Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Jinamizi la kihistoria lazima likome mara moja Gaza – UN

Mwanamke na mtoto wakitembea katika mji ulioshambuliwa kwa bomu sana wa Khuza'a katika Ukanda wa Gaza.
© UN Women/Samar Abu Elouf
Mwanamke na mtoto wakitembea katika mji ulioshambuliwa kwa bomu sana wa Khuza'a katika Ukanda wa Gaza.

Jinamizi la kihistoria lazima likome mara moja Gaza – UN

Amani na Usalama

Ingawa mazungumzo ya kina yanaendelea kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka, hali ya kutisha huko Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli,  inaendelea kuzorota, huku operesheni za kijeshi zikisambaa na vifo vya binadamu vikiendelea kuongezeka kila saa.

Ni kauli ya Khaled Khiari, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa eneo la Mashariki ya Kati, Asia na Pasifiki  kutoka Idara ya Siasa na Ujenzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa, aliyoitoa mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama waliokutana leo kujadili hali Mashariki ya Kati, hususan hoja ya Palestina.

Mwanamke akiomboleza juu ya mjukuu wake aliyeuawa katika shambulio la anga kwenye nyumba yao huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF
Mwanamke akiomboleza juu ya mjukuu wake aliyeuawa katika shambulio la anga kwenye nyumba yao huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Bwana Khiari amesema operesheni kali za kijeshi za Israel huko Deir al Balah ambazo zimesababisha wakimbizi wa kipalestina kuongezeka tena, pamoja na mashambulizi ya moja kwa moja kwenye nyumba mbili za wageni za Umoja wa Mataifa, zimezidisha zaidi hali mbaya na kuzuia shughuli za kibinadamu.

Amesema takribani wapalestina 1,891 wameuawa Gaza tangu taarifa yake ya mwisho tarehe 30 Juni, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.

Takriban watu 294 waliripotiwa kuuawa wakati wakijaribu kuchukua msaada, ikiwemo katika maeneo ya karibu na vituo vya usambazaji wa misaada vilivyokumbwa na mashambulizi ya kijeshi.

Amesema vikosi vya Israel vimeendelea kutoa amri za kuhama, na hivyo kusababisha wakazi kulazimika kuhama mara kwa mara.

Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Riyad Mansour akihutubia katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.
UN Photo/Loey Felipe
Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Riyad Mansour akihutubia katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.

Palestina: Watoto Gaza wanakufa kwa njaa huku ‘israel ikiharibu kila kitu’

Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Riyad Mansour ameripoti kwamba siku ya Jumapili, mtoto  Razan mwenye umri wa miaka minne alipambana kadiri alivyoweza, lakini mwili wake ulidhoofika na akafariki kutokana na utapiamlo.

Kama hiyo haitoshi, jana Jumanne, Yousef mwenye umri wa wiki sita alifariki kwa njaa, na alikuwa miongoni mwa watu 15 waliokufa kwa njaa katika saa 24 zilizopita huko Gaza.

“Israel imeharibu kila kitu – maisha yao, nyumba zao, misikiti na makanisa, shule na hospitali, miundombinu yote ya maisha na hata makaburi,” amesema Balozi Mansour, akionya: “Lakini msikosee, lengo halisi ni Wapalestina milioni 2 waliobaki Gaza. Kwa Israeli, maangamizi yao ni sehemu ya mpango wa kuteka ardhi.”

Ameongeza kuwa mkutano wa kimataifa utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu kwa uratibu wa Saudi Arabia na Ufaransa ni fursa ya kipekee ya kubadilisha sheria ya kimataifa na makubaliano ya jumuiya ya kimataifa kuwa mpango wa kutekelezeka, na kuonyesha dhamira ya kweli ya kumaliza ukaliaji wa ardhi kwa mabavu na mzozo huu mara moja na milele.

Balozi Danny Danon wa Israel akihutubia katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.
UN Photo/Manuel Elías
Balozi Danny Danon wa Israel akihutubia katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Mashariki ya Kati, likiwemo swali la Wapalestina.

Israel ‘inafanya kazi ya Umoja wa Mataifa’ – Inafanya Mashariki ya Kati kuwa salama zaidi

"Israel inafanya Mashariki ya Kati kuwa salama zaidi kwa kila mtu anayethamini amani na utulivu," amesema Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Danny Danon.

Ameongeza kuwa,  "kwa maneno mengine, tunafanya kazi ya Umoja wa Mataifa huku Israel ikivunja mitandao ya kigaidi na kulinda maisha ya wasio na hatia."

"Umoja wa Mataifa unafanya nini?" amehoji. Akitaja kuwa Umoja wa Mataifa unashikilia ajenda yake ya kisiasa, unalinda upendeleo wake, na kutetea mashirika ambayo kwa muda mrefu yameacha kuwa na msimamo wa kati, aliendelea  kukosoa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA).

Akipuuza takwimu zilizotolewa na ofisi hiyo — zikiwemo zile za vifo vya raia na idadi ya malori yanayopeleka chakula na dawa Gaza — kama "zinazopotosha hali halisi," amesema kuwa Israel haina budi kuchukua hatua.

Mamia ya wafanyakazi wa OCHA wanapitia mchakato wa ukaguzi wa kiusalama, na baadhi ya watendaji muhimu hawataruhusiwa kuhuisha vibali vyao “kutokana na ushahidi dhahiri wa uhusiano wa karibu na Hamas.”

Halikadhalika amesema kiongozi wa Ofisi ya OCHA katika eneo linalokaliwa la Palestina hatapewa upya kibali cha kuingia Israeli na analazimika kuwa ameondoka ifikapo tarehe 29 Julai.

"Imetosha na unafiki, umetosha na upendeleo, umetosha na kampeni isiyoisha ya kuliandika vibaya Taifa la Israel,” ametamatisha Balozi Danon.