Umwagiliaji kwa kutumia nishati ya sola waleta matumaini kwa wakulima wa Sidama, Ethiopia
Umwagiliaji kwa kutumia nishati ya sola waleta matumaini kwa wakulima wa Sidama, Ethiopia
Mradi unaoendeshwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Ethiopia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), ubalozi wa China wa kutumia nishati jadidifu ya jua kwa umwagiliaji, umeleta matumaini mapya kwa jamii za wakulima katika mkoa wa Sidama, kusini mwa Ethiopia.
Katika vijiji vya mkoa wa Sidama, ambako umeme wa gridi ya taifa haujafika, suluhu ya nishati ya jua kwa mara ya kwanza imekuwa mkombozi wa kweli kwa wakulima wadogo, kwani sasa wanaweza kumwagilia shamba bila kutegemea mvua au kuteka maji kutoka ziwani.
Tarehe 26 mwezi Novemba mwaka 2024, UNDP na wadau walikabidhi rasmi mfumo wa kisasa wa kusukuma maji kwa kutumia sola wenye uwezo wa kilowati 145 – ubunifu unaotarajiwa kuleta mapinduzi katika maisha ya maelfu ya watu.
Charu Bist, Naibu meneja wa mradi huo wa UNDP Ethiopia akiwa amehudhuria halfa hiyo ya makabidhiano anasema, " Ni heshima kushiriki katika hafla hii muhimu ya makabidhiano hapa Hawassa, mkoa wa Sedama nchini Ethiopia. Upatikanaji wa nishati nafuu, safi, na mbadala unasalia kuwa kipaumbele kikuu kwa Ethiopia. Na leo, tunafanya majaribio hapa Sedama wa uwekaji wa mfumo wa umwagiliaji wa mradi wa jua wa kilowati 145 ambao unasaidia zaidi ya mashamba 750 ya wakulima wadogo.”
Kwa familia kama ya Eyob Ledamo, mradi huu haubadilishi tu kilimo, bali maisha ya kila siku.
“Tulikuwa tunavuna mahindi na kisha tunapanda viazi. Tulikuwa tunavuna mazao yetu ya kilimo kwa kusubiri msimu wa mvua ufike. Wakulima wengine walikuwa wakivuna mara 3 kwa mwaka kwa kuwa walitumia mifumo ya umwagiliaji wakati sisi hatufanyi hivyo kwa sababu njia pekee ya kupata maji ilikuwa ni kuteka maji kutoka ziwa Hawassa.”
Kwa miaka mingi, wakulima kama Petros Shiberu waliteseka wakitegemea maji ya ziwani kwa ndoo au madumu ya plastiki. Leo, hali hiyo imebadilika.
" kabla ya kuanzishwa kwa mradi huu tulikuwa tukisafiri hadi ufukweni mwa ziwa na kununua maji, lakini sasa ni matumaini yetu kuwa mradi huu utaturahisishia maisha yetu, kwani hapo awali tulikuwa tunavuna bidhaa zetu mara moja tu kwa mwaka kwa subira ya mvua.Mradi huu utatuwezesha kuvuna mara tatu hadi nne kwa mwaka na kutambua mbegu zinazoweza kuvunwa ndani ya miezi 3."
Mbali na mashamba binafsi, mradi huu pia umewezesha uhamishaji wa maarifa kwa kiwango kikubwa. Takribani maafisa 500 wa serikali na wataalamu wa nishati wamefundishwa kuhusu suluhu za nishati jadidifu kuhakikisha mradi unadumu kwa muda mrefu.