Guterres apongeza makubaliano ya amani kati ya Serikali ya DRC na kundi la AFC/M23
Guterres apongeza makubaliano ya amani kati ya Serikali ya DRC na kundi la AFC/M23
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amekaribisha kwa moyo mkufunjufu kutiwa saini kwa Azimio la Kanuni kati ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kundi la Alliance Fleuve Congo/Mouvement du 23 Mars (AFC/M23), huko Doha, Qatar.
Kupitia taarifa iliyotolewa New York, Marekani na msemaji wake siku ya Jumapili, Katibu Mkuu amepongeza hatua hii muhimu akisema kuwa makubaliano hayo yanayotaja sitisho la kudumu la mapigano linalotarajiwa kuanza kutekelezwa tarehe 29 mwezi huu, yanafungua njia kuelekea amani ya kudumu, usalama, pamoja na kurejea kwa wakimbizi na watu waliolazimika kuhama makwao kutokana na mzozo.
“Ni hatua ya matumaini inayoweza kurejesha hali ya kawaida kwa watu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” amesema Katibu Mkuu.
Aidha, ameyataka makundi yote yanayohusika kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa ahadi walizozichukua katika makubaliano hayo. Katibu Mkuu pia ametambua mchango mkubwa wa serikali ya Qatar kwa kuwezesha mazungumzo haya na kufanikisha kutiwa saini kwa azimio hilo.
“Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka za kitaifa, washirika wa kikanda na wa kimataifa ili kuunga mkono juhudi za kuleta amani, kuwalinda raia, na kuimarisha uthabiti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,” ametamatisha Guterres.
Makubaliano haya yanakuja wakati ambapo mashariki mwa DRC imekuwa ikikabiliwa na machafuko ya muda mrefu yanayohusisha makundi ya waasi, hali ambayo imesababisha maelfu ya watu kupoteza makazi yao.
Makubaliano ya awali
Wakati huo huo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani nchini DRC, MONUSCO umesema kwa mujibu wa makubaliano ya tarehe 27 Juni kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda yaliyotiwa saini mjini Washington, DC, nchini Marekani, mazungumzo ya amani yanatarajiwa kurejelewa ifikapo tarehe 8 mwezi ujao wa Agosti, kwa lengo la kufikia mkataba wa mwisho wa amani ifikapo Agosti 18.
Umoja wa Mataifa (UN), Muungano wa Afrika (AU) na wadau wengine wa kimataifa wameisifu Qatar kwa jukumu lake la uratibu wa mazungumzo hayo. Kwa upande wake, MONUSCO imeahidi kuendelea kutoa msaada wake katika kuhakikisha mafanikio ya juhudi za amani.
Sintofahamu yaendelea M23 ikipinga baadhi ya vipengele
Hata hivyo, hali ya sintofahamu inaendelea baada ya kundi la waasi la AFC/M23 kupinga kipengele cha makubaliano kinachohusu kuondoka kwa vikundi vya kijeshi katika baadhi ya maeneo.
M23 pia limeishutumu serikali ya DRC – ambayo wameita "utawala haramu" – kwa madai ya kuendelea kupeleka wanajeshi wake katika eneo la Uvira, jimboni Kivu Kusini.
Katika muktadha huu wa mvutano unaoendelea, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakishirikiana na wanajeshi wa serikali ya FARDC wanaendelea kujibu mashambulizi ya makundi yenye silaha kaskazini-mashariki mwa Djugu na kaskazini mwa Eringeti, katika jimbo la Ituri.
Mauaji dhidi ya raia
Katika jimbo la Kivu Kaskazini, MONUSCO imeripoti mauaji ya watoto 12 mnamo tarehe 12 Julai, wakati wa operesheni ya M23 dhidi ya kundi la FDLR–katika eneo la Katwiguru.
Zaidi ya hayo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa unafuatilia kwa karibu hali ya watu waliolazimika kuhama makazi yao karibu na Nyanzale, kufuatia amri ya M23 ya kuwahamisha raia mnamo tarehe 15 Julai.
MONUSCO imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha usalama wa raia na kuhimiza urejeaji wa hali ya utulivu, huku jumuiya ya kimataifa ikiweka matumaini kwamba makubaliano ya mwisho yatafungua ukurasa mpya wa amani katika eneo hilo.