Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

SDGs si ndoto bali ni mpango wa kuboresha maisha ya wote, tuongeze kasi - Guterres

Katibu Mkuu UN António Guterres akizungumza katika jukwaa wakati wa Kongamano la Kisiasa la Ngazi ya Juu kuhusu Maendeleo Endelevu jijini New York.
UN Photo/Loey Felipe Katibu Mkuu António Guterres akihutubia sehemu ya Mawaziri ya Jukwaa la ngazi ya juu la Kisiasa kuhusu Maendeleo Endelevu.

SDGs si ndoto bali ni mpango wa kuboresha maisha ya wote, tuongeze kasi - Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa dunia kuongeza kasi na dhamira ya kweli katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayofikia ukomo wake 2030.

Akihutubia kwenye Mkutano wa mawaziri wa ngazi ya juu wa kisiasa, HLPF ulioanza leo jijini New York Marekani Guterres amesema ni asilimia 35 tu ya malengo ya SDGs ambayo yako katika mwelekeo sahihi au yanapiga hatua kwa kiasi cha wastani. Karibu nusu ya malengo hayo yanatekelezwa kwa mwendo wa polepole sana. Na asilimia 18 yanarudi nyuma. Wakati huo huo, uchumi wa dunia unazidi kudorora.

Tweet URL

Ni kwa mantiki hiyo Guterres amewaambia viongozi wa kimataifa, wataalamu wa maendeleo, na wawakilishi wa asasi mbalimbali, kwamba “mkutano huu unakuja wakati wa changamoto kubwa duniani ikiwemo vita na majanga ya asili– lakini pia fursa halisi ya mabadiliko.”

"SDGs si ndoto – ni mpango wa kweli wa kutimiza ahadi zetu kwa watu walio katika mazingira magumu, kwa kila mmoja wetu, na kwa vizazi vijavyo," amesema Guterres.

Ushirikiano wa kimataifa unazaa matunda

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa mkutano huu ni fursa ya kuhuisha ahadi ya pamoja ya kutokomeza umasikini, kulinda mazingira, na kuhakikisha ustawi kwa wote.

Pia ametaja mafanikio ya hivi karibuni katika mikutano ya kimataifa kama ishara ya kuwa ushirikiano wa kimataifa unaweza kuzaa matunda, ikiwemo:

  • Makubaliano ya kimataifa kukabiliana na majanga huko Geneva, Uswisi
  • Mkutano wa bahari huko Nice, Ufaransa
  • Mkutano wa Ufadhili wa Maendeleo huko Sevilla, Hispania.
Mstari wa mabango yenye rangi mbalimbali yanayoonyesha Malengo ya Maendeleo Endelevu UN nje ya Makao Makuu ya UN jijini New York.
UN News/Abdelmonem Makki Mabango katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa yakionesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs (Pichaya maktaba)

Tathmini ya Guterres ya malengo matano

Mkutano wa mwaka huu umejikita katika maeneo matano muhimu ambayo yana uwezo wa kuleta mabadiliko mapana katika malengo mengine. Malengo hayo ni:

Afya kwa wote (SDG 3)

Katibu Mkuu ameeleza kuwa janga la coronavirus">COVID-19 limeweka wazi pengo kubwa katika upatikanaji wa huduma za afya. Alitoa wito wa uwekezaji katika huduma ya afya kwa wote, inayozingatia msingi wa huduma ya msingi na kinga, hasa kwa walioko nyuma zaidi.

Usawa wa kijinsia (SDG 5)

Licha ya mafanikio, wanawake na wasichana bado wanakumbwa na ukatili, ubaguzi, na upungufu wa ushiriki wa kisiasa. Guterres amesisitiza umuhimu wa sera zenye haki, uwajibikaji, na ufadhili wa kweli kwa mipango ya kuwawezesha wanawake na wasichana.

Ajira zenye staha kwa wote (SDG 8)

Zaidi ya watu bilioni mbili wako kwenye ajira isiyo rasmi, huku vijana wengi wakiwa hawana kazi. Kupitia Mpango wa Kimataifa wa Kukuza Ajira na Ulinzi wa Jamii, nchi zinahamasishwa kuwekeza katika ujuzi, ulinzi wa kijamii, na sekta za ajira endelevu kama nishati safi.

Uhai chini ya bahari (SDG 14)

Bahari zinaathiriwa kwa kasi na uvuvi haramu, uchafuzi wa plastiki, na mabadiliko ya tabianchi. Guterres ametaka dunia kutekeleza kwa vitendo ahadi zilizotolewa kwenye Mkutano wa Bahari wa Nice ili kulinda viumbe wa baharini na jamii zinazotegemea bahari.

Ushirikiano wa kimataifa (SDG 17)

Ili kufanikisha maendeleo, Katibu Mkuu alihimiza uwekezaji katika sayansi, takwimu, teknolojia, na mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa ambao hautendei haki nchi zinazoendelea. Makubaliano ya Sevilla yanatoa mwelekeo mpya wa kuongeza nafasi ya fedha kwa ajili ya maendeleo.

Tusonge vipi mbele

Katibu Mkuu amehitimisha kwa kutoa wito wa kuendelea kujenga ushirikiano thabiti, kuweka fikra za muda mrefu kwenye maamuzi, na kujifunza kutoka kwa kila mmoja kupitia Tathmini za Kitaifa za Hiari kuhusu SDGs au (Voluntary National Reviews), ambazo sasa zimefikia zaidi ya 400.

"Kwa miaka mitano iliyobaki, ni wakati wa kugeuza cheche hizi za mabadiliko kuwa mwako mkubwa wa maendeleo kwa mataifa yote,”  amesema Katibu Mkuu.

Kwa mujibu wa Guterres, ni kwa hatua thabiti na mshikamano ndipo dunia inaweza kufanikisha SDGs – kwa ajili ya watu na kwa ajili ya sayari.

Katibu Mkuu UN Philémon Yang akizungumza katika jukwaa wakati wa Kongamano la Kisiasa la Ngazi ya Juu kuhusu Maendeleo Endelevu.
UN Photo/Loey Felipe Rais wa Baraza Kuu Philémon Yang akihutubia sehemu ya Mawaziri ya Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la Maendeleo Endelevu.

Tutumie tathmini za kitaifa kusongesha SDGs - Balozi Yang

Akihutubia washiriki, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Balozi Phillemon Yang amegusia tathmini za Kitaifa za Hiari au (VNR) akisema ni kielelezo cha umiliki wa kitaifa wa Malengo ya Maendeleo Endelevu na ushahidi wa maendeleo ambayo tayari yanaendelea kutokea. “Pia zinatoa maarifa ya thamani kuhusu jinsi Nchi Wanachama zinavyotekeleza ahadi za kimataifa kwa hatua za kitaifa. Nazipongeza nchi zote zinazowasilisha Tathmini zao mwaka huu.”

Balozi Yang amesema VNR zinaonesha jinsi takwimu, sera, na ujumuishaji vinavyosukuma utekelezaji wa Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. “Hapa ndipo matarajio ya dunia yanapokutana na vitendo vya kitaifa. Tathmini hizi zinastahili kupewa kipaumbele na kuungwa mkono kikamilifu.”