Athari ya ukame kwa watu na Uchumi duniani: Ripoti
Athari ya ukame kwa watu na Uchumi duniani: Ripoti
Kwa kuchochewa na mabadiliko ya tabianchi na shinikizo lisilokoma kwa ardhi na rasilimali za maji, baadhi ya matukio makubwa na yenye madhara zaidi ya ukame katika historia yameripotiwa tangu mwaka 2023, kwa mujibu wa ripoti mpya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Ripoti hiyo imeandaliwa na Kituo cha Kitaifa cha Marekani cha Kupunguza Ukame (NDMC) na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Jangwa (UNCCD), kwa msaada wa Muungano wa Kimataifa wa Mnepo dhidi ya Ukame (IDRA).
Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ni mshirika wa IDRA na linaendesha Mpango wa Usimamizi Jumuishi wa Ukame pamoja na Global Water Partnership ili kusaidia katika kutunga sera. WMO imekuwa ikihamasisha sera za kukabiliana na ukame kwa njia ya kutazama mbele badala ya kukabiliana wakati wa janga. UNCCD na NDMC ni wadau wa muda mrefu wa mpango huo (IDMP), pamoja na mashirika mengine 45. Aidha, WMO inafanya kazi kuimarisha ufuatiliaji wa ukame na tahadhari za mapema kupitia mpango wa Early Warnings For All.
“Ukame ni muuaji wa kimya. Unaingia taratibu, unamaliza rasilimali, na kuharibu maisha polepole. Makovu yake ni ya muda mrefu,” anasema Katibu Mtendaji wa UNCCD, Ibrahim Thiaw.
“Hii siyo ukame wa kawaida,” anasema Dkt. Mark Svoboda, Mkurugenzi wa NDMC na mwandishi mwenza wa ripoti. “Hili ni janga la kimataifa linaloendelea polepole—kubwa zaidi ambalo sijawahi kushuhudia. Ripoti hii inasisitiza umuhimu wa ufuatiliaji wa kimfumo wa jinsi ukame unavyoathiri maisha, riziki, na afya ya mifumo ya ikolojia tunayitegemea.”
Maeneo yaliyoathirika zaidi
Ripoti mpya inachambua taarifa kutoka serikali mbalimbali, sayansi na vyombo vya habari ili kuonesha athari katika maeneo yaliyoathirika zaidi na ukame. Inaonesha kuwa wanawake na watoto ndio walio hatarini zaidi.
Afrika
- Zaidi ya watu milioni 90 katika Afrika Mashariki na Kusini wanakabiliwa na njaa kali. Maeneo kadhaa yamekumbwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa.
- Nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambayo tayari huwa na ukame, zilikumbwa vibaya na ukame: watu milioni 68 walihitaji msaada wa chakula kufikia Agosti 2024.
- Katika Ethiopia, Zimbabwe, Zambia, na Malawi, mazao ya mahindi na ngano yameshindwa kuota mara kwa mara. Zimbabwe pekee, uzalishaji wa mahindi wa 2024 ulipungua kwa asilimia 70, bei ya mahindi iliongezeka mara mbili, na ng’ombe 9,000 walikufa kwa kiu na njaa.
- Somalia ilikadiria vifo vya watu 43,000 mwaka 2022 kutokana na njaa inayohusiana na ukame. Kufikia mwanzo wa 2025, watu milioni 4.4 (asilimia 25 ya wakazi) wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
- Zambia ilikumbwa na moja ya migogoro mikubwa ya nishati duniani baada ya Mto Zambezi kushuka hadi asilimia 20 ya wastani wake. Uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Kariba ulishuka hadi asilimia 7, na kusababisha mgao wa hadi saa 21 kwa siku, kufungwa kwa hospitali, viwanda na maduka ya mikate.
Mediterranea
- Hispania: Uhaba wa maji uliathiri kilimo, utalii, na matumizi ya nyumbani. Kufikia Septemba 2023, ukame wa miaka miwili na joto kali ulipelekea kushuka kwa asilimia 50 ya mazao ya mizeituni.
- Morocco: Idadi ya kondoo mwaka 2025 ilikuwa chini kwa asilimia 38 ikilinganishwa na mwaka 2016, hali iliyosababisha wito wa kifalme kufuta kafara za Eid.
- Türkiye: Ukame uliharakisha upungufu wa maji ya chini ya ardhi, na kusababisha mashimo makubwa hatari kwa jamii na miundombinu.
Amerika ya Kusini
- Bonde la Amazon: Viwango vya chini vya mito mwaka 2023-2024 vilisababisha vifo vya samaki wengi na pomboo walioko hatarini, huku upatikanaji wa maji ya kunywa na usafiri ukisitishwa kwa maelfu.
- Mfereji wa Panama: Viwango vya maji vilishuka na kupunguza idadi ya meli kutoka 38 hadi 24 kwa siku kati ya Oktoba 2023 na Januari 2024. Usafirishaji wa mazao ya soya ya Marekani ulipungua, na maduka ya Uingereza yakaripoti upungufu wa matunda na mboga.
Asia ya Kusini Mashariki
- Ukame ulivuruga uzalishaji wa mazao muhimu kama mchele, kahawa, na sukari. Katika 2023–2024, hali kavu nchini Thailand na India ilisababisha upungufu wa mazao na kupanda kwa bei ya sukari na bidhaa tamu kwa asilimia 8.9 Marekani.
Masomo na Mapendekezo
Ripoti inatoa wito wa uwekezaji wa haraka katika maandalizi dhidi ya ukame, ikijumuisha:
- Kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema na ufuatiliaji wa ukame na athari zake kwa wakati halisi.
- Suluhu za asili kama urejeshaji wa vyanzo vya maji na matumizi ya mazao ya asili.
- Miundombinu yenye mnepo, ikiwemo nishati isiyohitaji gridi kuu na teknolojia mbadala za maji.
- Mikakati jumuishi ya kijinsia, kuhakikisha wanawake na wasichana hawatengwi zaidi.
- Ushirikiano wa kimataifa, hasa katika kulinda mito ya mipakani na njia za biashara.