Mapendekezo manne ya Naibu Katibu Mkuu wa UN kuharakisha maendeleo ya Afrika
Mapendekezo manne ya Naibu Katibu Mkuu wa UN kuharakisha maendeleo ya Afrika
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, ametoa wito mzito wa kuchukua hatua za haraka na za kimfumo ili kuongeza kasi ya maendeleo barani Afrika, wakati wa mkutano wa wadau uliofanyika jana Julai 21 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.
Mkutano huo uliojadili matokeo na mapendekezo ya ripoti ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu utekelezaji wa ahadi za maendeleo ya Afrika, umebainisha hali ya kusikitisha: maendeleo kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yamesimama, na imani kwa serikali imepungua kwa zaidi ya asilimia 10 katika nchi 30 za Afrika katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Licha ya hali hiyo ya kusikitisha, Bi. Mohammed akihutubia mkutano huo kwa njia ya video anaeleza kwa matumaini na msisitizo mkubwa, akisema: “Afrika ina kila kitu kinachohitajika kubadilisha hali hii.” Kisha akaeleza mabadiliko manne makuu ambayo, yakitekelezwa kikamilifu, yanaweza kubadilisha mwelekeo wa maendeleo kuelekea ustawi wa watu na maendeleo endelevu katika bara hili.
1. Kudhibiti Mzunguko wa Fedha
Bi. Mohammed anasisitiza umuhimu wa mataifa ya Afrika kuwa na udhibiti wa uchumi wao. “Afrika inapoteza dola bilioni 90 kila mwaka kupitia mtiririko haramu wa fedha, nusu yake kupitia udanganyifu wa bei katika biashara, na dola bilioni 68 nyingine kupitia matumizi yasiyo na ufanisi ya umma,” anasema. Anaongeza kuwa fedha hizi zingeweza kujenga shule, hospitali, na miundombinu ya kidijitali na viwanda vyenye thamani ya kuongeza uzalishaji.
Anatoa wito kwa nchi za Afrika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuwekeza katika mifumo ya kidijitali kwa ufanisi zaidi wa kifedha, na kuhamasisha sekta binafsi kushiriki kwa nguvu.
2. Kuwekeza kwa Vijana wa Afrika
Kwa kuwa bara la Afrika linatarajiwa kuwa na vijana milioni 850 ifikapo 2050, Bi. Mohammed anaeleza kuwa huu ni wakati wa fursa ya kipekee ambayo haipaswi kupuuzwa. “Uwekezaji katika elimu ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), miundombinu ya kidijitali, na sera madhubuti ni jambo la lazima,” anasema na kusisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unatafsirika moja kwa moja kuwa ajira zenye staha na fursa kwa vijana.
3. Kujenga Mifumo Imara na Jumuishi
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasisitiza kuwa ulinzi wa kijamii si tu kuhusu kutoa msaada kwa walioko hatarini, bali ni msingi wa uthabiti unaowezesha jamii kujaribu, kuvumbua na kukua. Anasisitiza haja ya kuunganisha mifumo ya jadi ya kijamii na ile ya kisasa, pamoja na kujenga taasisi zinazowahudumia watu kwa uwazi, uwajibikaji na ufanisi.
“Mabadiliko ya tabianchi yanavuruga maisha na riziki. Migogoro inasababisha watu kukimbia makazi yao na kuhamisha rasilimali kutoka maendeleo kwenda kwa kukabiliana na migogoro. Tunahitaji mifumo inayoweza kustahimili misukosuko hii,” aliongeza.
4. Kufanya Uwajibikaji Uonekane kwa Wananchi
Akisisitiza uongozi wa ndani wa maendeleo ya Afrika, Amina J Mohammed anasema kuwa serikali za Afrika lazima ziongoze kwa uwazi na Umoja wa Mataifa uko tayari kuwa mshirika mwaminifu kwa kuhimiza majadiliano ya wazi, kuleta fedha, na kusaidia utungaji wa sera bora.
“Tumeona madhara ya kutibu dalili badala ya chanzo cha matatizo. Lakini pia tumeona mafanikio pale tunapofanya mambo kwa usahihi,” anasema.
Wito wa Kuchukua Hatua Sasa
Bi. Mohammed anahitimisha kwa kutoa wito wa wazi kwa viongozi na wadau wa maendeleo: “Tunaweza kuendelea na hali ile ile na kuacha Ajenda ya mwaka 2030 isitimie. Au tunaweza kuchochea mabadiliko ya kimfumo na kuisaidia Afrika kufikia mustakabali wake, mustakabali unaolingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na Ajenda ya mwaka 2063 ya Afrika.”
Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi kutoka serikali mbalimbali, asasi za kiraia, taasisi za kifedha na sekta binafsi, na unatarajiwa kuwa msingi wa sera na ushirikiano wa baadaye wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya maendeleo ya Afrika.