Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kazi yetu siyo kuhamisha tu chakula – Idara ya Ugavi WFP Uganda

WFP Uganda Karamoja
WFP/Marc Hofer
WFP Uganda Karamoja

Kazi yetu siyo kuhamisha tu chakula – Idara ya Ugavi WFP Uganda

Msaada wa Kibinadamu

Licha ya changamoto za ufadhili, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini Uganda linasisitiza umuhimu wa usafirishaji katika kutoa msaada wa chakula. Sahir Aslam, Mkuu wa Idara ya Ugavi ya WFP Uganda, akizungumza kutokea huko huko Uganda katika maghala ya shirika hilo anafafanua kila kilomita moja ambayo msaada wa chakula wa WFP unasafiri.

“Kwenye mazingira ya sasa, ambapo bei ya chakula inapanda, mahitaji ya kibinadamu yanazidi kuongezeka, na bajeti zinapungua, shughuli za usafirishaji zimekuwa mkombozi wa maisha. Kama mnavyoona hapa nyuma yangu, mzigo huu una tani 2,000 za mahindi kutoka Tanzania. Bidhaa hii ni sehemu ya akiba ya kimkakati ya kituo cha kimataifa cha usimamizi wa bidhaa, kilicho katika eneo la kimkakati hapa Uganda kwa ajili ya shughuli za ndani ya nchi na mataifa jirani. Kutoka kwenye maghala haya, mahindi haya yatasafirishwa hadi maeneo ya mbali ambapo yatatumika kwa mpango wa lishe shuleni, msaada kwa wakimbizi, na kusaidia shughuli muhimu za WFP hapa Uganda.”

Bwana Aslam anaeleza umuhimu wa Idara hii ya Ugavi inayohusika na usimamizi na  usafirishaji wa misaada ya kibinadamu, idara anayoisimamia,

“Kazi yetu katika Idara ya Usafirishaji siyo tu kuhamisha chakula, bali pia kuchagua kwa uangalifu namna tunavyotumia rasilimali zetu. Kila dola, kila lita ya mafuta, kila kilomita tunayopitia lazima itumike kwa ufanisi mkubwa. Ufanisi huu tunaouleta kwenye shughuli za kila siku unamaanisha kuwa chakula kingi kinawafikia familia nyingi zaidi. Hata tukikabiliwa na ufadhili mdogo, lengo letu ni kuhakikisha matokeo makubwa zaidi na hiyo ndiyo inayotupa motisha kila siku.”

Mnamo mwaka wa 2024, WFP Uganda ilisafirisha tani 173,000 za chakula kwenda maeneo 545 ambayo ni magumu kufikika kote nchini Uganda.