Azimio la kanuni za msingi ni hatua muhimu kuelekea amani ya kudumu DRC- MONUSCO
Azimio la kanuni za msingi ni hatua muhimu kuelekea amani ya kudumu DRC- MONUSCO
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC,(MONUSCO) umekaribisha hatua ya kusainiwa wa azimio la Kanuni za Msingi kati ya serikali ya DRC na kundi lililojihami la (AFC/M23), ikisema ni hatua ya msingi katika mchakato wa kurejesha amani ya kudumu nchini humo.
Taarifa ya MONUSCO iliyotolewa Jumamosi mjini Kinshasa, inasema azimio hilo lililotiwa saini leo mjini Doha, Qatar, kwa usuluhishi wa serikali ya Qatar, linaonesha dhamira ya pande zote mbili kutumia mbinu za amani, kuanzisha usitishaji mapigano, pamoja na kuweka mfumo wa pamoja wa utekelezaji wake kwa vitendo.
“Hili ni tamko muhimu linaloonesha mabadiliko kuelekea kupunguza mvutano na kulinda raia waliodhurika vibaya na mzozo huu. Tunapongeza ahadi zilizotolewa na tunazitaka zitekelezwe kwa wakati na kwa nia njema,” amesema Bruno Lemarquis, Mwakilishi Maalum Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC na Kaimu Mkuu wa MONUSCO.
MONUSCO pia imepongeza dhamira ya pande zote kuhakikisha kurejea kwa hiari, kwa usalama na kwa utu kwa wakimbizi wa ndani na nje, kwenda katika maeneo yao ya asili au nchi wanakotoka.
Mazungumzo jumuishi
Ujumbe huo umetilia mkazo umuhimu wa mazungumzo jumuishi ili kushughulikia mizizi ya mzozo na kujenga amani ya kweli na ya kudumu.
Azimio hilo pia limeweka msisitizo mkubwa katika ulinzi wa raia na kuungwa mkono kwa usitishaji wa mapigano, likihusisha msaada kutoka MONUSCO pamoja na mifumo ya kikanda.
MONUSCO imerejea nia yake ya kuunga mkono kusitishwa kwa uhasama, hasa kupitia kuanzishwa kwa chombo madhubuti na cha pamoja cha ufuatiliaji.
Katika taarifa hiyo pia MONUSCO imetoa wito kwa pande zote kutekeleza ahadi zao kwa moyo wa uaminifu, kuweka mbele haki za binadamu, usalama na matumaini ya wananchi wa Kongo katika kila hatua ya maamuzi.
Ujumbe huo pia umetambua mchango mkubwa wa serikali ya Qatar, hususan Waziri wa Nchi anayehusika na Mambo ya Nje, Dkt. Mohammed bin Abdulaziz Al-Khulaifi, ambaye alikuwa na dhima muhimu katika kuwakutanisha wahusika wakuu wa makubaliano hayo.
MONUSCO imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka za kitaifa, wadau wa kikanda na wa kimataifa, katika kuendeleza juhudi za amani, maridhiano na utulivu nchini DRC, kwa mujibu wa mamlaka yake.
TAGS: Amani na Usalama/Afrika/DRC/M23/Qatar/MONUSCO