Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama la UN lapitisha azimio la kuimarisha njia za amani za utatuzi wa migogoro

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe wake wa kulinda amnai nchini DRC, MONUSCO, wakiwa doria mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini. (Picha: Maktaba)
© MONUSCO/Aubin Mukoni Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kwenye ujumbe wake wa kulinda amnai nchini DRC, MONUSCO, wakiwa doria mjini Goma, jimboni Kivu Kaskazini. (Picha: Maktaba)

Baraza la Usalama la UN lapitisha azimio la kuimarisha njia za amani za utatuzi wa migogoro

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne Julai 22,  limepitisha kwa kauli moja rasimu ya azimio linalolenga kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani, azimio lililopitishwa wakati wa kikao cha ngazi ya mawaziri wa nchi wanachama wa chombo hicho.

Akihutubia Baraza hilo baada ya kupigwa kwa kura ya kupitisha rasimu hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema, “duniani kote tunashuhudia kupuuzwa kabisa — au hata ukiukwaji wa moja kwa moja — wa sheria za kimataifa, zikiwemo sheria za kimataifa za haki za binadamu, sheria za kimataifa za wakimbizi, sheria za kimataifa za kibinadamu, na hata Katiba ya Umoja wa Mataifa yenyewe, bila kuwapo uwajibikaji wowote.”

Ghamara ya mashambulizi ni kubwa kuliko inavyodhaniwa

Guterres amesema gharama ni kubwa mno — ikipimwa kwa maisha ya watu, jamii zilizosambaratishwa, na maisha ya baadaye yaliyopotea. “Hatuhitaji kuangalia mbali zaidi ya kile kinachoendelea Gaza — maangamizi na vifo vya kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika nyakati za hivi karibuni.”

Aidha ameeleza kuwa kwa kuwa operesheni za kijeshi za Israel zinaendelea kushamiri na maagizo mapya ya kuhama yakitolewa huko Deir al-Balah, ukanda wa Gaza unaokaliwa kimabavu na Israeli, uharibifu unaongezeka juu ya uharibifu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mjadala wa wazi wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani 22 Julai 2025.
UN /Manuel Elias Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia mjadala wa wazi wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani 22 Julai 2025.

Hata majengo yasiyopaswa kushambuliwa, yanashambuliwa

“Nimeshtushwa kwamba majengo ya Umoja wa Mataifa yameshambuliwa — yakiwemo ya Ofisi ya Huduma za Miradi ya Umoja wa Mataifa (UNOPS) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), ikiwa ni pamoja na ghala kuu la WHO’” amesema Katibu Mkuu.

Amesema mashambulizi hayo yalifanyika licha ya kwamba pande zote zilipewa taarifa kuhusu maeneo ya majengo hayo. “Majengo haya ni muhimu na yanapaswa kulindwa chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu — bila ubaguzi wowote.”

“Amani ni uamuzi. Na dunia inatarajia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusaidia mataifa kufanya uamuzi huo,” ameeleza Guterres, akieleza kuwa Baraza hilo katikati ya muundo wa dunia wa amani na usalama.

Amesema “kuanzishwa kwake kulitokana na ukweli mmoja mkubwa. Ushindani kati ya mataifa ni hali halisi ya kijiografia. Lakini ushirikiano — uliojengwa juu ya maslahi ya pamoja na manufaa ya wengi — ndio njia endelevu ya kuelekea amani.”