Wajitolea kisiwa cha Governors ili kuiga mfano wa Mandela
Wajitolea kisiwa cha Governors ili kuiga mfano wa Mandela
"Umekuwa ni uzoefu mzuri sana kufanya kazi kwenye mazingira haya katika siku ya Mandela. Nimeng ‘oa magugu kwenye miti nikiwa na timu nzuri sana," ni kauli ya Meritxell Font Vilaginés Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Andorra kwenye Umoja wa Mataifa aliyoitoa baada ya kushiriki kazi ya kujitolea kuadhimisha siku ya kimataifa ya Mandela Julai 18.
Bi. Vilaginés alikuwa miongoni mwa takriban watu 80 waliojitokeza Ijumaa kwenye Kisiwa cha Governors jijini New York, Marekani kushiriki shughuli za huduma kwa jamii kama njia ya kuadhimisha siku hiyo.
Wakiwa wamevalia glovu za kufanyia kazi shambani, wakisukuma matoroli na wakibeba nyaya za plastiki za kukarabati uzio, walitumia dakika 67 kufanya kazi za upambaji wa mazingira – ikiwa ni ishara ya miaka 67 ambayo Nelson Mandela alijitoa kwa utumishi wa umma na haki za binadamu.
Maeneo ya kujitolea kwa umma
Washiriki waliweka uzio wa urefu wa futi 350 karibu na eneo litakalojengwa Kituo cha Majawabu ya Mabadiliko ya Tabianchi, wakakusanya taka kwenye ekari 120 za kisiwa hicho, na wakapalilia miti ya matunda iliyo kwenye bustani ya The Open Orchard, sehemu ambayo mashine za kukata majani haziwezi kufikia kwa urahisi bila kuharibu mimea.
Bustani ya The Open Orchard, iliyoanzishwa na msanii Sam Van Aken, si bustani ya kawaida. Ina miti ya matunda 102 ya asili ya New York, ambayo ilikuwa karibu kutoweka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na kilimo cha kibiashara, lakini sasa inarejeshwa kupitia mbinu hii. Matunda yakikomaa, watalii wanaruhusiwa kuchuma na kuchukua.
Kwa kutumia matoroli yasiyopungua matano, maeneo karibu yote ya miti yalifanikishwa kusafishwa – isipokuwa moja, ambapo ndege wa porini aina ya Killdeer aliyekuwa akilinda mayai yake alionekana akijikinga ndani ya nyasi.
Kisiwa ni kisafi kuliko tulivyotarajia
Kando ya nguzo za uzio, Julie Okello kutoka Ofisi ya Usaidizi wa Ujenzi wa Amani alikuwa akifunga wavu pamoja na Mwakilishi wa Kudumu wa Angola kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Mateus Luemba ambaye amesema, “kila mtu ana furaha kuwa nje na kufanya kazi kwa pamoja.”
Balozi Msaidizi wa Afrika Kusini, Simon Cardy, alifurahishwa na hali ya mazingira lakini alikiri kuwa walitarajia kuona taka nyingi zaidi. Alitembea “kisiwa chote kwa nusu mfuko” wa taka, lakini alipata kitu cha kipekee – bango la dharura lililoachwa.
“Kwangu mimi Mandela anamaanisha vitendo..kusonga mbele, badala ya kutumia maneno tu na kukaa kwenye Baraza Kuu,” ni kauli ya Laura Mora Roger, Afisa kutoka Uwakilishi wa kudumu wa Andorra kwenye Umoja wa Mataifa .
Maryann Kithome kutoka Kenya amesema “kulinda mazingira ni muhimu sana kwa ajli ya vizazi vijavyo.”
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakfu wa Nelson Mandela aliyefika moja kwa moja kutoka Johannesburg, Afrika Kusini, Dkt. Mbongiseni Buthelezi, akatoa shukrani akisema, “makao yetu ni Johannesburg, na tuko hapa kusema asante kwenu nyote kwa kuwepo hapa mchana huu kumuenzi Mzee Mandela.”
Kisiwa cha Governors
Mradi huu wa huduma uliandaliwa na Ofisi ya Masuala ya Kimataifa ya Meya wa jiji la New York, nchini Marekani kwa kushirikiana na Idara ya Mawasiliano ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa pamoja na Ubalozi wa kudumu wa Afrika Kusini kwenye Umoja wa Mataifa, Wakfu wa Kisiwa cha Governors, Wakfu wa Nelson Mandela na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Kisiwa cha Governors kiko kwenye makutano ya mto wa Hudson na tawi lake la Mashariki na ni umbali wa takribani mita 730 ambapo feri inatumia chini ya dakika 10.