mahakama imefafanua kuwa nchi inayoshindwa kutimiza wajibu wake wa kisheria na kusababisha madhara makubwa ya kimazingira hasa kwa nchi za visiwa vidogo au kwa vizazi vijavyo inaweza kuwajibika kimataifa. Uwajibikaji huo unaweza kujumuisha adhabu za kisheria, ikiwemo kutoa fidia au kushiriki katika jitihada za pamoja za kupunguza na kuhimili athari hizo.

Ijapokuwa Mahakama haikuhukumu nchi yoyote, imeweka msingi wa kisheria unaowezesha uwasilishaji wa madai dhidi ya nchi zinazoshindwa kuchukua hatua stahiki za kulinda mazingira.

Ushindi kwa watetezi wa haki ya tabianchi

Maoni haya yanachukuliwa kama ushindi mkubwa kwa mataifa ya visiwa vya Pasifiki na harakati zinazoongozwa na vijana zilizotafuta tafsiri ya kisheria kuhusu wajibu wa nchi katika kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Ijapokuwa si lazima kufuatwa kisheria, maoni ya ICJ yana uzito mkubwa kisheria na kimaadili, na yanatarajiwa kuathiri mazungumzo ya kimataifa, kesi za mazingira, na sera za kitaifa kuhusu tabianchi.

Maoni haya yanakuja ikiwa ni siku moja tu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres,  katika hotuba maalum kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, jana Julai 23 ametangaza kuwa dunia “imevuka hatua ya kutorejea tena nyuma” katika mabadiliko kuelekea nishati mbadala, na akazisihi serikali kuwasilisha mipango mipya ya ​ kabla ya mkutano wa tabia nchi wa COP30 utakaofanyika nchini Brazil mwezi Novemba. Amesema enzi za nishati ya kisukuku zinaelekea ukingoni.

Zaidi bofya hapa.