Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP na Mfuko wa CRDB Tanzania wafundisha wanawake 300,000 kuhusu Soko Huru la Afrika

Mratibu Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara (kulia), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa CRDB, Tully Esther Mwambapa, wakati wa kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya pande mbili.
UN News
Mratibu Mkazi wa UNDP Tanzania, Shigeki Komatsubara (kulia), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa CRDB, Tully Esther Mwambapa, wakati wa kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya pande mbili.

UNDP na Mfuko wa CRDB Tanzania wafundisha wanawake 300,000 kuhusu Soko Huru la Afrika

Na Assumpta Massoi - New York, Marekani
Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mfuko wa CRDB kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP nchini Tanzania wamefanikiwa kuwawezesha wanawake zaidi ya 300,000 nchini humu kupata mafunzo ya kuuza bidhaa zao katika Soko Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), lengo likiwa ni kuwaunganisha wanawake katika uchumi wa kikanda na kimataifa.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa CRDB Tully Esther Mwambapa, amesema kuwa programu hiyo inalenga kuwawezesha wanawake kwa kuwapatia maarifa, mbinu, na rasilimali zitakazowawezesha kufikia masoko mapya na kukuza biashara zao.

Utekelezaji wa SDG17

Ushirikiano kati ya UNDP Tanzania na CRDB Foundation unasaidia katika utekelezaji wa Ajenda ya 2030.Ask ChatGPT
UN News
Ushirikiano kati ya UNDP Tanzania na CRDB Foundation unasaidia katika utekelezaji wa Ajenda ya 2030.Ask ChatGPT

Ubia kati ya UNDP Tanzania na Mfuko wa CRDB nim fano wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, hususan lengo namba 17 linalotaka ubia kati ya taasisi za kimataifa na kitaifa ambapo kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres huwezesha uwekezaji katika sayansi, takwimu, teknolojia, na mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa.

"Tumeamua kushirikiana na Umoja wa Mataifa kwa sababu tuliona wanawake wengi Tanzania hawajanufaika vya kutosha na soko hili jipya la Afrika. Kupitia ushirikiano huu, tumeweza kuwafikia wanawake zaidi ya laki tatu na kuwapatia mafunzo," amesema Bi. Mwambapa.

Mafunzo yanayotolewa ni pamoja na mbinu za kufungasha bidhaa, uuzaji na uwasilishaji wa bidhaa kwa wateja wa kimataifa, pamoja na uelewa wa mahitaji ya masoko ya nje. Aidha, wanawake wanafundishwa kuhusu ujasiriamali na kujiamini kama wajasiriamali waliokomaa.

"Tunawaambia wanawake kuwa wao tayari ni jasiri, na bidhaa zao ni bora. Kinachohitajika ni ujasiri wa kutoka na kuuza nje ya mipaka ya Tanzania," ameongeza.

Mradi wa Funguo

Mbali na kuwawezesha wanawake waliopo kwenye biashara, Mfuko wa CRDB pia inalenga vijana wenye kampuni changa kupitia programu maalum iitwayo "Funguo". Kupitia programu hiyo, vijana wanapatiwa mafunzo ya kifedha, uendeshaji wa kampuni, na mbinu za kuvutia wabia wa ndani na nje ya nchi. Mfuko wa CRDB hutoa dhamana ya mkopo kwa vijana hawa ili waweze kupata mikopo nafuu ya kuendeleza biashara zao.

"Funguo inalenga kuwawezesha vijana kuwa viongozi wa kampuni kubwa kesho. Kupitia mikopo ya masharti nafuu, wanaweza kununua vifaa, kukuza biashara na kuvutia wawekezaji," amesema Bi. Mwambapa.

Changamoto zitokanazo na mafanikio

Kwa upande wa mafanikio ya Mfuko wa CRDB, Bi. Mwambapa ameeleza kuwa ushirikiano na Serikali kupitia wizara na taasisi mbalimbali umechangia kwa kiasi kikubwa. Alitaja Taasisi ya Sayansi na Teknolojia kama mshirika muhimu katika kuchambua ubunifu wa vijana waliowezeshwa.

"Benki ya CRDB yenye matawi kote nchini imesaidia pia kusogeza huduma karibu na wananchi. Serikali za mitaa, wilaya na mikoa zimeshirikiana nasi kikamilifu baada ya kuona faida za moja kwa moja kwa wananchi," amefafanua.

Hata hivyo, Bi. Mwambapa hakusita kueleza changamoto zilizopo. Mojawapo ni ongezeko kubwa la mahitaji ya huduma kuliko uwezo wa sasa wa taasisi. Vilevile, gharama za kuwasaka wanufaika vijijini na mikoani ni kubwa.

"Tunawashukuru Maafisa Maendeleo waliotusaidia kuwafikia wanawake vijijini. Hata hivyo, tunahitaji wabia zaidi wa kuwekeza katika dhamana ili wanawake wengi zaidi waweze kunufaika," amehitimisha.

Tazama mahojiano yote hapa.