Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atangaza zama za kufifia kwa nishati ya kisukuku

Mwanamke aliyevaa sari yenye rangi nyingi anasimama kati ya safu za paneli za jua huko Bangladesh.
© UNEP/Reza Shahriar Rahman Mabadiliko ya kuelekea nishati safi, kama vile nishati ya jua, yanaongezeka kwa kasi duniani kote.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atangaza zama za kufifia kwa nishati ya kisukuku

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametangaza kuwa dunia “imevuka hatua ya kutorejea tena nyuma” katika mabadiliko kuelekea nishati mbadala, na akazisihi serikali kuwasilisha mipango mipya ya ​ kabla ya mkutano wa tabia nchi wa COP30 utakaofanyika nchini Brazil mwezi Novemba. Amesema enzi za nishati ya kisukuku zinaelekea ukingoni.

Katika hotuba maalum katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Bwana Guterres amenukuu kuongezeka kwa uwekezaji katika nishati safi na kupungua kwa gharama za nishati ya jua na upepo ambazo sasa zinashindana na nishati ya kisukuku.

“Mabadiliko ya nishati hayawezi kusimamishwa. Lakini mabadiliko haya bado hayatoshi kwa kasi wala kwa usawa,” amesema.

Hotuba hiyo iliyolenga “Wakati wa Fursa: Kuchochea enzi ya nishati safi” – ikiwa ni mwendelezo wa hotuba ya mwaka jana “Wakati wa Ukweli” – imetolewa sambamba na ripoti mpya ya kiufundi ya Umoja wa Mataifa inayotegemea mashirika ya kimataifa ya nishati na fedha.

“Fuata tu pesa,” amesema Guterres, akionesha kuwa dola trilioni 2 ziliwekezwa katika nishati safi mwaka jana – dola bilioni 800 zaidi kuliko zilizoelekezwa kwenye nishati ya kisukuku, na ongezeko la karibu asilimia 70 ndani ya muongo mmoja.

Usafishaji wa paneli za sola nchini Niger
© UNCDF/Adam Rogers Usafishaji wa paneli za sola nchini Niger

Mabadiliko ya uwezekano

Guterres  amenukuu takwimu mpya kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) inayoonesha kuwa sola, ambayo awali ilikuwa yenye gharama mara nne zaidi, sasa ni asilimia 41 nafuu kuliko nishati ya kisukuku.

Vivyo hivyo, upepo wa baharini sasa ni asilimia 53 nafuu, huku zaidi ya asilimia 90 ya nishati mbadala mpya duniani ikizidi hata chaguo la bei ya chini zaidi la nishati ya kisukuku.

Hili siyo tu mabadiliko ya nguvu. Ni mabadiliko ya uwezekano,” anasema.

Nishati mbadala sasa inakaribia kufikia uwezo wa nishati ya kisukuku duniani, na “karibu nishati yote mpya iliyojengwa” mwaka jana ilitokana na vyanzo safi, akibainisha kuwa kila bara liliongeza zaidi ya nishati safi kuliko ya kisukuku.

Nishati safi haiwezi kusimamishwa

Bwana Guterres amesisitiza kuwa mustakabali wa nishati safi “siyo tena ahadi, ni ukweli.” Hakuna serikali, hakuna tasnia, wala kundi la maslahi maalum linaloweza kuizuia.

Bila shaka, wafuasi wa nishati ya kisukuku watajaribu – na tunajua ni umbali gani wataenda. Lakini nina imani zaidi kwamba watashindwa kwa sababu tumeshavuka hatua ya kutorejea.”

Anahimiza nchi kufungamanisha azma kubwa katika duru ijayo ya mpango mpya wa kitaifa wa kupunguza hewa chafuzi (NDCs inayopaswa kuwasilishwa ndani ya miezi michache. Bwana Guterres amezitaka nchi za G20  zinazosababisha asilimia 80 ya uzalishaji wa hewa ukaa  kuwasilisha mipango mipya inayolingana na lengo la 1.5°C na kuiwasilisha katika mkutano wa ngazi ya juu mwezi Septemba.

Malengo, ameongeza, ni pamoja na “kudhibiti matumizi ya nishati mara mbili na kuongeza mara tatu uwezo wa nishati mbadala ifikapo 2030” huku wakiharakisha “mabadiliko kutoka kwa nishati ya kisukuku.”

Katibu Mkuu António Guterres akitoa hotuba maalum kuhusu Hatua kwa Hali ya Hewa "Wakati wa Fursa: Kuongeza Chaji kwa Enzi Mpya ya Nishati".
UN Photo/Mark Garten Katibu Mkuu António Guterres akitoa hotuba maalum kuhusu Hatua kwa Hali ya Hewa "Wakati wa Fursa: Kuongeza Chaji kwa Enzi Mpya ya Nishati".

Uhuru halisi wa nishati

Katibu Mkuu pia ameeleza hatari za kiusalama za utegemezi wa nishati ya kisukuku.

Tishio kubwa zaidi kwa usalama wa nishati leo ni nishati ya kisukuku,” anasema, akirejelea misukosuko ya bei baada ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Hakuna kupanda kwa bei kwa mwanga wa jua. Hakuna vikwazo kwa upepo. Nishati mbadala inamaanisha uhakika wa kweli wa nishati… Uhuru wa kweli wa nishati. Na uhuru wa kweli dhidi ya kuyumba kwa nishati ya kisukuku.

Maeneo sita ya fursa

Bwana Guterres ameeleza maeneo sita ya fursa ya kuharakisha mabadiliko:

  1. NDCs zenye malengo makubwa
  2. Mitandao ya kisasa ya kusambaza umeme na hifadhi ya nishati
  3. Kukidhi mahitaji yanayokua kwa njia endelevu
  4. Mpito wa haki kwa wafanyakazi na jamii
  5. Mabadiliko ya sheria za biashara ili kupanua mnyororo wa usambazaji wa teknolojia safi
  6. Uhamasishaji wa fedha kwa masoko yanayoibukia

Hata hivyo, fedha ni kikwazo kikubwa. Afrika, ambayo ina asilimia 60 ya rasilimali bora za sola duniani, ilipokea asilimia 2 tu ya uwekezaji wa kimataifa wa nishati safi mwaka jana, amesema.

Ni dola moja tu kati ya tano zilizowekezwa katika nishati safi ndani ya muongo mmoja iliyokwenda kwa nchi zinazoendelea (isipokuwa China). Fedha hizi lazima ziongezeke zaidi ya mara tano ifikapo 2030 ili kuendelea na lengo la nyuzi joto 1.5 na kufanikisha upatikanaji wa nishati kwa wote.

Bwana Guterres anahimiza mageuzi ya mfumo wa fedha duniani, kuimarishwa kwa benki za maendeleo za kimataifa, na msamaha wa madeni, ikiwemo ubadilishanaji wa madeni kwa ajili ya hali ya hewa.

Zama za nishati ya kisukuku zinayumba na zinashindwa. Tuko kwenye enzi mpya ya nishati. Ulimwengu huo umo ndani ya uwezo wetu. Lakini hautatokea wenyewe. Wala si kwa kasi ya kutosha. Wala kwa usawa wa kutosha. Ni juu yetu… Huu ndio wakati wetu wa fursa.” amesema akihitimisha.